Wednesday, 25 September 2019

Messi Aumia Barca Ikishinda Kiduchu


BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi alipata maumivu wakati akianza kwa mara ya kwanza msimu huu katika mchezo, ambao Barcelona ilipata ushindi kiduchu wa mabao 2-1 dhidi ya Villarreal kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Messi, ambaye alikuwa akiponya majeraha ya nyama za paja, alibadilishwa mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kujitonesha tena.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina, alianza mchezo wake wa 400 wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga alipiga mpira wa kona uliomkuta Antoine Griezmann aliyepiga kichwa juu ya mwamba, kabla Arthur hajafunga na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Bao la kwanza la Barcelona lilifungwa katika dakika ya sita na Griezmann kabla Santi Cazorla hajaifungia Villarreal bao la kufutia machozi katika dakika ya 44.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Barca Ernesto Valverde alielezea maumivu ya Messi kuwa ni “tatizo dogo”, ambalo halitakawia kupona.

"Wakati kitu chochote kinapotokea kwa Messi, kila kitu kinasimama, sio tu uwanjani, lakini pia hata jukwaani mambo yanasimama, “alisema.

"Kama kuchukua tahadhari tuliamua kutofanya kitu hatari, kinadharia hakuna cha ziada, lakini kesho tutaona nini kinaendelea.”

Ingawa wako mbali na hali yao ya kawaida, kimsimamo Barcelona wamepanda hadi katika nafasi ya nne katika msimamo wa La Liga na kupunguza presha baada ya kuanaza msimu vibaya.

Baada ya maumivu, nahodha huyo wa Barca alipata matibabu nje ya uwanja kabla ya kuendelea hadi mapumziko.

Mshambuliaji huyo nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji Mfaransa wa Ousmane Dembele mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kwingineko, timu iliyopanda daraja ya Granada ilishika usukani wa La Liga – wakiwa pointi sawa na Athletic Bilbao na Real Madrid – baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Real Valladolid.

Real Madrid jana ilitarajia kucheza dhidi ya Osasuna wakati Bilbao waliopo mkiani watachezaji dhidi ya Leganes.

No comments:

Post a Comment