LONDON, England
ARSENAL leo imepokea kichapo cha nne katika mechi tano za Ligi Kuu ya England
wakati Craig Dawson akifunga mara mbili na kuisaidia West Brom kupeleka kipigo
kikubwa kwa the Gunners.
Kipigo hicho kimeifanya Arsenal kupoteza matumaini ya kumaliza ligi hiyo
ikiwa ndani ya nne bora, nafasi ambayo ingeiwezesha kufuzu moja kwa moja kwa
Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Dawson alifanikiwa kufunga mabao yake mawili kwa kichwa, akiunganisha
mipira ya kona huku mabeki wa the Gunners wakishindwa kuokoa.
Arsenal ilisawazisha kupitia kwa Alexis Sanchez aliyefunga kwa shuti la
karibu likiwa ni bao lake la 18 katika ligi msimu huu.
Hatahivyo, Arsenal walijikuta wakiwa nyuma tena ndani ya kipindi cha pili
wakati mchezaji aliyetokea benchi Hal Robson-Kanu akifunga bao baada ya kuugusa
mpira mara ya pili tangu aingie uwanjani.
Arsenal, iliyopoteza kipa wao Petr Cech kutokana na maumivu, walishindwa
kufanya kweli na kujikuta wakichapwa la tatu.
Kipigo hicho ni pigo mara mbili kwa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger,
ambaye jana alijikuta matatani baada ya baadhi ya mashabiki kubeba mabango
wakimtaka ajiuzulu.
Kundi la mashabiki ambao hawamtaki Wenger walikuwa wakipiga kelele huku
wakiwa wamebeba mabango, ambayo mengine yalisomeka ‘inatosha inatosha’.
Hatma ya Wenger kuendelea kuifundisha timu hiyo baada ya kumalizika msimu
huu, iko matatani baada ya kutupwa pointi tano kutoka katika nafasi ya nne ya
msimamo wa ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment