Thursday 9 March 2017

Samatta atupia mbili Genk ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Gent ligi ndogo ya Ulaya


Mbwana Samatta (kulia) akifurahia baada ya kufunga moja ya mabao yake hivi karibuni.
a Mwandishi Wetu
NYOTA ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta imeendelea kung’ara baada ya usiku wa jana kufunga mabao mawili wakati timu yake ya Genk ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya wapinzani wao wa Ubelgiji ya Gent katika mchezo wa raundi ya 16 bora ya Mashindano ya Ligi ya Ulaya.

Mchezo huo wa kwanza wa Ligi ya Ulaya ulipigwa usiku wa jana kwenye Uwanja wa Arena mjini Gent.

Samatta alizifumania nyavu katika dakika ya  41 na 72, wakati mengine ya wageni yalifungwa na kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy dakika ya 21, mabeki Mgambia Omar Colley dakika ya 33 na Mfinland Jere Uronen dakika ya 45.

Wenyeji waliandika mabao yao kupitia kwa mshambuliaji kutoka Nigeria, Samuel Kalu Ojim dakika ya 27 na mshambuliaji kutoka Mali, Kalifa Coulibaly katika dakika ya 61 na sasa Genk watakuwa na mchezo mwepesi wa marudiano nyumbani kuwania kutinga robo fainali ya mashindano hayo.

Samatta jana amefikisha mabao 16 katika mechi 47 alizoichezea Genk tangu asajiliwe Januari mwaka jana kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
 
Kati ya mechi hizo 47, michezo 18 Samatta alicheza msimu uliopita na 29 msimu huu na kati ya hizo, ni michezo 28 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 18 msimu huu.

Mechi 19 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 11 msimu huu, wakati 11 hakumaliza baada ya kutolewa, sita msimu uliopita na tisa msimu huu na katika mabao hayo 16, 10 amefunga msimu huu na sita msimu uliopita.

Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa: Ryan, Castagne, Brabec, Colley, Uronen, Berge, Malinovskyi/Heynen dk80, Pozuelo, Authors/Trossard dk90, Boetius/Buffalo dk45 na Samatta.

KAA Gent: Kalinic, Gigot, Coulibaly, Matton, Mitrovic Saief/Simon dk76, Kalu, Perbet/Foket dk76 Verstraete/Rabiu dk45 Esiti na Gershon.

No comments:

Post a Comment