Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Elias
Kwandikwa amewakumbusha na kuwashauri Wafanyakazi wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhusu ufanisi wa kazi na hatua zinazopaswa
kuchukuliwa ili Mamlaka hiyo iweze kuongeza ufanisi wa kazi zaidi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa
Baraza la Wafanyakazi leo Jijini Dodoma Kwandikwa alisema Baraza
lina nafasi kubwa ya kuishauri Mamlaka juu ya maslahi bora kwa
Wafanyakazi.
“Naomba mjadili changamoto mnazokutana nazo mahala pa kazi
na katika utekelezaji wa mipango ili kuhakikisha mnatoa huduma bora kwa
wananchi, pia mjadili kuhusu makisio ya mapato na matumizi ya Mamlaka”alisema.
Pia alitaka Baraza hilo lisaidie katika kuleta maelewano
kazini kwani Rasilimali watu ni muhimu katika kusimamia Rasilimali
zingine na mipango katika Taasisi.
“Lazima tufanye kazi kwa umoja ili tuweze kupiga hatua, kwahiyo
uwepo wenu ni muhimu katika kujadiliana namna ya kuendeleza Taasisi kwa
kushirikiana”alisema.
Pia Kwandikwa alisema Baraza liweke mazingira ya kuongeza tija
kwa Watumishi wanaotimiza majukumu yao ambapo lengo ni kutambua mchango wao na
kuuthamini.
“Watumishi pia watimize majukumu yao kwa weledi kwa kuzingatia
sheria kanuni na taratibu za Utumishi wa umma”alisema.
Katika hatua nyingine Kwandikwa amewataka wafanyakazi wa
Mamlaka wafanye maandalizi juu ya ufunguzi wa Jengo la tatu la
abiria.
“Endeleeni kufanya uchunguzi juu ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza
baada ya kuanza matumizi ya jengo hilo,na mshirikishane na kudhibiti
mapema vihatarishi hivyo”alisema.
Pia aliwataka Watumishi sekta ya Anga kufanya kazi kwa weledi
ili kuboresha huduma za usafiri wa Anga ili kuongeza ushindani wa Kitaifa na
Kimataifa.
Pia alisisitiza kuwa ni muhimu Watumishi wa Mamlaka
kujitambua kuwa wanamchango katika kukuza pato la Taifa kutokana na
huduma wanazotoa ambazo zina mchango Mkubwa katika ujenzi wa Taifa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Mhandisi
Julius Ndyamukama kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi aliainisha baadhi ya
changamoto zinazoitatiza Taasisi kuwa ni maslahi duni kwa Wafanyakazi, uchache
wa Wafanyakazi pamoja na nyenzo za ufanyaji kazi kama magari ya Zimamoto.
Ambapo Kwandikwa alisema “Serikali itafanyia kazi changamoto
hizo ili kuhakikisha inaboresha sekta ya Usafiri wa Anga huku akitoa wa wito
kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa huku akisisitiza Maazimio ya
Baraza hilo yale ambayo yamekuwa changamoto yawe fursa ili yaweze kufanyiwa
kazi.
Mkutano huo wa 23 wa Baraza kuu la Wafanyakazi unafanyika kwa kwa
siku mbili katika ukumbi wa Takwimu Jijini hapa.
No comments:
Post a Comment