Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania, Johnson
Mshana akimkabidhi mshindi wa tuzo za Kimataifa za DStv Eutelsat Star Awards, Pricilla Marealle cheti cha ushindi wakati wa mahafali ya kidato cha sita
katika shule ya St Mary Goretti hivi karibuni. Kulia ni Ofisa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania. Grace Mgaya.
Na Mwandishi Wetu
KWA mara nyingine tena Tanzania imeibuka
kinara katika tuzo za kimataifa za
wanafunzi zijulikanazo kama DStv Eutelsat Star Awards ambapo mwanafunzi
Priscilla Marealle kutoka shule ya sekondari ya St. Mary Goreti mkoani
Kilimanjaro ameweza kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa kunyakua nafasi ya
kwanza katika kipengele cha uchoraji bango
ikiwa ni baada ya mchuano mkali baina ya mamia ya wanafunzi kutoka nchi
zaidi ya 10 kote barani Afrika.
Kwa upande wa uandishi wa insha kijana Tanaka
Chonyera kutoka nchini Botswana aliweza
kujinyakulia ushindi wa kwanza.
Tuzo hizi ambazo huhusisha uandishi wa insha maalum
au kuandaa bango yenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za
wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19
kote barani Afrika ambapo kampuni ya MultiChoice inaendesha shughuli zake.
Priscilla ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita
wa mchepuo wa Sayansi katika shule ya Mtakatifu Maria Goreti alitangazwa rasmi
kuwa mshindi mjini Accra nchini Ghana ambapo ndipo jopo la watahini liliongozwa
na Paolo Nespoli, mwanaanga nguli kutoka European Space Agency (ESA) lilikaa
kupitia kazi kutoka kwa wanafunzi walioshinda katika nchi mbalimbali.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo ya Mtakatifu
Maria Goreti Sister Lucresia Njau alisema kuwa anaishukuru sana kampuni ya
MultiChoice Tanzania kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika Mashindano hayo
na hatimaye kuweza kunyakua tuzo hiyo kupitia mwanafunzi wao Priscilla.
“Huyu kijana ana jitahidi sana katika chochote kile
anachokifanya, iwe ni darasani au hata katika majukumu mengine nje ya darasani.
Ni msikivu mtiifu lakini zaidi ya yote ni mbunifu sana. Naamini haya ndiyo
yaliyomfanya aweze kushinda tuzo hizi” alisema Sr. Lucrecia Njau.
No comments:
Post a Comment