Tuesday, 13 March 2018

Zawadi Ngorongoro Marathon 2018 Zatangazwa

Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa Ngorongoro Marathon 2018 wametangaza zawadi, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha Sh milioni 1, ambazo zitafanyika Aprili 21.

Mkurugenzi wa mbio hizo, Meta Petro (pichani chini), akizungumza kwa njia ya simu kutoka Karatu, Arusha jana alisema kuwa, mshindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake, kila mmoja ataondoka na Sh milioni 1.

Alisema kuwa mshindi wa pili atapewa Sh 500,000, huku mshindi wa tatu kwa kila upande ataondoka na Sh 250,000.

Alisema kuwa pia kutakuwa na mbio za kujifurahisha za kilometa tano pamoja na zile za watoto wadogo za kilometa 2.5, ambazo hazina viingilio ili kuwawezesha watoto kujitokeza kwa wingi.

Alisema lengo la mbio za mwaka huu ni Kukimbiza Jangili, ambapo wanapiga vita mauaji ya wanyama kama vile tembo, simba, chui, twiga na wengine, ambao wamekuwa wakiuawa kwa sababu ya pembe, meno, kucha na ngozi zao.

Alisema wanyama kama tembo na faru wamekuwa wakiuawa kwa ajili ya biashara haramu ya pembe zao huku twiga na pundamilia wakiuawa kwa ajili ya nyama, na simba na chui wamekuwa wakiuawa kwa ajili ya ngozi zao.
Akielezea ada ya ushiriki, Petro alisema kuwa kwa Watanzania watakaokimbia kilometa 21 watalipa Sh 10,000 kwa fomu huku wageni watalipa dola za Marekani 50.

Alisema kwa wale watakaoshiriki kilometa tano kama timu, kuanzia mtu mmoja hadi watano, watalipia dola za Marekani 500, wakati mtu mmoja mmoja Mtanzania atalipia Sh 10,000 na asiye Mtanzania atalipa dola 10.

Wakati huohuo, Petro amesema kuwa bado wanasaka wadhamini kwa ajili ya mbio hizo, ambazo mbali na kupiga vita vya ujangili, pia zinatangaza vivutio vya utalii nchini.

Friday, 9 March 2018

Vitakavyojiri Kwenye DStv wikiendi hii!


Na Mwandishi Wetu
KWENYE Ligi Kuu ya England wikiendi hii ndani ya DStv, Timu mbili zilizobeba makombe mara nyingi England, zenye historia nzuri kwenye ligi ya Uingereza, zenye heshima kubwa kwenye historia ya Soka Uingereza na Duniani kwa Ujumla.

Ikumbukwe, mzunguko wa kwanza ndani ya Anifield timu hizi zilizotoka sare bila kufungana. Man United wakiwa nafasi ya pili wakahitaji ushindi kuendelea kuweka hai matumaini yao ya nafasi ya pili wakati Liverpool nao wakihitaji ushindi ili kuishusha Man United kwenye nafasi ya pili.

Hakika hii sio Game ya kukosa kabisa, kwa sh.69, 000 tu kifurushi DStv Compact
ndani ya Supersport 3 utawashuhudia kina Paul Pogba, Romelo Lukaku, Nemanja Matic, Anthony Martial wakipigania heshima ya Manchester United huku Mohamed Salah, Saido Mane, Emre Can, Frimino wakipigania kukamata nafasi ya pili.

Je hujajiunga na DStv?  wahi sasa Ofa ya THE PUNGUZO, burudika na miezi miwili bure kwa kununua Dekoda pamoja na Dish kwa sh.79, 000 tu!

DStv Kujiunga piga 0659 070707, na ukitaka kujihudumia piga *150*46# kisha fuata maelekezo. THE PUNGUZO na DStv!!

