Wachezaji wa Simba wakijifua kwa ajili ya nusu fainali ya SportPesa jijini Nakuru hivi karibuni. |
Na Mwandishi Wetu, Nakuru
SIMBA na
Singida United zimepania kufuzu fainali ya Mashindano ya SportPesa Super Cup
yanayofanyika katika Uwanja wa Afraha mjini hapa kwa kuzifunga timu za Kenya
ambazo wanakutana nazo kwenye nusu fainali leo.
Timu zote
zimefuzu nusu fainali kwa penalti kwenye
michezo yao ya robo fainali ambapo, Simba iliifunga Kariobang, ambao
waliwafungisha virago Yanga wakati Singida United ikaifunga AFC Leopard.
Simba itakuwa
ya kwanza kutupa karata yake kwa kucheza na Kakamega Homeboys saa 7:00 mchana
na Singida itawakabili mabingwa wa Kenya na mashindano ya SportPesa Super Cup,
Gor Mahia saa 9:15 alasiri.
Wakizungumzia
kwa nyakati tofauti, Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema mchezo wa
leo hautakuwa kama mchezo wa kwanza, kwani
hawakucheza vizuri na kuahidi timu yake itabadilika kwenye mchezo huo na
kufanya 'surprise'.
"Natarajia
leo tutacheza vizuri kila mtu aliona namna, ambavyo tulicheza kwa kiwango
kibovu, hivyo mchezo utakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chetu ," alisema
Djuma.
Naye nahodha
wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alisema "penalti sio nzuri ni kama
bahati nasibu, mchezo uliopita tuliingia tukiwa na nia ya kushinda katika
dakika 90, lakini sasa tunarejea tukiwa tumesahihisha makosa yetu na kuja na
mbinu mpya," alisema.
Kwa upande wa
kocha wa Singida United, Hemeda Morocco, ambaye anakutana na Gor Mahia alisema
itakuwa ni mechi tofauti na jinsi walivyocheza na AFC Leopards, hivyo
watabadilika ili waweze kushinda mapema japo hawapewi nafasi ya kufika fainali,
lakini hawana hofu.
"Mchezo huo
utakuwa tofauti na wa juzi, kwani nimepata kuwafahamu wachezaji kidogo sasa
baada ya mazoezi ya siku mbili tutacheza soka la tofauti na na mchezo wa juzi,
tunaiheshimu Gor lakini tuko tayari kupambana," alisema Morocco.
Pia
alisema hawataki kufika kwenye penalti
kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa juzi hivyo wamejipanga kumaliza kazi ndani ya
dakika 90.
Naye kocha msaidizi
wa Gor Mahia, Ottieno alisema: "Utakuwa mchezo mgumu kwani nimewaona
Singida United wanavyocheza ila tumejiandaa kutetea ubingwa wetu, ukitaka
kushinda lazima ufunge mabao tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,"
Simba na
Singida endapo zitashinda zitakutana kwenye hatua ya fainali itakayochezwa
Jumapili mjini hapa.
Mwaka jana
mashindano hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo
Gor Mahia iliifunga AFC Leopards na kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Everton
kwenye uwanja huo.
Bingwa wa
mwaka huu, ambali na kuondoka na Kombe, fedha taslimu, itapata fursa ya kwenda
England kucheza na Everton kwenye Uwanja wa Godson Park.
No comments:
Post a Comment