Wednesday, 6 April 2016

Wanariadha wazidi kujitokeza kujiandikiza kushiriki Ngorongoro Marathon 2016, Mkuu wa mkoa wa Arusha athibitisha kushiriki mbio hizo



Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mbio za Ngorongoro zilizofanyika mwaka jana.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA kibao wamezidi kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki mbio za Ngorongoro zitakazofanyika Aprili 16 mwaka huu, imeelezwa.

Mbio za mwaka huu zinatarajia kuwa na msisimko wa aina yake huku tayari wanariadha zaidi ya 700 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa wamejiandikisha kwa ajili ya mbio hizo.

Mratibu wa Ngorongoro Marathon 2016, Zulfa Fadhili alisema jana kuwa, usajili wa wanariadha wanaotaka kujiandikisha unaendelea katika vituo kadhaa pamoja na katika mtandao.

Fadhili alivitaja baadhi ya vituo hivyo kuwa ni pamoja na Arusha katika duka la Lemaya, wakati Karatu Deus Super Market huku Moshi usajili unafanyika katika ofisi za Zara na Malenga Investment.

Aliwataka wanariadha kuendelea kujiandikisha kwa ajili ya ushiriki wa mbio hizo, ambazo mwaka huu zinatarajia kuwa na msisimko wa aina yake.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Daud Ntibenda, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha akizungumza wakati wa mbio za mwaka juzi katika Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu.
Aidha, Fadhili alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda amethibitisha kushiriki mbio hizo ambazo mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe.

Lengo la mbio hizo ambazo zinadhaminiwa na Bonite Bottlers, Zara Charity na Zara Tours, Davis Mosha, Malenga Invstment, Exim Bank na African Safaris, ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendesha shule za watoto wa Kimaasai, ambao wanasomeshwa bure.

Tuesday, 5 April 2016

Conte atua rasmi Chelsea, Sutton amponda asema hataleta miujiza



LONDON, England
UTEUZI wa Chelsea kumfanya Antonio Conte kuwa mbadala wa muda mrefu wa Jose Mourinho hakuna maana yoyote, anasema mshambuliaji wazamani wa Blues Chris Sutton.

Mourinho, 53, alitimuliwa Desemba nwaka jana akidaiwa kutoelewa na baadhi ya wachezaji wakubwa wa timu hiyo.

Conte, alitua jijini hapa na kumwaga wino wa kuifundisha timu hiyo kwa miaka mitatu baada ya kumalizika kwa msimu huu.

"Ikiwa atakuja hapa na kuanza kukorofishana na wachezaji, basi anaweza kukosa mafanikio, alisema Sutton.

Chini ya Mourinho, Chelsea ilitwaa taji la Ligi Kuu ya England ikiwa na point inane zaidi msimu uliopita na pia ilitwaa Kombe la Ligi.

Lakini timu hiyo ilipoteza mechi zake tisa kati ya 16 za mwanzo za ligi na walikuwa katika nafasi ya 16 katika msimamo, pointi moja juu ya ukanda wa kushuka daraja, wakati Mourinho akitimuliwa.

Kocha wazamani wa Uholanzi Guus Hiddink, aliyeteuliwa kuchukua kwa muda nafasi ya Mourinho hadi mwishoni mwa msimu, hajapoteza mchezo wowote kati ya 15 tangu achukue timu hiyo.

Hatahivyo, the Blues imemchukua Conte, ambatye atawasili katika klabu hiyo mara baada ya kumalizika kwa fainali za Mataifa ya Ulaya za  Euro 2016 kama kocha wao wa kudumu.

"Chelsea walikuwa na nafasi nzuri ya kumbakisha Hiddink," aliongeza Sutton,mwenye umri wa miaka 43. Na chini yake timu iliimarika kila mahali.

Conte alishinda taji la Serie A katika miaka yake mitatu wakati akiwa kocha wa Juventus, kabla hajaachia ngazi na kutua katika timu ya taifa ya Italia mwaka 2014.

Wachezaji wazamani wa Chelsea Andy Townsend na Pat Nevin wote wanaamini the Blues imefanya uteuzi mzuri
 .
"Sifikiri kama Conte atafanya tofauti na vile ambavyo alikuwa akipenda Jose katika kiwango chake, alisema kiungo wazamani wa kimataifa wa Ireland Townsend.