Thursday, 8 March 2018

Wanawake TAA Walivyosheherekea siku yao Dar

Wanawake wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo Machi 8, 2018 wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Mlimani City kwa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo kauli mbiu ni “Kuelekea uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake Vijijini”.
 Bi. Anna Myovela (kulia) na Bi. Linah Kidemi (aliyeinama) wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakicheza kwa furaha katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika Mlimani City kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Mgeni rasmi alikuwa ni Mke wa Rais, Bi. Janeth Magufuli, ambapo kauli mbiu ni “Kuelekea uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake Vijijini”.
 Wanawake wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakifurahia siku yao leo Machi 8, 2018 kwa kucheza ngoma, katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika Mlimani City kwa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo Kauli mbiu ni “Kuelekea uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake wa Vijijini”.
 Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni “Kuelekea uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini”, ambapo Wanawake wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo Machi 8, 2018 wakiungana na wenzao Mlimani City mkoani Dar es Salaam kuadhimisha siku hiyo.
Maandamano ya wanawake ya kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani yamefanyika leo Machi 8, 2018 kwa mkoa wa Dar es Salaam na kauli mbiu ni Kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini, ambapo pichani ni wanawake wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), nao waliungana na wenzao kusherehekea siku hiyo.

Tuesday, 6 March 2018

Madrid Yatangulia Robo Fainali Mabingwa Ulaya


PARIS, Ufaransa
MABINGWA wa Ulaya Real Madrid imetinga katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuifunga vinara wa Ligue 1 Paris St-Germain 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Parc des Princes.

Cristiano Ronaldo ndiye alikuwa kinara wa mchezo huo baada ya kutupia nyavuni moja ya mabao yaliyowezesha timu hiyo ya Hispania kushinda mechi zote mbili, nyumbani na ile ya ugenini.

Mabingwa hao watetezi wametinga robo fainali kwa kupata ushindi wa jumla ya mabao 5-2 baada ya kushinda 3-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizopita Hispania.
Kikosi cha Real Madrid.
Katika mchezo wa kwanza, ambapo walishinda 3-1, Ronaldo alifunga mara mbili huku jingine likiwekwa kimiania na Casemiro katika dakika ya 80.

PSG ilijikuta matatani baada ya kiungo wake, Marco Verratti kutolewa nje baada ya kupewa kadi ya pili ya njano, kabla Edinson Cavani hajafunga bao la machozi.
Kikosi cha PSG
Kwa PSG, ambao ina pointi 14 zaidi kileleni mwa msimamo wa Ligue 1, hii ni msimu wake wa pili mfululizo kutolewa katika hatua ya 16 bora huku ikiacha hatma ya kocha wake Unai Emery kuwa katika utata.

Timu hiyo ilishuka dimbani bila nyota wake majeruhi Mbrazil Neymar na haikusaidiwa na msaada wa Verratti, ambaye alitolewa katika dakika ya 66. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia alitolewa baada ya kumchezea rafu Casemiro katika kipindi cha kwanza na alioneshwa ya pili.

Simba Uso kwa Uso na Al Masry Uwanja wa Taifa


Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiikaribisha timu ya Al Masry ya Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika utakaoanza saa 12:00 jioni.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanaingia uwanjani wakiwa na ari ya ushindi ili kupunguza kazi katika mchezo wa marudiano, kwani Waarabu wana tabia ya kucheza kwa kujihami ugenini na nyumbani kushambulia sana.

Kocha wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre alisema anaifahamu Al Masry na timu nyingine za Misri kuwa ni timu zinazocheza soka la kujihami zikiwa ugenini, lakini nyumbani wanashambuliaji hivyo watajitahidi kuhakikisha wanapata ushindi nyumbani ili ugenini wawe na kazi nyepesi.

“Wachezaji Emanuel Okwi na John Bocco watakuwepo lakini sisemi tutaingia kwa staili gani bali tutacheza kutafuta ushindi kwa sababu timu zinazotoka nchi za Kiarabu zinatabia ya kucheza mchezo wa kujihami ugenini,” alisema Lechantre.

