Tuesday 17 March 2020

Corona Yasimamisha Michezo Yote



Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetangaza kusimamisha kwa mwezi mmoja michezo yote inayokusanya watu wengi, ikiwa ni tahadhari ya kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona, ambao tayari umeshaingia nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (pichani) alitangaza hayo wakati akilihutubia taifa kwa njia ya radio na televisheni, kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya janga hilo la corona.

Kwa tamko hilo, kuanzia mechi za mchangani hadi zile za Ligi Kuu Tanzaia Bara na ile ya Zanzibar, zitakuwa zimesimamishwa kwa mwezi mmoja, kwani ligi hizo zinahusisha mkusanyiko wa watu wengi.

 “Tunatangaza kusimamishia rasmi michezo yote inayokusanya idadi kubwa ya watu, makundi ya watu kama Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la pili na Umishumta, Umisseta na mashindano ya mashirika ya umma na michezo mingine kwa kipindi cha mwezi mmoja,” alisema Majaliwa.

Alisema baada ya tamko hilo wizara yenye dhamana na michezo ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo watasambaza barua kwa mashirikisho yote nchini wakitakiwa kufanya hivyo.

Kabla ya kutolewa tamko hilo la jana, tayari Ofisi ya Rais, Tawala za  Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia  waziri wake, Selemani Jafo ilifuta Mashindano ya Shule za Msingi na Sekondari kuanzia hatua ya mashule, ambayo yalitarajia kuanza hivi karibuni.

Nchi kadha zikiwemo zile zenye ligi tano kubwa kama England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa zimesimamisha ligi zao hadi mwanzoni mwa mwezi ujao ili kuamgalia mwenendo wa jango hilo la corona, ambalo tayari limewakumba baadhi ya wachezaji wa ligi hizo.

Mbali na kusimamishwa kwa ligi kubwa Ulaya, Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limesogeza mbele fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 hadi mwakani kuanzia Juni 11 hadi Julai 11, 2021.

Pia Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ijumaa lilitangaza kusimamisha mechi zote za kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021) na jana ilitangaza kusimamisha fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan 2020), ambazo zingefanyika Cameroon mwezi ujao.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilitangaza kikao cha dharura ambacho kitafanyika leo jijini Dar es Salaam kuzungumza hatma ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusu janga la corona.

Kikao hicho pia kitajadili kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars inayoendelea kujiandaa na fainali za Kombe la Chan nchini Cameroon pamoja na mechi za majaribio za timu hiyo.

Rais wa TFF, Wallace Karia aliagiza Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuitisha kikao cha dharula leo kujadili mustakabali wa michuano hiyo wakati huu wa mlipuko wa virusi vya corona.

Karia alisema kikao hicho kitakachoanza saa 3:00 asubuhi kitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam.

“Ajenda kubwa katika kikao hicho ni kuangalia mustakabali wa ligi kutokana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona ambao umeingia nchini,”alisema Karia.

No comments:

Post a Comment