Na Mwandishi Wetu, Nakuru
WAKATI Simba imetinga fainali ya mashindano ya
SportsPesa Super Cup, swali ni je wameachana na makocha wao baada ya leo kuwa
katika jukwaani wakishuhudia timu yao ikishinda kwa penalti 5-4 katika mchezo
uliofanyika kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
Kocha Mkuu, Pierre Lechantre na kocha wa viungo wa
timu hiyo kutoka Morocco, jana walishuhudia pambano hilo kutokea jukwaani na
taarifa zilidai kuwa tayari wameachana na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba
wao.
Hatahivyo, taarifa zingine zilidai kuwa, Mfaransa
Lechantre ametofautiana na uongozi wa Simba na hivyo hawako tayari kumuongezea
mkataba mwingine, licha ya kuipatia mafanikio timu hiyo hadi kuipatia ubingwa
wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoukosa kwa karibu miaka mitano.
Hatahivyo, hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa tayari
kulizungumzia hilo, lakini walisema wangekuwa na kikao jana usiku na taarifa
kamili wangezitoa baadae.
Timu hiyo jana ilikuwa chini ya kocha msaidizi
Mburundi Masoud Djuma, ambaye ndiye akapewa mikoba hiyo.
Wakati
huohuo, Singida United ya Tanzania jana ilitolewa katika
mashindano ya SportPesa Super Cup baada ya kulambwa mabao 2-0 na mabingwa wa
Kenya katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Afraha mjini hapa.
Kwa kipigo hicho, Singida United wanaungana na
mabingwa wazamani wa Tanzania Bara, Yanga na JKU ya Zanzibar kuyaaga mashindano
hayo baada ya kutolewa katika nusu fainali, Yanga na JKU wenyewe walitolewa
katika robo fainali.
Mabao yote ya Gor Mahia yalifungwa na Meddy Kagere
katika kila kipindi na kuifanya timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza
dhidi ya Simba katika fainali itakayopigwa Jumapili kwenye uwanja huo.
No comments:
Post a Comment