Naye nahodha wa timu hiyo, John Bocco alisema matokeo ya sare ya 3-3 ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United yasiwatie hofu waje kwa wingi kuishangilia timu yao, kwani wachezaji wanajua deni walilonalo kwao.
“Kocha amefanya kazi yake na sisi wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunapata ushindi, kwani ni muda mrefu Simba haijashiriki mashindano ya kimataifa hivyo mashabiki waje kwa wingi kuisangilia timu yao,” alisema Bocco.

Wakati Simba ikiongoza Ligi Kuu Tanzania Bara, wapinzani wao wanashika nafasi ya nne katika ligi nchini Misri.

Kocha wa Al Masry, Hossam Hassan atakuwa na kumbukumbu ya kipigo alichopata toka kwa Simba wakati akichezea Zamaleck mwaka 2003 baada ya kufungwa bao 1-0 Dar es Salaam na ugenini Simba ikafungwa bao 1-0 na kutolewa kwa penalti 3-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1.

Timu hiyo inamtegemea mshambuliaji raia wa Burkinafaso Aristide Bance ambaye amegeuka gumzo hapa nchini na kwenye mitandao ya kijamii.

Simba ilifuzu hatua ya awali kwa kuiondoa Gendermarie ya Djibout kwa mabao 5-0 wakati wapinzani wao Al Masry walifuzu kwa kuishinda Green Buffalo ya Zambia kwa mabao 5-2.
Kiingilio katika mchezo huo VIP A ni Sh 20, 000, VIP B ni Sh 15,000 na mzunguko Sh 5,000.

Baada ya mchezo wa huo wa leo, timu hizo zitarudiana siku 10 baadaye mjini Cairo, Misri na mshindi wa jumla ataingia kwenye mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi kwa kucheza na moja ya timu zilizotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu zinazoingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho hupewa dola za Marekani 150,000 (zaidi ya Sh milioni 300), ambazo huongezeka kila timu inaposhinda na kusonga mbele.

Bingwa wa Kombe la Shirikisho hupata Dola za Kimarekani 625,000 (zaidi ya Sh bil 1.5), mshindi wa pili wa Kundi hupata dola 239,000.

Yanga Yajiweka Matatani Mabingwa Afrika


Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika Yanga wamejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu kucheza hatua ya makundi baada ya kufungwa 2-1 na Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 Kwa matokeo hayo, mabingwa hao wa Tanzania Bara, sasa wanahitaji ushindi wa kuanzia angalau mabao 2-0 na kuendelea.

Katika mchezo wa jana wageni waliandika bao la kwanza katika dakika ya 11 kupitia kwa Lemponye Tshireletso aliifungia bao Township bao la kuongoza baada ya kupiga shuti kali nje ya meta 18 lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Obrey Chirwa aliisawazishia Yanga katika dakika ya 30 baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Tshishimbi.

Yanga walitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini wachezaji wake hawakuwa makini na  kukosa mabao.

Katika dakika ya tatu, wapinzani wa Yanga nusura wafunge baada ya Joel Morogorosi kutokuwa makini na mpira kuwahiwa na kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili.

Ibrahim Ajib alikosa bao katika dakika ya 25 baada ya kupiga mpira uliopaa juu ya lango la wapinzani wao hao kutoka Botswana.

Yanga ilianza kwa nguvu kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi kadhaa, ambapo katika dakika ya 48 nusura  wapate bao baada ya Gadiel Michael kushindwa kufunga baada ya kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango.

Timu hizo zitarudiana mjini Gaborone, Botswana Machi 17 katika mchezo wa utakaoamua timu ipi itinge hatua ya makundi huku Yanga ikiwa na kibarua kigumu zaidi.
Nahodha wa Yanga, Pius Buswita akizungumza baada ya mchezo huo jana alisema kuwa wapinzani wao walitumia vizuri nafasi walizopata, lakini na wao wanaweza kushinda katika mchezo huo wa ugenini.

