Saturday, 8 August 2015

Alikiba kula sahani moja na Mafikizolo, Black Motion, Sauti Sol Jumamosi Agosti 15 Kenyatta Drive Dar es Salaam




Mwanamuziki Alikiba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha kubwa la muziki la kimataifa litakalofanyika Jumamosi ijayo Agosti 15 kwenye viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MWANAMUZIKI wa Tanzania Ali Kiba na Feza Kessy watapanda jukwaa moja na wakali Mafikizolo na Black Motion zote za Afrika Kusini katika tamasha la muziki la Party in the Park litakalofanyika Jumamosi jijini Dar es Salaam.

Alikiba alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, amejipanga vizuri kuhakikisha anafanya vizuri ili kujitangaza mbele ya wasanii hao wa kimataifa.
Meneja Masoko wa benki ya KCB, Edgar Masatu (kushoto), akizungumzia udhamini wao wa tamasha la muziki litakalofanyika Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa kwa sasa anaendelea na mazoezi ili aweze kufanya vizuri mbele ya wasanii hao wa kimataifa, ambao na yeye lengo lake kufikia huko.

Mbali na Black Motion na Mafikizolo, pia kutakuwa na Beatenberg nayo kutoka Afrika Kusini pamoja na Sauti Sol ya Kenya na wasanii wengine chipukizi kibao kutoka Tanzania.
Mkurugenzi wa Juega Casa, Harry Magere (katikati), akizungumzia kuhusu tamasha hilo la muziki. Kulia ni meneja wa masoko wa KCB, Edgar Masatu na bosi wa Rasilimali Watu wa Wantanshi, Irene Mwenda.
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo linaloandaliwa na Juega Casa Harry Magere, litafanyikia katika viwanja vya The Green au Uwanja wa Farasi mtaa wa Kenyatta Drive jijini Dar es Salaam.

Magere alisema kuwa lengo la tamasha hilo ni kuwajengea uwezo wanamuziki wa Kitanzania wanaopenda kufika mbali katika medani za muziki kimataifa.
 
Alisema tamasha hilo, ambalo litakuwa na burudani za kila aina, linatarajia kuanza saa 5:00 asubuhi hadi saa 1:00 usiku, ambapo Eaters Point watakuwa wakitoa huduma za chakula.

Mbali na Eaters, wadhamini wengine ni pamoja na Peps Cola, KCB Bank Tanzania Limited, Savanna,Black Energy, Wantanshi, Eatv na East African Radio.
 
Alikiba aliwataka wapenzi wa muziki nchini kujiandaa kupata burudani ya uhakika, kwani amejipanga vizuri kutoa vitu adimu siku hiyo na kwa sasa anaendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya onesho hilo.
Wasanii Feza Kessy na Alikiba wakizungumza na waandishiwa habari kuhusu tamasha la muziki la Party in the Park litakalofanyika Jumamosi Agosti 15 katika viwanja vya The Green au Uwanja wa Farasi Oyesterbay.


 

RISALA YA MGENI RASMI WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO YA WALIMU MCHEZO WA MPIRA WA MIKONO, MKUZA, KIBAHA TANZANIA 07/08/2015.



Washiriki wa mafunzo ya ufundishaji mpira wa mikono wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi pamoja na viongozi waliosimamia mafunzo hayo yaliyofanyika katika shule za Filbert Bayi Mkuza Kibaha jana Ijumaa.
 Katibu Mkuu, Kamati ya Olimpiki Tanzania  Ndugu Filbert Bayi

Viongozi wa Vyama vya Michezo (TAHA/ZAHA)

Mkufunzi wa Kimataifa,

Waratibu wa Mafunzo (TOC na TAHA/ZAHA)

Washiriki wa Mafunzo,

Mabibi na Mabwana.

Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru TOC na TAHA/ZAHA kwa kunipa heshima hii ya kuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo haya ya walimu wa mchezo wa Mpira wa Mikono.

