Monday, 21 March 2016

Vijana Temeke walivyomkaribisha mkuu mpya wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kwa jogging kuanzia Uwanja wa Taifa hadi viwanja vya Buliaga Temeke








Na Mwandishi Wetu
KLABU za mbio za pole pole `jogging wilayani Temeke zimemkaribisha rasmi Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na kumtaka awasaidie kujikwamua kiuchumi.

Makonda akizungumza katika hafla hiyo alizitaka klabu hizo za jogging wilayani Temeke kuwatimua viongozi wasioeleweka, ambao wamekuwa wakichelewesha maendeleo yao.

Hafla hiyo ya kumkaribisha  Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam ilifanyika kwenye Viwanja vya Buliyaga Temeke.

Alisema kuwa hataki kuona viongozi wa klabu za jogging kazi yao kubwa  kupita kwa wanasiasa kuomba pesa kutumia  majina ya vijana. 

Alisema kuwa kiongozi kama huyo atakuwa anawachelewesha katika mipango yao ya maendeleo, hivyo msimvumilie na badala yake mumuondoe haraka.

Aidha, Makonda alisema kuwa vijana wengi hawataki kufanya safari ya mapambano na hivyo kushindwa kufanikiwa kwani hawana nidhamu, hawana bidii na wala hawamuweki Mungu mbele. 

Alisema kuwa yuko tayari kuwasaidia vijana wa Temeke ili waweze kuondokana na umasikini, mradi tu wakubali kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kumuweka Mungu mbele.

Makonda alisema kuwa Aprili 10 atakutana na vijana wote wa jogging mkoa wa Dar es  Salaam pamoja na wanamichezo wote na wasanii ili kuzungumzia fursa za kujikwamua kiuchumi.

Pia Makonda alisema kuwa atatoa Sh  milioni 2 kwa kikundi cha jogging ambacho kitakuwa na mipango mizuri ya kujikwamua kiuchumi.

Naye msanii maarufu wa mashairi nchini, Mrisho Mpoto ambaye ndiye mratibu wa hafla hiyo alisema kuwa anguko la vijana wa Temeke liko mikononi mwa Makonda, ambapo alimtaka kuhakikisha vijana hao wanajikwamua katika umasikini.

Alisema kuwa chini ya Makonda wanataka kuiona kesho mpya ya Temeke, ambayo itatoa fursa kwa vijana kujikwamua kiuchumi tofauti na zamani.

Jumla ya klabu 66 za jogging kutoka wilaya ya Temeke vikiwa na jumla ya washiriki 2,000 walishiriki katika hafla hiyo, ambapo walianza kwa kukimbia na Makonda kwa kilomita saba kuanzia Uwanja wa Taifa hadi Viwanja vya Buliaga Temeke.





Msanii mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kabla ya kuanza mbio za pole `Jogging' zilizoanzia Uwanja wa Taifa hadi Temeke.












Baada ya kushiriki mbio za pole na baadae kufanya mazoezi na kuwahutubia vijana kwenye viwanja vya Buliaga Temeke, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikunywa chai kwa `mbilimbi' pamoja na viongozi wa jogging wa Temeke.



Arsene Wenger alia na mashabiki wa Arsenal kumzomea licha ya kushinda



Kocha wa Arsenal, Mfaransa Arsene Wenger akiwasili kabla ya mchezo wa timu yake na ile ya Everton wa Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Goodison Park jijini Liverpool mwishoni mwa wiki.
LONDON, England
ARSENE Wenger anakiri kuwa ameachwa na `maumivu baada ya mashabiki wa Arsenal kutokuwa na imani naye katika mechi za hivi karibuni.

 Ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya Leicester City mwezi Februari uliirejesha timu hiyo katika mbio za ubingwa, lakini vipigo kutoka kwa Manchester United na Swansea City na sare dhidi ya Tottenham viondoa matumaini kwa timu hiyo.

Kipigo cha jumla ya mabao 5-1 kutoka kwa Barcelona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na kufungwa nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Watford katika Kombe la FA kumeifanya Arsenal kusalimisha nafasi yake ya kutwaa taji msimu huu.

Mashabiki wameongeza upinzani dhidi ya kocha huyo mkongwe katika Ligi Kuu ya England, ambapo wametaka atimuliwe ili timu hiyo ifanye vizuri.

Pia mashabii wamekuwa wakimlaumu mmoja wa wamiliki wenye hisa kubwa katika klabu hiyo, Stan Kroenke.

"Kitu kinachoniuma sana ni kwamba katika kipindi muhimu cha msimu ndio tunacheza katika mazingira magumu,  

alisema Wenger baada ya Arsenal kurejea katika mstari kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Everton Jumamosi.

Baada ya mchezo wa Tottenham ambako tulicheza mchezo mzuri sana, tulicheza na wachezaji 10 dhidi ya 11 na tulitoka nyuma na kutoka sare ya mabao 2-2, kwa kweli sielewi kwanini sasa wakati tunahitaji kila mmoja awe nyuma yetu, tunakuwa na mvurugano.

