Mshindi wa mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Marathon 2020, Kiplagat akimaliza mbio hizo Moshi hivi karibuni. |
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya
Kilimanjaro, imekuwa mdhamini mkuu wa mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon
mfululizo toka zilipoanzishwa hadi sasa zinatimiza miaka 18.
Kauli hii inakuja siku chache baada ya kumalizika
mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2020 mjini Moshi ambazo
zilihusisha washiriki zaidi ya 11,000 na idadi kama hiyo ya watazamaji.
Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha, ambaye
alishuhudia msimu wa 18 Kili Marathon Machi Mosi mwaka huu, aliwapongeza
wadhamini hao huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kudhamini
mashindano mbalimbali katika kukuza mchezo wa Riadha Tanzania.
Msitha, alisema kwa miaka yote hiyo 18 kumekuwa na
mabadiliko makubwa Kilimanjaro Marathon na leo limekuwa tukio kubwa ndani na
nje ya nchi, hivyo Kilimanjaro Premium Lager wanapaswa kupongezwa na kuigwa na
wengine pia.
Aliongeza kuwa, mashindano kama hayo husaidia pia
kuleta umoja kwa jamii.
“Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wanaohitaji kutoa
udhamini katika matukio kama haya, kujitokeza kwani husaidia katika kuleta
umoja wa kipekee kwa jamii,” alisema.
Hivi karibuni, BMT ililiagiza Shirikisho la Riadha
Tanzania (RT), kupunguza tozo kwa waandaaji wa mbio za barabarani kutoka Sh.
Milioni 3 hadi Sh. Milioni 1.5 ili kuwasaidia waandaaji katika kuandaa matukio
yenye uhakika.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager,
Irene Mutiganzi amewashukuru watanzania na washiriki wote kwa kujitokeza kwa
wingi katika mbio za mwaka huu ambapo namba za mbio za km 42 na 21 ziliisha
mapema kabla ya muda wa mwisho uliotangazwa.
“Hii ni dhahiri kuwa mbio hizi zimekuwa maarufu sio
nchini tu ila hata nje ya nchi ndio maana sisi kama wadhamini tumekuwepo kwa
miaka 18 sasa tangu mbio ghizi zianzishwe,” alisema.
Wadhamini wengine waliofanikisha mbio za mwaka huu ni
TPC Limited, Simba Cement, Unilever, Absa Bank Tanzania Limited na watoa huduma
rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na
CMC Automobiles.
No comments:
Post a Comment