Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) limeipa Tanzania uenyeji wa
kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya iaka 17 zitakazofanyika
mwaka 2019.
Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa Mkutano wa Kamati ya Utendaji ya
CAF uliofanyika jijini Zurich, Uswisi juzi jioni.
“Kamati ya Utendaji ya CAF imekubali ombi la Shirikisho la Soka
Tanzania la kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri
chini ya miaka 17 mwaka 2019, “ ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya CAF.
Tanzania iliwasilisha ombi hilo kwa msaada wa serikali kupitia
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya waziri wake, Fenella
Mukangara.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema
ni heshima kubwa kwa Tanzania kuandaa mashindano hayo ya Afrika.
“Kuandaa mashindano ya vijana ya Afrika ni hatua kubwa katika
maendeleo ya soka na itafungua milango kuandaa fainali za wakubwa za Mataifa ya
Afrika za Afcon mbeleni, ” alisema Malinzi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za
Afrika, ambapo imejihakikisha nafasi ya kushiriki fainali hizo kama mwenyeji
baada ya kusota kwa miaka mingi ikisaka kufuzu.
TFF ilisema kuwa katika kuandaa
kikosi bora cha kushiriki fainali hizo, Tanzania, mwezi ujao itaandaa
mashindano ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 na wachezaji bora wa
mashindano haya wataunda kikosi cha mwanzo cha taifa kuelekea fainali hizo za mwaka
2019.
TFF inamshukuru sana Rais Jakaya
Kikwete na Mukangara Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
kufanikisha maamuzi haya, na inaamini ushirikiano huu wa Serikali na wadau
wengine utafanikisha mashindano haya mwaka 2019.
“Kupitia mashindano haya
ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 huko jijini Mwanza yatasaidia
kuunda kikosi imara tena cha ushindano cha U17 mwaka 2019,”aliongeza
Malinzi katika ukurasa wake rasmi wa Twitter.
Malinzi tayari ameelezea mipango kabambe ya TFF ya kuunda kikosi
imara kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye
umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika Madagascar mwaka 2017.
Kwa sasa, TFF inaendesha program za vijana wenye umri chini ya
miaka 13 na 15 kwa ajili ya kupata timu imara za taifa za vijana kwa ajili ya
kufuzu kwa fainali hizo za Madagascar 2017, na zile za vijana za Afrika za
mwaka 2019.
Timu hizo zitakuwa zikipiga kambi na kucheza mechi kadhaa za
kirafi ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Botswana
na Afrika Kusini.
Katika mkutano huo wa CAF, Niger imepewa uenyeji wa kuandaa
fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakaofanyika mwaka 2019.
No comments:
Post a Comment