"Kutoka katika vyombo vya habari, sawa. Lakini hata kwa mashabiki wetu? Ni ngumu kulipokea hilo.

Kitu kizuri kwa Arsenal kwa sasa ni kiwango cha kuvutia cha Danny Welbeck, ambaye alifunga bao lake la nne katika mechi tisa tangu arejee uwanjani kutoka katika maumivu wakati alipofunga bao katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Obama atua Havana,Cuba kwa ziara ya kistoria



Rais wa Marekani, Barack Obama akisalimia na baadhi ya wafanyakazi na familia zao nchini Cuba.

HAVANA, Cuba
RAIS wa Marekani Barack Obama amewasili nchini Cuba kwa ziara ya kihistoria katika kisiwa hicho na kuzungumza na kiongozi wa Kikoministi.

Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa rais wa Marekani kutembelea Cuba tangu yalipofanyika Mapinduzi ya mwaka 1959.

Akizungumza wakati wa kufungua tena ofisi ya ubalosi wa Marekani jijini hapa, aliita ziara hiyo kuwa ni ya kihistoria. Pia alitumia muda fulani katika katika jiji hilo kongwe.

Obama alikutana na Rais wa Cuba Raul Castro, lakini hakukutana na mwanamapinduzi mstaafu Fidel Castro, na wawili hao watazungumzia pia masuala ya biashara na mabadiliko ya siasa.

Rais huyo wa Marekani alitoka katika ndehe yake ya Air Force One akiwa na mkewe Michelle na watoto wake wawili wakike Sasha na Malia.

Akiwa ameshikilia mwamvuli, wawili hao walitembea wakielekea katika zuria jekundu akisalimiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez.
  
"Tukirejea nyuma mwaka 1928, Rais [Calvin] Coolidge alikuja hapa kwa meli ya kivita. Ilimchukua siku tatu kufika hapa, lakini mimi imenichukua saa tatu tu, Air Force One kutua Cuba na hii ni kituo chetui cha kwanza tangu tulipopaa.

Baadae Obama alianza kutembelea jiji la zamani la Havana.

Monday, 14 March 2016

Mabingwa TP Mazembe waanza kwa sare na Saint George ya Ethiopia



CAIRO, Misri
MABINGWA wa Afrika wameanza kwa sare ya mabao 2-2 kutetea taji la Ligi ya Mabingwa ugenini dhidi ya Saint George ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 bora.

Wakiwa chini ya kocha wao mpya Mfaransa Hubert Velud (pichani), Mazembe jana walijikuta katika wakati mgumu dhidi ya wapinzani wao hao wa Ethiopia.

Hatahivyo, mabingwa hao watetezi wameondoka Ethiopia wakiwa na faida ya mabao mawili ya ugenini kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika wikiendi ijayo jijini Lubumbashi, Kongo.

Saint George walipata bao la kuongoza katika dakika ya 11 wakati Assefa Behaile alipowafanya wenyeji kuwa mbele kwa bao 1-0.

Mghana Daniel Nii Adjei aliisawazishia Mazembe, huku bao la kujifunga la Isaac Isiende yaliwapatia mabingwa hao watetezi uongozi wa mabao 2-1 hadi kipindi cha pili.

Saint George waliongeza presha kwa wapinzani wao na kufanikiwa kusawazisha kwa bao lililofungwa na Girma Adane na kufanya matokeo kuwa mabao 2-2.

Kwingineko katika mechi zilizofanyika Jumapili, kocha mpya wa Zamalek Alex McLeish alifurahia ushindi wa timu yake wa bao 1-0 dhidi ya Union Douala nchini Cameroon katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kocha huyo wazamani wa Scotland, McLeish amekuwa kocha wan ne wa Zamalek msimu huu baada ya kocha Mreno, Mbrazil na Mmisri kutimuliwa katika timu hiyo.

Baada ya miaka kadhaa ya kupigania kutoshuka daraja England akiwa na timu ya Birmingham City na majirani zao wa Aston Villa, McLeish yuko mbioni kutwaa taji akiwa na Zamalek, ambayo imewahi kushinda taji la Afrika katika vipindi vitano.

Zamalek ilianza vizuri jijini Douala huku beki wa Burkina Faso Mohamed Koffi akifunga bao la ushindi katika dakika ya 59.

Jumamosi, Al Ahly, ambao ni majirani wa Zamalek walijikuta wakitoka suluhu dhidi ya Recreativo Libolo nchini Angola. Kwa sasa Ahly inafundishwa na Mholanzi Martin Jol kocha mwingine wa timu ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Kwingineko, timu ya Nigeria ya Enyimba ilitawala mchezo wao wa nyumba dhidi ya Vital'O ya Burundi, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa Port Harcourt.