Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha amehimiza usafi maeneo
yanayozunguka kiwanja hicho, ili kuepusha kuzaliana kwa ndege wanyama wa aina
mbalimbali.
Rwegasha aliyasema hayo wakati
akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini
(TAA), Mhandisi George Sambali jana wakati wa kufanya usafi wa mazingira
ulioongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,Bw. Laurent Mwigune kwa
wafanyakazi wa TAA kushirikiana na wakazi wa mtaa wa Kigilagila Relini ikiwa ni
muendelezo kuelekea kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016.
Alisema uchafu unachangia ongezeko la ndege wanyama
ambao ni hatari kwa ndege za abiria.
“Ndugu zangu tusiruhusu mazingira yetu yakawa
machafu, kwani ni hatari kubwa kwa sisi kiwanja cha ndege, kwani ndege mnyama
akiingia kwenye injini ya ndege ya abiria atasababisha hasara kubwa.
Hivyo tujitahidi kufanya mazingira yetu yawe
safi ili ndege kama kunguru na wengine wasizaliane hapo kwani wanaweza kuleta
madhara,” alisema Rwegasha.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo iliyotolewa
Kitaifa na Mhe January Makamba , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) ni Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu.
Alimtaka Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigilagila
Relini na Vituka kuhakikisha dampo lisilo rasmi lililoanzishwa karibu na ukuta
wa JNIA linaondolewa haraka, na waweke ulinzi kuzuia utupaji wa taka eneo hilo.
Aidha, alisema TAA imekuwa mstari wa mbele
kushirikiana na majirani zake wanaozunguka JNIA, ili kuweka mazingira hayo
katika hali ya usalama na usafi, lakini bado wapo wakazi wachache
wanaosababisha uhusiano huo kulegalega kwa kufanya vitendo vya kutupa taka hovyo.
Alifafanua zaidi kuwa TAA inaendelea na zoezi
la kufyeka vichaka vilivyozunguka JNIA, ili kuzuia uhalifu wa watu wabaya
kutumia mwanya huo kuruka uzio na kuingia ndani ya kiwanja hicho.
“Sisi hatutanii tena tunaagiza hili dampo liondoke na
tutaweka mabango
ya kuzuia utupaji wa taka hapa, na Wenyekiti tunaomba mhakikishe mnawakamata
wale wote watakaokiuka agizo hilo na tutawachukulia hatua za kisheria,” alisema Rwegasha.
No comments:
Post a Comment