Sunday, 6 November 2016

MAISHA MAGIC BONGO YAZINDULIWA RASMI NA KUIPAISHA JUU BONGO MOVIES



Mgeni rasmi pamoja na waheshimiwa wengine wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguaji wa uzinduzi.
Na Mwandishi Wetu
MAISHA Magic Bongo kwa kushirikiana na maprodyusa wa filamu nchini wameleta mapinduzi  makubwa kwenye sanaa ya filamu za Kibongo.

Palikuwa na full shangwe na vifijo  kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam siku ya  Ijumaa, Novemba 4,  2016. Shangwe hii ni baada ya Maisha Magic Bongo kwa kushirikiana na Multichoice Tanzania kuzindua rasmi chaneli yao ya (160) Maisha Magic Bongo. Miongoni mwa waalikwa walikuwa waigizaji maarufu na maprodyusa wa filamu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Maharage Chande akizungumza katika hafla hiyo.
 Uzinduzi huu ulilenga kwenye kusheherekea kazi nzito za maprodyusa wetu wa filamu hapa nyumbani , na utambulisho rasmi wa chaneli yetu yenye mandhui ya kitanzania. Chaneli hii imelenga kuburudisha na kuelimisha watazamaji wetu wa kitanzania kupitia filamu, tamthiliya, na maigizo mbalimbali ya Kiswahili. 
Mkurugenzi Mkuu wa MNET, Yalisa Phawe akizungumza. Kulia ni Mkuu wa Chaneli ya Maisha Magic Bongo, Barbara Kambogi.
 Chaneli hii inapatikana kwenye kifurushi cha huduma za DStv (160). Uzinduzi huo ulifuatiwa na maonesho ya tamthilia ya kimapenzi ya “Huba”, na vidokezo vya video za mambo yajayo yaliyoandaliwa kwenye chaneli ya Maisha Magic Bongo. Watazamaji wetu wajiandae kwa uhondo zaidi kupitia vipindi vijavyo vya “Harusi Yetu”, 
Mwenyekiti wa Bodi ya DSTV, Balozi Ami Mpungwe.
Movi za kihindi zenye tafsiri ya Kiswahili kama “Doli”, na filamu mbalimbali kuanzia msimo mpya wa Februari 2017.

Wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, Mkuu wa chaneli ya Maisha Magic Bongo Barbara Kambogi alisema “Tumefurahia kupata fursa ya kuwapatia watazamaji wetu wa kitanzania chaneli ya Maisha Magic Bongo yenye mandhari halisi ya Kiswahili.

Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo.
Tumebahatika kusheherekea maadhimisho yetu ya Maisha Magic Bongo kutimiza mwaka mmoja. Pamoja na hayo, tunatambua mchango mkubwa wa maprodyusa wa filamu za kitanzania katika kushirikiana nasi. 

Kwani kwa pamoja tumeweza kuiendeleza tasnia yetu ya kitanzania. Ndugu zangu, huu ni mwanzo tu wa Maisha Magic Bongo na tunatarajia kusonga mbele. Tutaendelea kushirikiana na maprodyusa wa filamu za hapa nyumbani, kwani sasa tumewapa fursa maprodyusa wetu kutusaidia kuitangaza sanaa yetu ya Tanzania kwenye masoko ya nje.”

Maisha Magic Bongo chaneli (160) imewaandaliwa mambo mazito na ya uhakika ili kuburudisha  wateja wetu  na kujivunia utanzania wetu kupitia kazi nzito za maprodusa na waigizaji wetu.

Mgeni rasmi alimalizia kwa kuishukuru Maisha Magic Bongo kwa kuisogeza mbele sanaa ya filamu ya Tanzania na kuendeleza vipaji vya maprodyusa wetu kupitia kazi zao nzuri.”

Tuesday, 1 November 2016

Simba kuwavaa kiboko wa Yanga Africans, Azam FC katika mtanange wa Ligi Kuu leo Jumatano



Na Mwandishi Wetu
SIMBA, Yanga na Azam zinashuka dimbani leo kwenye viwanja tofauti kwenye michuano ya Ligi Kuu Soka Tanzania bara kila mmoja ikisaka pointi tatu muhimu.]

Hata hivyo, mchezo utakaovuta hisia za wapenzi wengi wa michezo ni ule wa Simba na Stand United utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, kwani wapiga debe hao walizikalisha Yanga na Azam FC zilipocheza hapo.

Simba ndio kinara ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza michezo 12 na kushinda 10 ikitoka sare mara mbili. Kwa upande wa Stand United imecheza michezo 13, imeshinda mitano, sare saba na kupoteza mmoja ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 22.

Timu hiyo ya Shinyanga iko vizuri msimu huu na imekuwa ikizishtukiza timu kubwa kwenye Uwanja wa Kambarage, ikijivunia kumchapa Yanga bao 1-0 na Azam FC bao 1-0 na kutamba kuwa hata Simba itakaa chini pia.

Iwapo kama kuna timu itafungwa basi yuko hatarini kupitwa na wenzake katika mbio hizo za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo itakuwa na mvutano wa aina yake kwani mashabiki wa soka watataka kuona kama Stand FC  itaendeleza ubabe kwa vigogo au ilibahatisha kwa Yanga na Azam tu.

Uongozi wa klabu ya soka wa Stand United imeahidi ushindi katika mchezo wao wa leo dhidi ya klabu ya Simba.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Athuman Bilal aliahidi kuwa watapambana kufa au kupona ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

Bilal alisema timu yake imejiandaa vyema isipokuwa mshambuliaji wake Abasirim Chidiebele bado majeruhi yanamsumbua. 

Mchezaji huyo wa timu ya Pamba fc alisema vijana wake wako safi na ni lazima washinde mchezo huu. 