 

Mafunzo haya ambayo yalifunguliwa siku 12 zilizopita na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Ndugu Gulam Rashid ambaye nina uhakika amewaambia mambo mengi mazuri ambayo mnatakiwa kuyazingatia wakati wa mafunzo haya yaliyohusisha walimu na wachezaji wa Taifa.
Ni matumaini yangu kuwa mmepata dozi nzuri ya taaluma na mbinu mbalimbali ya kufundisha mchezo huu. TOC inauthamini sana  mchezo wa mpira wa mikono, kwani ni kati ya michezo ambayo TOC inaamini kuwa ni baadhi ya michezo iliyokuwa inapendwa sana na watanzania pamoja na kuchezwa katika Mikoa michache hasa na vilabu vya Majeshi yetu (Polisi, JWTZ, Magereza, JKT/JKU nk.

Kama kweli tunataka mchezo huu uenee nchi nzima, vyama husika havina budi kufanya jitihada ya kufufua vyama vya mchezo huu Mikoani kama vipo na kuanzisha katika  Mikoa ambayo havina vyama hivyo, hali kadhalika na kuueneza katika Shule zetu za Msingi na Sekondari ambapo ndipo penye vipaji vingi. Tusisubiri tu wakati wa Michezo ya Umisseta na Umitashumta Taifa.  

Kama nilivyofahamishwa vyema haya ni mafunzo ya pili kufanyika kwa walimu wetu hapa Tanzania. Mafunzo ya awali kwa walimu yalifanyika mjini Dar Es Salaam  mwaka 2007 yote yakifadhiliwa na  Olimpiki Solidariti kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania.

Pia naamini mmefaidika na elimu mliopata kutoka kwa mtaalamu wa Kimataifa Ndugu Tuma ambaye amekuwa wakiwaandalia masomo yote ya nadharia na vitendo kwa muda wote wa siku 11. Ni mategemeo yangu elimu mliyopata itawasaidia kuandaa timu zenu na kutambua vipaji vipya katika maeneo mnayotoka. Ni ukweli usiopingika kwamba  mmejiongezea elimu ya kufundisha mchezo huu wa mpira wa mikono kwa kiwango cha hali ya juu, mkilinganisha uwezo na elimu mliyokuwa nayo awali na wachezaji wa taifa kufaidika kwa ushiriki wao wa mara ya kwanza.
Wakati wote nimewahi kusikia TOC kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza taaluma ya ufundishaji na mbinu za kisasa za kuboresha uwezo wa walimu, ili waweze kufikia viwango vinavyotakiwa kwa timu zetu zinaposhindana katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Ningependa kusisitizia sana kwenu walimu mnaomaliza mafunzo haya kwamba, mhakikishe mchezo huu wa mipra wa mikono  unapiga hatua kufikia kiwango ambacho kitatupeleka kwenye michezo ya Kanda, Afrika na Kimataifa.
Tanzania haina tofauti na nchi kama Misri, Algeria, Nigeria, Tunisia nk  ambao zimekuwa tishio katika mchezo wa mpira wa mikono katika bara letu la Afrika.

Ningependa kuwasihi walimu mnaomaliza mafunzo haya leo kuupeleka mchezo huu mashuleni walipo vijana wengi wenye vipaji vingi ambao wanafundishika na rahisi kuelewa. Inahitajika mipango mahususi ya mazoezi na mashindano ambayo nina imani Vyama vyetu vya Mpira wa Mikono Tanzania Bara na Zanzibar wanayo mipango hiyo.

Wizara zinazoshughulikia michezo Tanzania zimetayarisha mipango kwa kushirikiana na vyama vya michezo kuendeleza michezo ya aina yote. Linalotakiwa hivi sasa ni kwa walimu wetu kutumia mafunzo haya katika kuendeleza mchezo wa mpira wa mikono nchini. Changamoto itoke kwenu ili Vyama, Mabaraza na Wizara husika na wanamichezo baadhi yao ambao wako hapa leo waweze kuchangamkia mipango yenu mtakayoandaa.
Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru mtaalamu wa Kimatafa Ndugu Tuma kwa jitihada zake za kutoa mafunzo haya kwa ufanisi mkubwa, waratibu wa TAHA/ZAHA, TOC na Walimu washiriki kwani bila wao kuwepo hapa mafunzo haya yasingefanyika.

Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Olimpiki Solidariti kwa kufadhili mafunzo haya, Shirikisho la Kimataifa la mpira wa mikono (IHF) kwa kumteua  Mkufunzi niliyemtaja hapo juu kuendesha mafunzo, TOC na TAHA/ZAHA kwa maandalizi mazuri, mwisho kabisa nawashukuru wale wote waliohusika katika kufanikisha mafunzo haya kwa namna moja au nyingine hasa waratibu wa TOC na TAHA/ZAHA, Taasisi ya Filbert Bayi kama mwenyeji kwa huduma zote  nzuri mpaka kufika siku hii ya mwisho.
Kwa haya machache sasa natamka kwamba mafunzo yenu ya ualimu wa mchezo wa Mpira wa Mikono ninayafunga rasmi.


Ahsanteni!

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege walivyoshiriki maonesho ya Nane Lindi

Emmanuel Mbwambo (kulia), akimpa maelezo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, katika maonesho ya 22 ya Nanenane yanayofanyika kitaifa mkoani Lindi.
Wananchi wakiangalia mkanda wa video katika banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) unaoonesha shughuli za mamlaka hiyo katika maonesho ya Nane mkoani Lindi.

Tuesday, 4 August 2015

Mahafali ya Shule ya awali Joyland yalivyofana Kigamboni



 

Na Mwandishi Wetu

WAZAZI wamehimizwa kujenga utamaduni wa kupitia kazi na watoto wao wanaporudi shuleni kwa lengo la kusaidia ufahamu wao na kuwarahisishia kazi walimu katika suala la taaluma.

Pia wamekumbushwa kufuatilia nyendo za watoto wao kujua wanacheza wapi, na akina nani na rafiki gani wanaokuwa nao kwa muda mrefu sambamba na kutowaachia kutumia muda mrefu kwenye runinga kwani ni moja ya sababu ya kuharibika kwao na kuporomoka kimasomo wawapo likizoni.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Joyland, Fredrick Otieno wakati wa mahafali ya wanafunzi wa masomo ya awali wa shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo, Tua Ngoma, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Otieno alisema ushirikiano wa wazazi na walimu katika malezi ya watoto ni msaada mkubwa wa wanafunzi, lakini kama wazazi na walezi wataliacha jukumu hilo kwa walimu tu ni mtihani mkubwa na kuchangia kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini. Alisema ni lazima wazazi na walezi wakague madaftari na kazi za watoto wao wawapo majumbani na pia kuwazuia kuingia katika makundi au kuumia muda mrefu kucheza wakati wa likizo ili viwango vyao kitaaluma visiporomoke.

Pia aliwakumbusha wazazi na walezi kujenga tabia ya kuwalipa ada watoto wao ili kurahisisha kazi kwa shule wanazosoma kuwa kile kinachostahiki, alisema kucheleweshwa kwa ada ni tatizo ambalo linapunguza morali wa kazi kwa walimu, ingawa alisema Joyland imekuwa ikijitahidi kuhakikisha wanafunzi wanakipata kile kilichowapeleka wakati wazazi na walezi wakikumbushwa wajibu wao wa kuwalipia ada.

Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa hakuna hazina bora kama mtoto kupewa elimu ambayo huja kumsaidia ukubwani kwa kuzingatia kuwa dunia ya sasa inaendeshwa kisasa na bila elimu bora na ya kutosha ni vigumu kijana kusimama na kukabiliana na changamoto hizo.



Naye Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda, Shani Kanungira aliwasisitiza wazazi kutumia kujitolea na kutimiza wajibu wao kuwasomesha watoto badala ya kutumia fedha nyingi kwa mambo yasiyo na tija kwa watoto na familia zao kwa ujumla.

Shani alitoa nasaha yake kabla ya kumpisha Mwakilishi wa Ofisa Elimu ya Msingi Manispaa ya Temeke, Frank Makingi aliyesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kujenga utamaduni wa ushirikiano dhidi ya walimu wa shule wanazosoma watoto wao.

Makingi alisema siyo kila jambo la wanafunzi kuachwa mikononi mwa walimu tu, kadhalika alikumbusha kuwasaidia watoto katika kuwalea katika maadili mema ili kulifanya taifa kuwa na raia wema na viongozi wazuri na waadilifu wa baadaye.