Moja ya kazi ya Conte atakapotua Stamford Bridge inaweza kuwa ni kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya John Terry.

Nahodha huyo wa Chelsea mwenye umri wa miaka 35 atamaliza mkataba wake katika kipindi cha majira ya joto na anasema bado hajapewa mkataba mpya.

Lakini Townsend anaamini kuwa kuwasili kwa Conte kunaweza kusaidia kuongeza mkataba kwa beki huyo wazamani wa England ili aweze kuendelea kubaki Stamford Bridge.

Conte pamoja na kujihakikishia kibarua Chelsea, lakini hajaahidiwa fungu na mmiliki wa timu hiyo Roman Abramovich ili kusajili wachezaji wapya.

Lakini mshambuliaji huyo wazamani wa England anafikiri the Blues itapambana kuvutia wachezaji wa kubwa Ulaya bila kuvuruga sheria za matumizi ya fedha katika usajili.

Chelsea,ambayo ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 2012 na lile la Ligi ya Ulaya mwaka 2013, wako katika nafasi ya 10 katika Ligi Kuu ya England, wakipitwa pointi 10 na timu nne za kwanza katika msimamo huo.

Yaya Toure kuondoka Man City kumkwepa kocha Guardiola anayetua mwishoni mwa msimu



LONDON, England
KIUNGO wa Manchester City Yaya Toure ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu baada ya hadi sasa kutopewa mkataba mpya, amesema wakala wake.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast, na ni mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2011, alijiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu akitokea Barcelona kwa pauni milioni 24 Julai mwaka 2010.

Miaka sita iliyopita Toure aliuzwa na aliyekuwa kocha wa Barca Pep Guardiola, ambaye sasa anatua Man City kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini wakati Mhispania huyo atakapoondoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu.

"Tulisubiri kwa muda mrefu. Manchester City iliahidi kuongeza mkataba lakini hakuna kilichofanyika hadi sasa, hivyo Yaya ataondoka Juni, alisema wakala wake Dimitri Seluk.

"Bila shaka hilo litakuwa limesikitisha sana Yaya, lakini ni mchezaji wa kulipwa atabaki katika mataba na ataendelea kuifanyia mazuri Man City katika kipindi kilichobaki.

Vyombo vya habari vimekuwa vikimuhusisha Toure na kutaka kuhamia Inter Milan inayofundishwa na kocha wazamani wa Man City Roberto Mancini.

"Ofa kibao zimekuja zikitaka kumsajili Yaya na tunazichambua, alisema Seluk. "Inter? Tunazungumzia kuhusu klabu kubwa.

"Kila mmoja anajua kuhusu uhusiano kati ya Yaya na Mancini lakini...bado hatujafanya uamuzi wowote.

Toure alishinda taji la Ligi Kuu ya England akiwa na Man City mwaka 2012 na 2014, Kombe la FA mwaka 2011 na lile la ligi mwaka 2014 na 2016.

Man City leo watakuwa wageni wa Paris St Germain katika mchezo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Friday, 1 April 2016

Ibrahimovic ataka sh. 1,881,000,000 kwa wiki kusajiliwa klabu za Ligi Kuu England



LONDON, England
MCHEZAJI Zlatan Ibrahimovic anataka apewe kiasi cha pauni 600,000 (sawa na sh. 1,881,000,000)kwa wiki ili kuchezea klabu ya Ligi Kuu ya England.

Kiasi hicho cha fedha kimebainishwa na mchezaji huyo ambaye ataondoka katika klabu yake ya sasa ya Paris Saint-Germain akiwa huru katika kipindi cha majira ya joto.

'Tunataka kumsajili, lakini kiasi cha fedha anachotaka alipwe ndio tatizo,' kilisema chanzo cha ndani. ‘Tukifanikiwa hilo tutakuwa tumefanya jambo kubwa sana kumpata, lakini ukweli anahitaji kiasi hicho cha fedha, akiwa na umri wa miaka 34?
Ibrahimovic amekuwa akifanya mazungumzo na timu za China, ambako inasakiwa kuwa ameahidiwa kupewa kiasi cha pauni milioni 1 kwa wiki endapo atatua huko, lakini hana mpango wa kuhamia Mashariki ya Mbali.