 Kikosi cha Yanga: Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Said Ali, Kelvin Yondan, Papy Tshishimbi, Pius Buswita, Pato Ngonyani, Ibrahim Ajibu/Juma Mahadhi, Obrey Chirwa na Emmanuel Martine/Mwashiuya.

Sunday, 4 March 2018

Wakenya Waendelea Kutamba Kili Marathon

Wanariadha wakichuana katika mbio za Tigo Kili Nusu Marathon leo mjini Moshi.
Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAKENYA wameendelea kutamba katika mbio za Kilimanjaro Marathon kwa kilometa 21 na zile za kilometa 42 zilizofanyika leo mjini hapa na kushuhudiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe.

Katika mbio za kilometa 42, Wakenya wameshikilia nafasi 10 za kwanza kwa uoande wa wanaume na wanawake huku Failuna Abdil akiwa Mtanzania pekee aliyekuwemo katika nafasi tatu bora kwa upande wa wanawake katika mbio za kilometa 21 baada ya kushika nafasi ya pili kwa kutumia saa 01:13:52.

Waziri wa Habari,Utanaduni, Sanaa na Nichezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa amesononeshwa a matokeo ya mbio za Kilimanjaro Marathon baada ya Tanzaniaa mmoja tu kuwemo katika tatu bora kati ya washindi 20.

Katika mbio za kilometa 21, Failuna Abdi alimaliza wa pili nyuma ya Mkenya Flavious Kwamboka huku nafasi zingine zote katika 10 bora zikichukuliwa na Wakenya ambao walitawala pia mbio za wanaume za kilometa 21 kuanzia nafasi ya kwanza hadi 10.

Mbali na mbio hizo za kilometa 21, Wakenya pia walishika nafasi 10 za kwanza kwa upande wa wanajume na wanawake katika mbio za kilometa 42 zilizoanzia na kumalizikia kwenye Uwanja wa Ushirika mjini hapa.

Mwakyembe akizungumza baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo kwenye uwanja huo alisema kuwa lazima aseme ukweli na hayuko tayari kuwapaka mafuta wakati matokeo hayajamfurahisha baada ya nafasi zote za juu kuchukuliwa na Wakenya.

Aliwataja vijana wa Moshi kufanya mazoezi kwa bidii ili mwakani waweze  kulitoa taifa kimasomaso kwa kufanya vizuri katika mbio hizo na kutwaa fedha zote zinatolewa kwa washindi.

Mwakyembe alipongeza maandalizi mazuri ya mbio hizo ambazo ni kubwa kabisa nchini kwa upoande wa marathon.

Grace Kimanzi wa Kenya alimaliza wa kwanza katika mbio za kilometa 21 kwa kutumia saa 01:13:46 huku Failuna akitumia saa 01:13:52 huku mshindi wa pili tatu ni Mkenya Pauline Rkahenya aliyetumia saa 01:13:54 wakati kwa wanaume, Geofry Torotich wa Kenya alishinda mbio hizo kwa wanaume kwa kutumia saa 01:03:26 na Simon Muthon alikuwa wa pili kwa saa 01:03:29.

Mshindi wa tatu katika mbio za kilometa 21 kwa wanaume alikuwa Shadrack Korir aliyetumia saa 01:03:35, ambao walizawadia sh mil 2, mil 1 na 650,000 kwa upande wa wanawake na wanaume.

Katika mbio za kilometa 42, Cosmas Muteti alimaliza wa kwanza katika mbio hizo kwa kutumia saa 02:17:01, huku mshindi wa pili alikuwa Eikana Yego aliyetumia saa 02:19:25 na George Onyancha aliyetumia saa 02:20:25.

Mwaka huu jumla ya washiriki wa mbio zote za kilometa 21, 42 na zile za kujifurahisha za kilometa tano,walikuwa zaidi 11,000.


