Na Mwandishi Wetu
MABALOZI 42 wanaowakilisha Tanzania katika nchi
mbalimbali duniani wamelimwagia sifa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha
Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA).
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa akizungumza
kwa niaba ya wenzake baada ya kutembelea jengo hilo jana, alisema jengo hilo ni
kioo cha nchi na ndipo wageni wengi wa
nje ya nchi ndio wanafikia, ni kivutio kizuri.
“Hapa (JNIA)
ni kioo cha nchi. Tukiharibu mambo kwa kutoweka kaunta nzuri, tunaharibu
taswira ya nchi. Hii ndiyo Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) yetu. Lazima
izingatie viwango vya kimataifa, “alisema Slaa huku akisisitiza kutoogopa
kujifunza kutoka nje.
Dk. Slaa aliishukuru serikali kwa kuwapa mabalozi hao
fursa ya kutembelea jengo hilo kujionea kazi nzuri ya serikali ya awamu ya tano
iliyomalizia ujenzi wa jengo hilo.
Alisema kiwanja cha ndege ni sehemu ya kuingilia
nchini na kama kina huduma na vifaa bora, kama ulivyo huo wa JNIA Terminal 3 utashawishi
watu wengi kuingia nchini kupitia lango hilo.
Jengo hilo lina uwezo wa kupokea abiria milioni 6 kwa
mwaka wakati lile la Terminal 2 lina uwezo wa kuchukua watu milioni 2 tu, hivyo
ni hatua kubwa imepigwa kuhakikisha wasafiri wanahudumiwa kwa haraka na kwa
muda mfupi, tofauti na huko nyuma.
Awali, akizungumza wakati akiwakaribisha mabalozi hao
ambao wako nchini kuhudhuria mkutano wa Sadc Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya
Ndege nchini, Julius Ndyamukama alisema tayari makampuni 29 kati ya 41 ya usafi
yanaendelea na huduma mengi yao yakiwa ni ya wazawa.
Mabalozi hao walitembezwa kuanzia sehemu ya mwanzo ya
ukaguzi, sehemu ya uhamiaji, kuondokea abiria, daraja la kuingilia ndani ya
ndege, sehemu ya kufikia abiria na sehemu ya mizigo kabla ya kutoka nje ya
kiwanja hicho.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk Asha Rose
Migilo alimwambia mwandishi wetu kuwa kutokana na kazi nzuri wanayofanya mabalozi
nje ya nchi, watu wengi wakiwemo watalii wanataka kutembelea Tanzania, hivyo
kiwanja hicho kinaendana na wakati.
Alisema uwezo wake wa kuchukuwa watu wengi kwa wakati
mmoja, huduma kiwanja hicho kina hadhi ya hali ya juu na itasaidia sana kupokea
watu hao na kuwapokea bila tatizo.
No comments:
Post a Comment