Mchezo wa netiboli nao utakuwepo katika bonanza hilo la michezo la Shimiwi. |
Na Mwandishi Wetu
BONANZA la Michezo la Shirikisho ya Michezo ya Wizara
na Idara za Serikali (Shimiwi) litafanyika jijini Dodoma Februari 2 na 3 kwenye
Uwanja wa Jamhuri, imeelezwa.
Tamasha hilo litatanguliwa na mkutano wa viongozi wa
michezo, ambao ni wenyeviti na makatibu wa klabu za michezo za Wizara, Idara
zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu
wa Shimiwi Moshi Makuka, mbali na mazoezi ya viungo na mbio za pole (jogging),
tamasha hilo litahusisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli na ule wa kuvuta
kamba.
Makuka alisema katika taarifa hiyo ni matumaini yake
kuwa waajiri watatoa ruhusa kwa wahusika ili kuhakikisha bonanza hilo la
michezo linafana kwa kushirikisha watu wengi bila kukosa.
Mkutano huo utafanyika Februari Mosi kuanzia saa 2:00
asubuhi na kufuatiwa na bonanza hilo litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia
Februari 2 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuanzia saa 12:30 asubuhi.
Alisema kuwa waajiri mbali na kutoa ruhusa, pia wanatakiwa
kuwapatia wafanyakazi wao nauli na posho ya kujikimu ili waweze kushiriki
vizuri katika mkutano na bonanza hilo la michezo katika siku zilizotajwa.
No comments:
Post a Comment