Tuesday 19 March 2019

MultiChoice Yatangaza Fursa kwa Wadau wa Filam Nchini, Afrika


Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya MultiChoice-Tanzania imetangaza  fursa ya kipekee kwa wadau wa tasnia ya filamu Tanzania na barani Afrika kwa ujumla ijulikanayo kama MultiChoice Talent Factory Portal iliyodhamiria kuleta mapiduzi ya hali ya juu katika uaandaaji wa filamu zenye viwango vya kimataifa kutoka barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano kutoka MultiChoice Tanzania Johnson Mshana alieleza kuwa programu hiyo ni muendelezo wa programu maalum ya iliyodhamiria kuleta mabadiliko katika tasnia ya filamu barani Afrika.

 “MultiChoice Talent Factory ambayo ni progamu mama  ilizinduliwa rasmi mapema  Mei mwaka jana na imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kwenye tasnia ya filamu hapa nyumbani Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Tulianza kwa kupeleka vijana wanne katika kambi maalum ya mafunzo ya uandaaji filamu katika akademia maalum kule Nairobi nchini Kenya, kisha mafunzo maalum kwa magwiji wa sauti yaliyofanyika Januari mwaka huu na hatimaye leo hii tumekuja tena na platform maalum yenye dhamira ile ile ya kuleta mapinduzi katika tasnia ya filamu barani Afrika”, alisema Mshana.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo alisema kuwa, anaishukuru sana Kampuni ya MultiChoice kwani imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya filamu hapa Tanzania.

 “Binafsi nilishuhudia uzinduzi wa programu ya MultiChoice Talent Factory mapema mwaka jana kule mjini Dodoma na leo hii tunazindua tena sehemu nyingine ya programu hiyo hiyo. Hakika ni fursa ya kipekee na ninapenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha wadau wote waliopo katika tasnia yetu kuitumia nafasi hii ipasavyo ili kuweza kujifunza, kubadilishana ujuzi na hatimaye kupata kazi zenye maudhui ya hali ya juu kutoka hapa hapa Afrika”,  alisema Fisoo.

Naye Ofisa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Grace Mgaya alimalizia kwa kueleza kuwa ukurasa huu ni wa wazi kwa watu wote hususani wadau wa filamu waliopo hapa nyumbani na Afrika kwa ujumla.

 “Tunaamini kwa kupitia program hii tutaweza kuwafikia wadau wengi zaidi na tunatarajia kazi zenye ubora wa hali ya juu kutoka barani Afrika kwa siku zijazo kutokana na matokeo chanya yatakyoletwa na program hii ya MultiChoice Talent Factory”, alisema Grace.


No comments:

Post a Comment