 

Monday, 3 August 2015

Shule ya Hazina ilipoibuka kidedea katika mtihani wa utamilifu mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka 2015



Wanafunzi wa shule ya msingi Hazina walioshika nafasi ya kwanza hadi ya 10 katika mtihani wa utamilifu mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka 2015 wakiwa katika picha ya pamoja na walimu wao baada ya kutangazwa washindi jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
SHULE ya msingi ya Hazina imeshika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Dar es Salaam katika mtihani wa utamilifu wa darasa la saba uliofanyika Juni 4 na 5 mwaka huu.

Ofisa Elimu mkoa wa Dar es Salaam Raymond Komba aliipongeza shule hiyo, ambayo pia ilitoa mwanafunzi wa kwanza hadi wa 10 katika mtihani hiyo.

Majengo ya shule ya Msingi Hazina yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, ambako wanafunzi walioshika nafasi 10 katika mtihani wa Utamilifu na kuzipita shule zote za mkoa huo.
Komba aliyasema hayo katika kikao cha watendaji wa elimu mkoa wa Dar es Salaam, walimu wakuu, wazazi na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo wa majaribio.

Aliipongeza shule ya Hazina kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika matokeo yote yaliyojumuisha shule za binafsi pamoja na zile za serikali, huku wanafunzi wake wakishika nafasi ya kwanza hadi ya 10.
Usafiri sio tatizo katika shule ya Hazina, Hilo ni moja ya mabasi ya shule hiyo ambayo hufanya wanafunzi kutohangaika katika usafiri.
 Wanafunzi wa shule hiyo walioshika nafasi ya kwanza hadi ya 10 ni Rajabu Said, Atif Mustifa, Zauditu Ally, Baraka Juma, Tatiana Ally, Warda Agapiti, Witness Jonas Mallosa, Henry Flowin Madiwa, Henry Godfrey Msuya na Ismail Khaliphan.

Jumla ya wanafunzi 58,489 kati ya 59,709 waliosajiliwa walifanya mtihani huo kwa mkoa wa Dar es Salaam, huku shule ya Kijitonyama Kisiwani ikiibuka ya kwanza kwa upande wa shule za serikali pekee.
Mapunda alisema kuwa ufaulu wa kila shule ndio unaotafsiri ufaulu wa wilaya na kuamua ufaulu wa Manispaa kwa ujumla, hivyo alizitaka shule kungeza juhudi wakati wa kuelekea katika mtihani wa taifa wa darasa la saba utakaofanyika Septemba 9-10.

Pia, ofisa huyo elimu alizipogeza shule za mkoa wa Dar es Salaam kwa kushika nafasi ya kwanza katika mtihani wa taifa mwaka jana na kuwataka kufanya vizuri zaidi mwaka huu ili kuendelea kuishikilia nafasi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza Rajabu Said alisema kuwa wamefanya vizuri kutokana na jitihada za bila kuchoka za walimu wao pamoja na wao kuwa wasikivu na kuelewa kile wanachofundishwa.

Pia, aliahidi shule yao kuendelea kuibuka ya kwanza katika mtihani wa kitaifa utakaofanyika mwezi ujao.




 

Mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi katika mtihani huo kwa kushika nafasi ya kwanza, Rajabu Said akihojiwa baada ya kutangazwa mshindi.
Rajabu Said akipongezwa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Komba.

Sunday, 2 August 2015

Shule ya Msingi Hazina haina mpinzani mtihani wa Utamilifu 2015

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Komba (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule zilizofanya vizuri katika mkoa wake katika mtihani wa Utamilifu au Moko uliofanyika Juni mwaka huu, huku shule ya Hazina ikishika nafasi ya kwanza na wafunzi wake wakishika nafasi ya kwanza hadi ya 10 katika mkoa wa Dar es Salaam wakati wakielekea kufanya mtihani wa taifa.

Azam FC mabingwa wapya Kombe la Kagame

Mabingwa wa wapya wa Kombe la Kagame timu ya Azam FC wakishangilia na kombe lao mara baada ya kukabidhiwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.