Friday, 2 March 2018

Lyimo, Anna Waahidi Makubwa TUGHE-JNIA


  Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gaudence Kadyango aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akitoa maelezo kwa wapigaji kura kwenye uchaguzi mdogo wa tawi hilo uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo Jengo la Kwanza la abiria(TBI).


 
Na Mwandishi Wetu
WENYEVITI Bw. Filbert Lyimo na Bi. Anna Myovela wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wameahidi makubwa katika kutetea haki za wanachama wao mara baada ya kuchaguliwa leo kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika katika ukumbi wa Transit uliopo Jengo la Kwanza la abiria (TBI).

Bw.  Lyimo aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TUGHE tawi la JNIA alisema atahakikisha anawawakilisha vyema wanachama kwa mwajiri, ikiwemo kutetea haki na maslahi yao ya kazi.


    Bw. Filbert Lyimo akijinadi katika nafasi ya Uenyekiti katika  uchaguzi mdogo wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) uliofanyika leo katika ukumbi wa Transit uliopo jengo la kwanza la abiria (TBI).


“Nashukuru kwa kunionesha ushirikiano nyie ndio mlionichagua mimi na sio mimi niliowachagua nyie, hivyo ninaahidi sintawaangusha nitakwenda kifua mbele kutetea haki zenu kwa mwajiri, na jambo la msingi tushirikiane ili kufanikisha haya ninayoyatarajia,” alisema Bw. Lyimo.

Pia amewakumbusha wafanyakazi wote ambao bado kujiunga kwenye chama cha Wafanyakazi sehemu ya Kazi, wafanye hima na wajiunge ili nao wapate haki za kutetewa endapo watapata matatizo mbalimbali.

   Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (wa kwanza kulia), akifuatilia kwa makini zoezi la uchaguzi mdogo wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la kiwanja hicho uliofanyika leo katika ukumbi wa Transit uliopo jengo la kwanza la abiria (TBI).

Wawakilishi wa wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Chama  cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakihesabu kura leo za nafasi ya Mwenyekiti mara baada ya uchaguzi uliofanyika leo katika Ukumbi wa Transit uliopo jengo la kwanza la abiria (TBI).


Naye Bi. Myovela aliyechaguliwa katika nafasi ya Uenyekiti Kamati ya Wanawake alisema atahakikisha anawatumikia wanachama wote bila kujali umri, dini wala kabila, ambapo amesisitiza hatakuwa na urafiki kwa yeyote  atayekwamisha jitihada zake hizo.
“Naomba ushirikiano wenu mkubwa ili tujenge TUGHE mpya ninayoamini itafanya vizuri kutetea wanachama wote,” alisema Bi. Myovela.  




Hata hivyo katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani  Bw. Lyimo alishinda kwa kishindo kwa kura 39 na kuwashinda Simon Mbogo (32) na Victor Mabote (3).


 Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakihesabu kura za nafasi ya Uenyekiti Kamati ya Wanawake, katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Transit wa Jengo la Kwanza la abiria (TBI).


Naye Bi. Myovela alipata kura 24 na kuwashinda Rehema Ambari aliyepata kura 17, Mwanahawa Mdee kura moja na Yusta Swebe hakupata kitu.

Kwa upande wa ujumbe Bw. Steven Ntambi alishinda kwa kura tisa, huku mpinzani wake Bi. Ambari akiambulia kura tano.

Uchaguzi huo umefanyika wa kuziba mapengo baada ya aliyekuwa Wenyeviti Bw. Abbas Rweyumamu, na Bi. Simai Ngasani kuhamishwa kituo cha kazi cha JNIA na kupelekwa Makao Makuu, huku Bw. Ntambi akijaza nafasi ya ujumbe iliyoachwa na Lyimo.


  Msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Honesta Ngowi kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana (kulia) akishughudia wanaohesabu kura za nafasi ya ujumbe wa TUGHE katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria (TBII).


