· Ataka
wananchi kufuata masharti yaliyotolewa
· Asema
kuanzia kesho mitaa kupuliziwa dawa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akipimwa joto alipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam (JNIA). |
Na Bahati Mollel,TAA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kujipanga vyema kwa
kushirikiana na wahudumu wa afya kwa kuweka maji yenye dawa maalum ya kunawa
mikono na kupima joto la mwili kwa watu wote wanaoingia na kutoka maeneo ya
viwanja vya ndege, ili kuzuia kuingia zaidi kwa watu walioambukizwa ugonjwa wa
homa kali ya Mapafu inayosambazwa na virusi vya corona (COVID19).
RC Makonda ametoa pongezi hizo leo alipofanya ziara
kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, ambapo alianzia
jengo la Tatu la abiria ambalo linahusisha zaidi ndege zinazotoka nje ya nchi,
na baadaye kwenda Jengo la Pili la abiria lenye ndege zenye safari za ndani ya
nchi na pia nje ya nchi.
Amesema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na TAA
kwa kuhakikisha hakuna ongezeko la watu walioambukizwa wanaoweza kuingia nchini
kupitia Kiwanja hiki.
“Nimejionea mwenyewe kila kona kumewekwa sanitizers,
na pale nje lipo tanki kubwa lenye maji yenye dawa lazima kila mtu anawe, na
hata huku ndani abiria wanaowasili na wanaoondoka wanapimwa joto la mwili kwa
mashine ya mkono na ile ya scanner, hivyo ninaimani kwa udhibiti huu hakuna
maambukizi zaidi yanayoweza kutokea,” amesema Mhe. Makonda.
Hatahivyo, amesema pia kuanzia tarehe 25 Machi, 2020
asilimia 98 ya ndege zenye safari za nje hazitaingia nchini baada ya zenyewe
kufuta safari zao kutokana na kukosekana kwa abiria, hivyo itasaidia kwa
asilimia 80 ya abiria kupungua kuingia kwa kuwa ni nchi nyingi zimeweka
makatazo na kufunga mipaka yao.
“Sisi hatujafunga mipaka lakini hadi sasa idadi ya
abiria wakigeni imeshuka kwa kiasi kikubwa mfano ndege yenye kubeba abiria 250
sasa inabeba abiria 20, hivyo asilimia 80 ya abiria aidha wenyewe kutokana na
elimu waliyopata kutokana na huu ugonjwa wameona hakuna sababu ya kusafiri na
wengine baada ya kuona masharti yaliyowekwa ya kwenda nchi moja ama nyingine
wakaamua kukaa majumbani mwao, na hii inadhihirisha jinsi gani Mhe. Rais John
Pombe Magufuli aliposema kuwa kama unaona safari haina ulazima basi usiende,”
amesisitiza Mhe. Makonda.
Pia amesema mashirika ya ndege yamekuwa na
ushirikiano na JNIA kwa kutoa taarifa kabla ya kutua endapo wanaabiria mwenye
kuhisiwa anaugua ugonjwa huo, na ikifika taratibu za kumpeleka katika kituo
kilichoteuliwa zinachukuliwa.
“Tunashukuru sana tena na tena hapa JNIA wamesema
hata idadi ya wasindikizaji imepunguzwa ili kuondoa kabisa msongamano katika
majengo ya abiria, maana wakiwa wengi itakuwa shida zaidi endapo yupo ambaye
anamaambukizi,” amesema.
Pia amesema kwa sasa abiria wote wanaowasili kutoka
kwenye nchi zilizokuwa na maambukizi wanapekelekwa kwenye hoteli na hosteli
zilizoteuliwa na mkoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa siku 14 kwa gharama zao
wenyewe. Katika hatua nyingine amesema leo abiria 200 wa nchi ya Comoro
wamezuiwa kuondoka baada ya nchi yao kufunga mpaka kutokana na kuzuia
maambukizi ya corona.
Pia amewataka watu wote wanaoingia na kutoka nchini
kwa kutumia usafiri wa ndege, mabasi na meli kufuata utaratibu uliowekwa na
Mamlaka za juu ili kuepukana na maambukizi, ambapo pia amesema katika usafiri
wa umma (Daladala) watu wasipande likiwa limejaa kupita kiasi na amesisitiza
kuwa ugonjwa huu hauna umri kuwa vijana hawafi, hivyo wanajidanganya na wachukue tahadhari
zilizowekwa.
Hali kadhalika amesema wananchi na watu wote kutokuwa
na hofu kuanzia kesho Jumatano tarehe 25 Machi, 2020, Ofisi yake kwa
kushirikiana na Maafisa Afya watapulizia dawa kwenye mitaa ili kuua wadudu
mbalimbali; na ofisi yake itaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maradhi ya corona.