Na Mwandishi Wetu
GYM ya kisasa nchini ya Bodystreet imempatia ofa ya
masomo nchini Ujerumani mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Cosafa 2019 kwa
wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 iliyomalizika wiki iliyopita nchini
Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo, Mtendaji Mkuu na muanzilishi wa Bodystreet hapa nchini, Emma
Lehner Lyayuka alisema kuwa wameamua kumpatia Enekia Kasonga ofa ya masomo
nchini Ujerumani.
Pia mbali na kusoma masomo hayo ya michezo, pia
atakuwa akicheza soka katika timu ya wanawake ya FFC Wacker München ya Munich,
Ujerumani katika kipindi chote atakachokuwa akisoma.
Kasonga ambaye anaichezea Alliance Queens ya Mwanza,
alikuwa mchezaji bora katika mchezo wa Tanzania (Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini,
ambapo Tanzania ilishinda 2-0 na yeye alifunga bao moja. Pia alifunga jumla ya
mabao manne katika mashindano hayo.
Pia mchezaji huyo alifunga bao pekee la Tanzania
wakati ilipofungwa 2-1 na Zambia katika hatua ya makundi na kuifanya kumaliza
ya pili na kutinga nusu fainali.
Lyayuka alisema kuwa walimuona Enekia katika mchezo
wa Tanzanite na Afrika Kusini wa Kombe la Cosafa na walivutiwa sana jinsi
alivyokuwa akicheza na kuisaidia Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa
mwaka huu.
Alisema wanafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) ili kukamilisha taratibu mbalimbali za kumuwezesha mchezaji huyo
kwenda kusoma Ujerumani mafunzo ya kuanzia miezi mitatu hadi mwaka.
Wakati wa kutangaza ofa hiyo, Bodystreet waliwaonesha
waandishi wa habari vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kufanyia mazoezi,
ambavyo ni vya kwanza kuwepo nchini.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC)
Filbert Bayi alifanyishwa mazoezi kupitia vifaa hivyo, ambapo alikiri kuwa
vinabana muda na mtu anafanyishwa mazoezi katika viungo vyote.
Bayi alisema kuwa gym hiyo inasaidia sana kubana muda
kwani mtu hatumii muda mwingi, lakini mwili mzima unafanyishwa mazoezi kutokana
na kizibao anachokivaa wakati wa mazoezi.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Alliance na TFF ili
kuzungumzia ofa hiyo jana hazikufanikiwa baada ya baadhi yao simu zao
kutopatikana kabisa na wengine ziliita bila majibu.
No comments:
Post a Comment