Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wakijifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani. |
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa
kucheza kesho dhidi ya timu ya taifa ya Kenya ‘Harembee Stars’ mchezo wa kwanza
wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan
2020) utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni muhimu kwa Stars kuhakikisha inatumia
vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri
ya kutinga raundi ya mwisho ya kufuzu. Timu hizo zitarudiana Agosti 4.
Stars inataka kulipiza kisasi hasa baada ya kufungwa
katika mchezo wa makundi kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) Misri
bada ya kuchapwa 3-2 licha ya kuongoza mara mbili.
Lakini mchezo wa leo utawahusisha wachezaji
wanaocheza ligi za nyumbani na Taifa Stars ndio inaonekana kuwa na faida zaidi
baada ya kuwa na asilimia kubwa ya kikosi chake kilichoenda Misri kupata uzoefu
mkubwa.
Iwapo watatumia vyema uwanja wa nyumbani
watajitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu.
Hatahivyo, Kenya sio timu ya kubeza kwani wako vizuri
na wanataka kuutumia mchezo huo kupata matokeo ili kujiweka vizuri kwa ajili ya
mchezo wa mwisho utakaofanyika Nairobi wiki ijayo.
Katika viwango vya ubora wa soka duniani bado Kenya
wako vizuri ukilinganisha na Tanzania, wanashikilia nafasi ya 107, huku ndugu
zao wakishika nafasi ya 137.
Kila mmoja ana nafasi ya kupata matokeo kulingana na
alivyojiandaa dhidi ya mpinzani wake kimbinu.
Mchezo huo utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa makocha
Ettiene Ndayiragije na wenzake walioteuliwa kukaimu nafasi ya Emmanuel Amunike
na Hemed Morocco.
Akizungumzia mchezo huo Kocha Ndayiragije alisema alisema
jana kuwa maandalizi yote yako vizuri na kwamba kinachohitajika kwa wachezaji
ni umakini kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Nahodha John Bocco alisema mchezo huo utakuwa mgumu
kwani kila mmoja atahitaji matokeo kujiweka katika nafasi nzuri, lakini
anaamini kwa morali walionao watapambana kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa
nyumbani.
Bocco aliwaomba Watanzania kutoenda uwanjani na
matokeo yaliyopita bali sasa wako vizuri kulipiza kisasi kwa kuhakikisha
wanapata ushindi katika mchezo huo.
Tanzania kwa mara ya mwisho ilishiriki fainali za
Chan zilipofanyika Ivory Coast 2009 ikiwa ni miaka 10 sasa, hivyo itataka mwaka
huu iweke rekosi tena kwa kufuzi fainali hizo.
Fainali za kwanza za Chan zilifanyika mwaka 2009 na
lengo la Shirikisho la Afrika (Caf) ni kutoa nafasi kwa wachezaji ambao
hawajasajiliwa nje ya nchi zao na kuwawezesha kujitangaza.
No comments:
Post a Comment