Hata hivyo kwa nyakazi tofauti wasimamizi wa uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gaudence Kadyango na Bi. Honest Ngowi kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana waliwataka viongozi waliochaguliwa kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama ili kuzidisha mshikamano sehemu ya kazi.

Wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) tawi la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza Katibu wa tawi hilo, Bw. Thawabu Njeni akitoa ufafanuzi kabla ya kutangazwa kwa matokeo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria (TBII).


Uongozi mzima wa TUGHE-JNIA ni Lyimo (Mwenyekiti), Thawabu Njeni (Katibu), Anna (Mwenyekiti wanawake), Mastidia Ndyomulwango (Katibu Kamati ya Wanawake), Mwanaisha Athuman (Kamati ya Vijana), Kidiga Baltazar (Kamati ya Walemavu), huku wajumbe ni Sadic Milulu, Theobald Beng’inus, Mwanaheri Omar, Adventina Rugimbila, Hussein Msuya, Ntambi na Mbogo.

Waziri Mwakyembe Akunwa na Uwekezaji wa Bayi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) akipita mbel;e ya Uwanja wa Ndani wa Michezo wa Filbert Bayi Sports Complex alipotembelea jana baada ya kufungua semina ya kuwawezesha wanawake ndani na kupitia michezo jana Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amepongeza uwekezaji mkubwa wa miuondo mbinu ya michezo uliofanywa na mwanariadha wazamani nchini Filbert Bayi.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana alipotembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi ya Fibert Bayi (FBF) yaliyopo Mkuza, Kibaha, ambako kuna viwanja mbalimbali vya michezo vikiwemo viwanja vya nje na ndani.

Mwakayembe baada ya kufungua semina ya kuwawezesha wanawake kupitia michezo iliyofanyika Mkuza, alitembelea maeneo hayo ya FBF na kushuhudia uwanja mkubwa wa ndani wenye viwango vya kimataifa.

Sehemu ya uwanja huo kwa sasa inatumiwa na wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa meza ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia mwezi ujao.

Dk Mwakyembe alisema kuwa hajawahi kufika Mkuza na wala hakujua kama kuna uwekezaji mkubwa kama huo uliofanywa na Bayi, ambapo aliwataka akina Mbana Samatta kuiga uwekezaji wa uliofanywa ma Bayi.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Filbert Bayi (FBF), Filbert Bayi akitoa maelezo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipotembelea taasisi hiyo jana Mkuza, Kibaha. Mwingine pichani ni Mkurugenzi wa shule za Filbert Bayi, Anna Bayi.
Alisema kuwa wachezaji wengi wakipata fedha zaoe wamekuwa wakinunua magari ya kifahari badala ya kuwekeza katika miundo mbinu mbalimbali kama alivyofanya Bayi na kutengeneza ajira kwa watu kibao.

Mbali na uwanja huo wa ndani ambao una viwanja vvya michezo yote ya ndani, pia kuna viwanja vya nje vya soka, netiboli na mpira wa kikapu.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akiwa na mmoja wa wakufunzi wa semina ya kuwawezesha wanawake ndani na kupitia michezo aliyofungua jana Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.





Daktari Mkuu wa Kituo cha Afya cha Filbert Bayi akisalimiana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe. Wengeni ni Bayi (wa pili kushoto) na mkurugenzi wa Shule za Filbert Bayi, Anna Bayi.

Ukumbi mkubwa wa shughuli mbalimbali wa FBF Mkuza, Kibaha.
Waziri huyo pia alitembelea majengo ya shule ya FBF kuanzia chekechea hadi sekondari, vyumba vya komputa, kituo cha afya, ukumbi na wodi ya wazazi na ile ya wagonjwa wa kawaida.

