Friday, 3 February 2017

Cameroon yaifunga ghana 2-0 na kuifuata Misri fainali Afcon itakayopigwa Jumapili



Wachezaji wa timu ya taifa ya Cameroon wakishangilia bao lao la pili walipocheza nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (afcon) dhidi ya Ghana. Cameroon ilishinda mabao 2-0.



LIBRAVILLE, Gabon
FAINALI ya Kombe la Mataifa Afrika, AFCON, itachezwa kesho, ambapo timu ya Cameroon itaumana na Misri huku Ghana ikiwa imekosa kwa mara nyingine kucheza fainali hizo.

Katika mchezo wa Cameroon na Ghana timu zote zilicheza kwa kiwango kizuri huku kila mmoja akijitaidi kufanya vema, ambapo Cameroon ilionekana kutumia vema nafasi ilizozipata na kuibuka na ushindi wa 2-0.

Mchezaji wa Cameroon, Michael Ngadeu-Ngadjui mnamo dakika ya 72 aliandikia bao la kwanza timu yake hiyo huku mwenzake Christian Bassogog akiandika bao la ushindi zikiwa zimebakia dakika za mwisho mchezo kumalizika.

Ghana kwa upande wake kupitia wachezaji wake akina Wakaso Mubarak na Christian Atsu iliendelea kusaka mabao bila ya mafanikio.
 
Wakaso anaechezea timu ya Panathinaikos  nafasi ya kiungo aliachia shuti kali kuelekea lango la Cameroon lakini liliondolewa na kipa Fabrice Ondoa, mwenzake Atsu saw anaechezea New Castle alipiga shuti lakini lilipita juu la lango la Cameroon.

Ghana iliibuka na ubingwa wa kombe hilo mwaka 1982 huku Cameroon ikiwa imecheza na kufikia hatua za juu pia kwenye michuano hiyo.

Kwa upande wake kocha wa Cameroon, Hugo Broos amesema kuwa ni sawa na ndoo iliyokuja kuwa kweli ka timu yake kufikia hatua hiyo ambapo mara ya kwanza kucheza fainali tangia mwaka 2008 ilipopoteza dhidi ya Misri.

Alisema kuwa timu kama ya Ghana ina uzoefu na michuano mbalimbali mikubwa lakini kwa timu yake imeweza kufanya tangia kuanza kwa michuano hiyo.

Alisema"ninakipenda kikosi changu na kuwa nina imani nacho sana kwa kuwa wachezaji wangu wamekuwa wakicheza kwa amani na uwezo wa hali ya juu kila wakati".

Alisema kuwa wachezaji wake walicheza licha ya kuwa timu shindani, Ghana, ilikuwa na wachezaji wakubwa kama akina Andre Ayew na kaka yake Jordan pamoja na Asamoah Gyan.

Beki wa Cameroon Ngadeu-Ngadjui ambae anachezea timu ya Slavia Prague alionesha umahiri mkubwa kwenye safu ya ulinzi huku akiisaidia kupata bao la kwanza kwa itmu yake hiyo.

Aliachia shuti kali lililomwacha beki wa Ghana John Boye na kipa wake Razah Brimah wasijue la kufanya.


YANGA YAITISHA SIMBA KWA KUICHAPA STAND UNITED MABAO 4-0 UWANJA WA TAIFA



Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Tanzania Bara Yanga leo walizidi kujichimbia kileleni baada ya kuichapa Stand United ya Shinyanga kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo ni mkwara mzito kwa Simba katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo baada ya wiki iliyopita kuwatoa kileleni. Wekundu hao wa Msimbazi leo wanacheza na Majimaji ya Songea katika mchezo utakaofanyika ugenini.

Yanga imefikisha pointi 49 ikiwa ni pointi nne zaidi ya Simba, ambayo leo itacheza na Majimaji ya Songea na hata ikishinda itakuwa nyuma kwa pointi moja.

Yanga katika mchezo huo walipata bao la kuongoza katika dakika ya 19 lililofungwa na Doland Ngoma kwa kichwa akiunganisha wavuni mpira wa Simon Msuva.

Baada ya kushindwa kufunga katika dakika ya 11, Msuva alisahihisha makosa yake katika dakika ya 27 pale alipoifungia timu yake bao la pili baada ya krosi ya Ngoma.

Stand United ambao katika mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania Bara Yanga walishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, nusura wafunge katika dakika ya 26 wakati Jacob Massawe aliposhindwa kuutumbukiza mpira wavuni akiwa nje ya 18.

Dakika ya 38, Stand walikosa tena bao baada ya Seleman Selembe kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alipiga mpira uliopanguliwa kifundi na kipa wa Yanga Munish aliyeupangua kabla ya kuudaka.

Yanga waliakianza kipindi cha pili kwa bao lililofungwa na Chirwa huku Msuva akikosa penalti katika dakika ya 58 baada ya kupaisha mpira.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya Revocatus Richard kufanya madhambi ndani ya 18, lakini Msuva alipiga shuti lililopa juu ya lango.