Yanga ambao wako katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo atakuwa na mchezo dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya. 

Timu hiyo ya Jangwani huenda ikaendelea kupambana kutafuta matokeo mazuri ili kukimbizana na wapinzani wao Simba wanaotesa kileleni. 

Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 katika michezo 12, ikishinda minane, sare tatu na kupoteza mmoja. Wametofautiana na wapinzani wao kwa pointi tano.

Mbeya City yenye pointi 16 katika michezo 13 iliyocheza sio timu ya kubeza hasa inapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Sokoine, ambapo amekuwa ikihitaji matokeo.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye uwanja huo Mei mwaka huu, Yanga ilishinda mabao 2-0. Lakini lolote linaweza kutokea kwani huu ni msimu mwingine.

Azam FC itakuwa Mwanza kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba dhidi ya Toto Africans. Timu hiyo ya Chamazi haikuwa vizuri katika michezo kadhaa iliyopita, lakini katika michezo kama miwili iliyopita imeonesha mwanga kuwa inarudi baada ya kushinda.

Azam FC imeshacheza michezo 12, imeshinda mitano, imepata sare nne na kupoteza mitatu hivyo, ikishika nafasi ya nne kwa pointi 19. 

Toto Africans licha ya kuwa iko vibaya msimu huu baada ya kucheza michezo 13 na kujivunia pointi 11 kwa nafasi ya pili kutoka mwisho, huwa haitabiriki hasa inapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani. Kila mmoja anahitaji kushinda kujiweka pazuri.

Katika mechi hizo hasa kwa Simba, Yanga na Azam FC, wachezaji ambao huenda wakaendeleza rekodi zao za ufungaji ni Shiza Kichuya wa Simba anayeongoza kwa magoli nane, akifuatiwa na Amis Tambwe wa Yanga mwenye saba na John Bocco wa Azam mwenye magoli sita.

Timu inayoongoza kwa safu bora ya ushambuliaji ni Yanga ikiwa imeshafunga magoli 27 na kufungwa matano, ikifuatiwa na Simba yenye magoli 24 ikifungwa matatu, ikifuatiwa na Azam FC iliyofunga 17 na kuruhusu 11 kupenya kwenye nyavu zao.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni Ndanda FC dhidi ya Tanzania Prisons, Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon na Majimaji dhidi ya JKT Ruvu.

Timu hizi kila mmoja anahitaji ushindi ili kujiweka vizuri, kwani bado wanasaka pointi zaidi ili kufanya vizuri.

Kilimanjaro Health Marathon kufanyika Desemba 4 Mjini Moshi



Na Mwandishi Wetu
MBIO za tatu za Kilimanjaro Health Marathon 2016 zitafanyika mjini hapa Desemba 4, imeelezwa.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Moshi, Mkurugenzi wa Community Vission & Better Future, Luka Ndalima alisema mbio  hizo zitakuwa za kilometa 10, 5 na tatu.

Alisema zinatarajia kuanza na kumalizikia katika viwanja vya Majengo Mjini Moshi.

Ndalima alisema lengo la mbio hizo za kila mwaka ni kutoa elimu ya afya katika Siku ya Ukimwi Duniani pamoja na ile ya Walemavu, ambazo zote hufanyika Desemba.

Siku ya Ukimwi Duniani hufanyika Desemba mosi wakati ile ya walemavu nayo hufanyika mwezi huo huo, hivyo tumeamua kuzisherehekea pamoja Desemba 4, wikiendi ya kwanza ya mwezi Desemba," alisema Ndalima.

Alisema kuwa pia mbio hizo zinatumika kutoa elimu ya afya na kuwataka kutowaficha ndani walemavu na badala yao wawatoe na kuwapatia elimu kama watoto wengine.

Alisema mafunzo watakayotoa ni kuwaelimisha watu kuhusu kujikinga na maambukizo mapya ya Ukimwi hasa kwa upande wa vijana.

Alisema mwaka jana walishiriki jumla ya wakimbiaji 1,200 huku watu wazima wakiwa 800 na watoto ni 400, ambapo mwaka huu wanatarajia kupata washiriki wengi zaidi.

Thomas Mashali kuagwa leo mchana Leaders Club na kuzikwa makaburi ya Kinondoni Dar es Salaam



Na Mwandishi Wetu
MWILI wa bondia wa ndondi za kulipwa nchini, Thomas Mashali aliyeuawa Kimara jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumatatu, utazikwa leo kwenye makaburi ya Kinondoni.

Baba mzazi wa marehemu, Malifedha Mashali alisema kuwa mwili wa mtoto wake huyo aliyeuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana, utazikwa katika makaburi ya Kinondoni Mwembejini.

Alisema mipango mingine ya mahali utakapoagiwa mwili huo na utakapoombewa, bado ilikuwa inaendelea na alikuwa hajajua shughuli hizo zitafanyikia wapi.

Mzee Mashali alisema kuwa mwili wa mtoto wake utaagwa katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni kuanzia saa 7 mchana kabla ya kwenda kupumzishwa katika nyumba yake ya mileleni katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 
Mashali alikuwa akishikilia mikanda ya WBO na UBO kabla ya kifo chake, ambapo amekufa huku akiacha mataji kibao ya ngumi ya hapa nchini na yale ya kimataifa.

Wadau wengi wa michezo walitoa masikitiko yao kuhusu kifo hicho cha Mashali huku wengi wao wakisema kuwa bondia huyo alikuwa na kipaji cha aina yake katika ndondi.

Mashali alizaliwa Dar es Salaam mwaka 1989 na alianza kupigana ngumi za kulipwa Novemba 27, 2009 alipopigana na kumtwanga Hamadu Mwalimu katika pambano lililofanyika katika ukumbi wa Texas, Manzese.