PARIS, Ufaransa
BEKI wa kushoto mwenye kipaji, Raphael Guerreiro ni mmoja kati ya
wachezaji watatu wa Ureno ambao watakaikabili nchi yao waliyozaliwa, wakati
watakapokutana na Ufaransa kwenye fainali ya mataifa ya Ulaya, Euro 2016, kesho Jumapili saa nne usiku kwa saa za hapa Bongo.
Guerreiro na golikipa, Anthony Lopes walizaliwa na kukulia nchini
Ufaransa, ambako ni nyumbani kwa Wareno wengi wahamiaji.
Kiungo Adrien Silva aliishi nchini Ufaransa hadi akiwa na umri wa
miaka 12, wakati alipohamia nchini Ureno na familia yake.
“Nilichagua
Ureno. Yalikuwa maamuzi yangu muhimu. Si familia yangu wala marafiki zangu
ambao waliweza kuubadilisha uamuzi wangu,” amesema Guerreiro
mwenye umri wa miaka 22, ambaye mwezi uliopita alikubali uhamisho wa kwenda kwa
miamba ya Ujerumani, Borussia Dortmund akitokea Klabu ya Lorient inayoshiriki
Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
Guerreiro alizaliwa kitongoji cha Le Blanc Mesnil jijini Paris, umbali
mfupi kutoka kwenye Uwanja wa Stade de France ambako fainali hiyo inachezwa leo.
Ufaransa inaingia kwenye mchezo huo ikiwa ni nchi ya kwanza kufika
mara mbili fainali ya Euro ikiwa nchi mwenyeji wa mashindano, mara ya kwanza
ilikuwa mwaka 1984.
Michel Platini bado anashikilia rekodi ya magoli mengi zaidi
kwenye msimu mmoja wa michuano ya Euro (magoli 9, Euro 1984) magoli matatu
zaidi ya Antoine Griezmann aliyefunga magoli 6 hadi sasa Euro 2016.
Kwa upande wao Ureno hadi wanamaliza hatua ya makundi walikuwa
hawajashinda mchezo hata mchezo mmoja. Ni mfumo tu wa mashindano ya mwaka huu
ndiyo uliwapa nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora, kupitia mlango wa nyuma.
Ureno mechi yao katika hatua ya 16 bora ilishuhudia dakika 90
zikiisha kwa sare. Bao la ushindi likapatikana dakika ya 117, dakika tatu kabla
ya dakika za nyongeza kumalizika.
Ureno kwenye hatua ya Robo fainali waliitoa Poland kwa mikwaju ya
penalti baada ya sare ya bao 1-1 dakika 120.
Cristiano Ronaldo ameifikia rekodi ya gwiji wa Ufaransa, Michel
Platini ya kufunga magoli 9 ya Euro. Ronaldo alifunga goli lake la kwanza
kwenye michuano ya Euro mwaka 2004.
Anahitaji goli moja ili kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye
michuano ya Euro.
Mara ya mwisho timu kutinga fainali kiujanja ujanja namna hii kama
Ureno, ilikuwa Italia kwenye kombe la Dunia 1982 na ikawa bingwa.
No comments:
Post a Comment