Thursday, 1 March 2018

Mkurugenzi JNIA Ataka Wafanyakazi Kujituma Zaidi

Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka akiongea na wafanyakazi wa kiwanja hicho kwenye ukumbi wa mikutano wa Transit uliopo Jengo la Kwanza la abiria (TB1) leo, ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya kiutendaji. Kulia ni Afisa Rasilimali Mkuu Bi. Fatma Matimba.

Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi wa Kiwanja CHA Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na juhudi ili kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Munanka alitoa kauli hiyo leo alipokutana na wafanyakazi wa JNIA,  katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Transit uliopo Jengo la Kwanza la abiria (TBI), ambapo amesema wafanyakazi wasipofanya kazi kwa bidii watashindwa kuzalisha kwa ziada. Huduma kubwa inayotoa JNIA ni pamoja na kutua na kuruka kwa ndege za ndani na nje ya nchi.

Wafanyakazi wa  Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza  Kaimu Mkurugenzi wa kiwanja hicho,  Bw. Johannes Munanka leo alipokuwa akizungumza nao mambo mbalimbali ya kazi.

Amesema wafanyakazi wasiofanyakazi kwa bidii watasababisha kuzorota kwa utoaji wa huduma kwenye Kiwanja hiki, jambo ambalo litasababisha kukimbiza abiria na wateja wengine wanaofanya shughuli zao mbalimbali kwenye kiwanja hiki, ambacho ni miongoni mwa viwanja viwili vya Kimataifa vilivyopo nchini. Kiwanja kingine cha Kimataifa ni cha Kilimanjaro (KIA).

“Ninawashukuru sana wafanyakazi wanaochapa kazi kwa bidii bila kusukumwa ingawa wengine asili ya kazi zao zinawasukuma kufanya hivyo, mfano mzuri ni waongoza ndege hawezi kutegea, tofauti na wachache waliopo katika idara nyingine wamekuwa hawana bidii ya kazi hadi wasukumwe,” amesema Bw. Munanka.


Meneja Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),  Bw. Vedastus Fabian (mwenye miwani mbele) akiandika mambo mbalimbali katika mkutano ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka leo.

Hata hivyo, amesema wafanyakazi wote wanaosubiri kusukumwa waache mara moja na wahakikishe wanajituma wenyewe, ili kuboresha huduma zinazopatikana JNIA, ambazo zitakuwa sifa nzuri ya kuvuta wateja kutoka ndani na nje ya nchi.

“Ukiangalia katika ngazi ya meneja au wanaoingia kwenye menejimenti nao wanatakiwa kuwasimamia kwa umakini mkubwa na endapo watashindwa kufanya hivyo inanilazimu nifanye kazi za kusimamia na umeneja, ambapo sio jambo zuri litasababisha kushindwa kutekeleza majukumu mengine zaidi ya kiutendaji, hivyo ndugu zangu tuchape kazi,” amesema Bw. Munanka.


Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka akijibu maswali ya wafanyakazi wa kiwanja hicho, leo alipokutana nao katika mkutano uiliofanyika katika ukumbi wa Transit ulipo Jengo la Kwanza la abiria (TBI).

Akizungumzia vitendea kazi, Bw. Munanka ameahidi kushughulikia kwa ngazi ya JNIA ili vipatikane haraka na pia kuwasilisha Makao Makuu (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania-TAA) vile vinavyohitaji idhini ya kuvinunua.
Ofisa Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Rachel Manyilizu akiuliza maswali kwa Kaimu Mkurugenzi wa JNIA (hayupo pichani) katika mkutano wa wafanyakazi uliofanyika kwenye ukumbi wa Transit katika jengo la Kwanza la abiria (TBI).

 

Ofisa Usalama, Bw. Musso John, akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyoulizwa katika mkutano ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Transit uliopo katika Jengo la Kwanza la abiria (TBI).



 Fundi Umeme Mwandamizi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi Mastidia Ndyomulwango akiwasilisha hoja kwenye mkutano wa Wafanyakazi wa JNIA, ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi wake, Bw. Johannes kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji wa kazi.