Mkongwe Nadir Haroub alifunga bao la nne kwa Yanga katika dakika ya 68 kwa kichwa akiunganisha wavuni kona iliyochongwa na Juma Abdul.

Vikosi vilikuwa:-
Yanga:Deogratius Munis, Nadir Haroub, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani/Vicend Andrew, Justine Zulu, Simon Msuva, Thabiti Kamusoko, Donald Ngoma, Obrey Chilwa na Haruna Niyonzima/Emmanuel Martin.

Stand United: Sebastiane Stanley/Mohamed Makaka, Jacob Massawe, Erick Mulilo, Adeyum Ahmed, Revocatus  Richard, Ibrahim Job, Abdulaziz Makame, Adam Salamba/Kheri Rashid, Frank Khamis, Absalim Chidiebele na Seleman Selembe.

Thursday, 2 February 2017

Makonda `ajilipua' amtaja Wema, TID, Chid Benz, askari 9 vinara wa dawa za kulevya



 Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amejitoa mhanga kwa kuagiza kuswekwa ndani kwa askari Polisi zaidi ya tisa wa mkoa huo pamoja na kuwataka wasanii maarufu nchini akiwamo aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi, akiwatuhumu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mbali na Wema ambaye alikuwa Miss Tanzania 2006 na kwa sasa ni mwigizaji maarufu, Makonda akawataka wasanii wengine maarufu kujisalimisha leo katika kituo hicho jijini Dar es Salaam, wakiwemo Khaleed  Mohamed (TID), Winfrida Josephat (Recho), Khery Sameer (Mr Blue), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu) na Rashid Makwiro (Chid Benz).

Makonda anakuwa kiongozi wa kwanza nchini kujitokeza hadharani na kutaja wahusika au watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kwa majina, baada ya miaka mingi wanasiasa kuishia kueleza kuwa wanayo majina ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu yenye fedha nyingi, lakini hawakuyataja hadharani.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Makonda aliwataja askari hao kwa jina moja moja ambao ni Swai, Neri, Willy, Mkomeo wote wa Kituo cha Polisi Oysterbay, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, Inspekta Fadhil wa Kinondoni, Steven wa Kinondoni, James wa Kinondoni, CP Dotto wa Kituo cha Kijitonyama na WP Glory wa Kituo cha Kawe.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Mkuu wa mkoa huyo pia amewataka wamiliki wenye leseni za kuendesha sehemu za starehe ambazo zinasadikika kujihusisha na uuzaji wa dawa hizo, kujisalimisha leo saa tano katika Kituo Kikuu cha Polisi wakiwemo wamiliki wa George Dragon, Element na Cuba Bar.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kushoto) akishiriki katika mbio za pole pole au jogging Temeke jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mrisho Mpoto au Mjomba.
Makonda ambaye kabla ya uteuzi wake aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliwaambia waandishi wa habari kwamba amefikia hatua hiyo baada ya kufanya msako wa kuwakamata wahusika wa dawa za kulevya katika mkoa huo na baadhi ya wananchi kuwataja askari hao kuwa wanahusika kuwaficha wauzaji wa dawa hizo.

Alisema baada ya msako, wananchi walikuwa wanawataja wahusika wa dawa hizo, lakini polisi hawawajui ndipo alipopata taarifa kuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, jambo linalofanya kushindwa kutokomeza dawa hizo katika mkoa huo.

“Kwa mamlaka niliyonayo nataka wakamatwe kama wapo ndani ya mkoa au nje waletwe na wawekwe mahabusu pale Central, watoe maelezo kwa nini wananchi wanawataja, kuna wengine wanatajwa kuwapigia simu wahusika wakati wakienda kuwakamata na wanatumiwa hela kupitia simu zao, hizi ni tuhuma na wao wana nafasi ya kujieleza,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda aliwataja baadhi ya watu wanaosadikika kuwa ni wafanyabiashara wa dawa hizo ambao tayari wameshakamatwa akiwemo Ahmed Ngahemela (Pettit man), Said Lina maarufu kama Alteza, Nassoro Nassoro, Bakari Khelef pamoja na Omary.

“Wapo wengi, lakini hawa ndio tayari tumewakamata na wengine wamekutwa na dawa hizo, tunaendelea na msako ambao nitauendesha mimi mwenyewe nikishirikiana na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, lengo ni kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya katika mkoa huu (Dar es Salaam) inatokomezwa,” alifafanua Makonda.

Makonda pia ametoa siku saba kutokomezwa kwa vijiwe na maeneo yote yanayojihusisha na uuzaji dawa za kulevya katika mkoa huo.
 Kamanda-Jeshi-la-Polisi-Kanda-Maalum-ya-Dar-es-Salaam-Simon-Siro.
“Mnafahamu nipo na Kamishna Sirro na kamati yake baada ya siku saba nitawaambia kama watashindwa kutokomeza dawa za kulevya Dar es Salaam maana yake wamekosa sifa za kuendelea kuwa askari katika mkoa wetu, kwa kuwa wameshindwa kuwafahamu wauzaji,” alibainisha Makonda.

Naye Kamanda Sirro alisema atalizungumzia hilo kwa waandishi wa habari atakapokutana nao leo.