Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga imesema kuwa inatafakari adhabu ya dola
5,000 (sawa n ash milioni 10) waliyopigwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf)
baada ya wachezaji wake kuchelewesha muda.
Caf juzi ilitangaza kuiadhibu Yanga baada ya baadhi ya
wachezaji wake kumzonga mwamuzi na kusababisha kuchelewesha mchezo wake timu
hiyo ilipocheza na GD Sagrada Esperanca uliofanyika Angola Mei 18, 2016.
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit anakiri
wachezaji wao kumzonga mwamuzi lakini kwa sasa wanatafakari kabla ya kutoa
tamko kamili.
Mchezo huo ulikuwa ni wa hatua ya kutafuta nafasi ya
kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Uamuzi wa mchezo huo Na. 100 ulifanywa na Kamati ya
Nidhamu ya CAF inayoundwa Mwenyekiti Raymond Hack –
Raia wa Afrika Kusini na wajumbe Mustapha Samugabo (Burundi) na Gbenga
Elegbeleye (Nigeria). Pia alikuwako Amina Kassem kutoka Sekretarieti ya CAF
ambaye ni Mtawala
katika Kitengo cha Nidhamu.
Katika mkutano huo uliofanyika Cairo, Misri –
Makao Mkuu ya CAF, Julai 3, 2016, kamati ilipitia taarifa zote za mchezo na
kufikia uamuzi wa kuipiga faini Yanga.
Taarifa za mchezo zinasema, wachezaji wa timu hiyo walionesha
utovu wa nidhamu kwa kumzonga mwamuzi na kumsukuma mara baada ya kutoa adhabu
ya penalti kwa wapinzani.
Kwa tukio hilo, mchezo huo ulisimama kwa dakika sita.
Polisi waliingia uwanjani kudhibiti hali hiyo.
Kwa kosa hilo, Wachezaji wa Yanga walivunja Ibara ya
82 inayozungumza utaratibu wa mawasiliano. Kwamba chama chochote cha mpira wa
miguu, klabu, ofisa au mtu yoyote wakiwamo wachezaji, lazima waheshimu
utaratibu za kuvumilia, uadiliufu na uanamichezo.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo ya Nidhamu ya CAF, Yanga ilistahili
kutozwa faini ya dola 10.000 za Marekani kwa makosa ambayo si uungwana kwenye
soka yaliyoonyeshwa na wachezaji wake.
Lakini kwa kuwa Yanga haikuonyesha utovu wa nidhamu
katika mchezo mingine ya kimataifa iliyofuata dhidi ya MOB ya Algeria na TP
Mazembe ya DRC, imepunguziwa adhabu na sasa wametakiwa kulipa dola 5,000 za
Marekani kama faini.
Faini hiyo haina budi kulipwa mara moja. Na imetakiwa
kuendelea kuwa na nidhamu, vinginevyo adhabu hiyo itawarudia.
No comments:
Post a Comment