Badala yake ameziambia klabu za Uingereza kuongeza mshahara wake aliokuwa akiupta PSG, ambako aliwapeleka mabingwa hao wa Ufaransa kutwaa taji jingine.

Ibrahimovic yuko mbioni kwenda kucheza England lakini ikiwa na maana kuwa kolabu moja itakuwa inatoa mshahara mkubwa nchini. Anaamini kuwa hatakuwa na furaha kutokana na kodi zilizotozwa Uingereza.

Mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa katika Ligi Kuu ya England kwa sasa ni Wayne Rooney, ambaye anaondoka na kitita cha pauni 260,000.

Arsenal, Manchester United, Chelsea na hata West Ham zimekuwa zikihusishwa na mshambuliaji huyo wa Sweden.

Wakala wa Ibrahimovic Mino Raiola aliliambia gazeti la Dello Sport: 'Ukiiondoa Manchester City, ambayo itamchukua (Pep) Guardiola, klabu zote kubwa zimepiga hodi zikitaka kumchukua kocha huyo.
 
Mahitaji hayo makubwa anayotaka Ibrahimovic bila shaka yatazigharimu klabu angalau pauni milioni 31 kwa msimu mmoja tu katika mkataba wake huyo anaoutaka.

Riadha Tanzania watangaza wachezaji kuunda timu ya taifa ya U-20 itakayopiga kambi kwa Filbert Mkuza Kibaha


Baadhi ya wanariadha chipukizi wa Tanzania wakichuana katika moja ya mashindano kwenye Uwanja wa Taifa hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) imetangaza majina 27 ya timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 kwa ajili ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika nchini Aprili 29 na 30.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Robert Kalyae, timu hiyo ya wanawake na wanaume ambayo itapiga kambi katika shule za Filbert Bayi Mkuza Kibaha, imechaguliwa baada ya kufanyika mashindano ya mchujo mara tatu.

Alisema kuwa mashindano hayo ya mchujo yaliyofanyika Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

Timu ya wanaume inaundwa na Adinani Haruna wa Moshi atakayeshiriki mbio za mita 100 na 200, Benjamin Michael wa Dar es Salaam atakayeshiriki mbio za mita 100 na 200, Oscar Prosper (Moshi) atakayekimbia mbio za mita 400.

Wengine ni Imani James na John Silima wa Dar es Salaam watakimbia mbio za mita 400, Thobias Bula, Simon Francis, Emmanuel Gadiye na Francis Dambel kutoka Karatu watakimbia mita 800 na 1500.
Wachezaji na viongozi wa timu ya mkoa wa Dar es Salaam katika picha ya pamoja baada ya kushiriki mashindano ya taifa mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kalyae aliwataja wachezaji wengi wa timu hiyo kuwa ni pamoja na Elisha Wema wa Manyara na Jackson Makombe wa Pwani mita 5,000.

Watakaorusha mkuki, kisahani na tufe ni pamoja na Sabas Daniel wa Bagamoyo, kuruka chini ni Anthony Mwanga, anayesoma Afrika Kusini, Dennis David wa Arusha, Hafidh Khalfan mita 400 na 800, na Jimmy Kisumo wa shule ya sekondari Tambaza ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa wanawake waunaokimbia mbio za mita 100 na 200 ni Rehema John toka Magu, Jane Maiga wa Pwani, (mita 400 na kuruka chini) watakuwa Hynes Bamopenja wa Dar es Salaam na Rose Seif wa Pwani.

Watakokimbia mita 800 na 1500 ni pamoja na Dorcas Boniface, Regina Deogratius, Betrina Michael na Easter Martin, Angelina Tsere mita 5,000 na Aisha Mohamed mita 5,000.
Mbali na Kalyae makocha wengine watakaoinoa timu hiyo ni pamoja na Mwinga Mwanjala na Ephania Mugaza wakati daktari ni Richard Yomba na meneja wa timu hiyo ni Peter Mwita.

Alisema vigezo walivyotumia kuchagua timu hiyo ni pamoja na kuzingatia muda wa wachezaji katika mashindano hayo ya majaribio, umri pamoja na bidii na kujituma.