Wednesday, 13 April 2016

Mwadui v Azam, Yanga na Coastal Union nusu fainali Kombe la Shirikisho

Na Mwandishi Wetu
RATIBA ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imefanyika usiku wa jana, huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata nafasi ya kucheza nyumbani.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Yanga wakipata nafasi ya kucheza michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.

Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku Wagosi wa Kaya Coastal Union wakicheza dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga siku hiyo hiyo.

Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya kombe hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).

Wakati huohuo, wadhamini wa michuano hiyo Azamtv kupitia kituo chake cha michezo cha Azam Sports, walilionesha hadharani kwa mara ya kwanza kombe la ubingwa na kulikabidhi kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine.

Monday, 11 April 2016

Simba yafungwa na Coastal Union na kutolewa Kombe la FA




 Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo imeonja chungu ya kufungwa baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Kombe la FA katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba imetupwa nje ya mbio za kusaka nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika. Bingwa wa FA hushiriki Kombe la Shirikisho la Afrika mwakani.

Coastal Union wako katika hatari ya kushuka daraja katika Ligi Kuu Tanzania Bara kufuatia kushika mkia katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 26 wakati Simba wanaoongoza kwa kuwa na pointi 57 baada ya kushuka dimbani mara 24.

Katika mchezo huo, Coastal Union ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika la 19 lililofungwa na Yusuph Sabo baada ya kupiga mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Coastal Union walikuwa mbele kwa bao hilo moja licha ya Simba kutawala zaidi kipindi hicho.

Kipindi cha pili kilipoanza Simba ilifanya mabadiliko, ambapo iliwatoa Said Ndemla na Justice Majbvi na kuwaingiza Hamisi Kiiza na Awadhi Juma.
Kiiza aliisawazishia Simba baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Ibrahim Ajibu katika dakika ya 51.

Dakika ya 83 Yusuph Sobo aliifungia Coastal Union bao la pili kwa penalti baada ya Novaty Lufunga kumchezea vibaya Ahmed Shiboli ndani ya eneo la hatari. Lufunga alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na rafu hiyo.

Naye Grace Mkonjera anaripoti kuwa, ratiba ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la TFF, inatarajiwa kufanyika leo  usiku kuanzia  saa 3 usiku na kurushwa  moja kwa moja kupitia kituo cha luninga cha AzamTwo.

Coastal inaungana na timu za Azam FC, Mwadui FC, na Yanga SC zilizotangulia kucheza nusu fainali ya mashindano hayo.

Katika mechi za Ligi Kuu Simba imeifunga Coastal mara mbili, ambapo mara ya kwanza ilishinda 1-0 Oktoba 28, 2015 kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuichapa tena 2-0 Machi 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Sasa Simba ambayo haijashiriki michuano ya kimataifa kwa miaka kadhaa, huenda mwakani ikaendelea kukaa kando baada ya kubaki na nafasi moja tu ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Afrika, endapo itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Saturday, 9 April 2016

Uchukuzi Sports Club yajifua kwa mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika Dodoma


Timu ya soka ya Uchukuzi Sports Club ikifanya mazoezi wakijiandaa kwa mashindano ya Mei Mosi

Na Cosmas Mlekani
TIMU ya Uchukuzi Sports Club imetamba kufanya vizuri katika mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika mjini Dodoma kuanzia Aprili 16 mwaka huu.
Wachezaji wa Uchukuzi Sports Club wakijifua kwa ajili ya Mei Mosi.
Mwenyekiti wa timu hiyo inayoundwa na wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mohamed Ally alisema kuwa yake itafanya vizuri katika mashindano hayo.

Ally alisema kuwa kwa sasa wako katika mazoezi makali kujiandaa na mashindano hayo, ambayo yatafikia kilele chake Mei Mosi mjini Dodoma.

Akinana wa Uchukuzi wakijifua kwa ajili ya kuvuta kamba.
Alisema Uchukuzi Sports Club ina timu za soka, netiboli, kuvuta kamba, bao, karata, riadha, baiskeli na vishale.

Alisema kuwa wana uhakika timu yao kutamba katika mashindano hayo ya Mei Mosi kutokana na kufanya maandalizi kabambe chini ya makocha wa kimataifa na wazoefu.

Ally aliwataja baadhi ya makocha ho kuwa ni pamoja na Kenny Mwaisabula, Robert Damian, Terry, Kingsley Malwilo na Abunu Issa, ambao wameifanya timu yao ya soka kuwa tishio kwa timu zingine.

Alisema kuwa timu zao hizo zimekuwa zikicheza mechi kibao za majaribio ili kuwawezesha makocha kubaini makosa na kufanya marekebisho ya mwisho kabla timu hiyo haijaondoka kwenda Dodoma.

Naye Meneja wa Uchukuzi Sports Club, Damiani alisema kuwa timu yao inatarajia kwenda Dodoma Aprili 14 tayari kwa mashindano hayo.

Alisema timu ya soka na netiboli zimefanya majaribio kadhaa ili kujiweka fiti kwa mashindano hayo, ambayo wana uhakika wa kutwaa ubingwa.
Kikosi kabambe cha timu ya soka ya Uchukuzi kikiwa pamoja na kocha na meneja wa timu hiyo Robert Damiani (kushoto).

Wednesday, 6 April 2016

Al Ahly yatua na kikosi cha wachezaji 21 tayari kuivaa Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa



Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Al Ahly ya Misri imetua nchini leo alfajiri tayari kwa pambano lao la Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Yanga litakalofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Pambano hilo ni la hatua ya 16 bora, ambapo timu hizo zitarudiana siku 10 zijazo nchini Misri ili kusaka timu itakayotinga hatua ya makundi.

Timu hiyo imekuja na wachezaji wakali 21 pamoja na kocha wao Martin Jol, ambaye alianza kuifundisha timu hiyo mwezi uliopita baada ya kumwaga wino.

Kocha wa Al Alhy, MMartin Jol mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere leo alfajiri.
Kocha huyo wa Ahly amewaita wachezaji wake wote wakali ambao wamo katika safari hiyo.

Pambano hilo linakumbushia lile la mwaka 2014, ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly kabla ya kufungwa bao kama hilo na kufanya mchezo huo kuamliwa kwa matuta, ambapo Yanga ilifungwa 4-3.

Said Bahanuzi na Mbuyi Twitte ndio walioikosesha Yanga ushindi baada ya kukosa penalti zao katika mchezo huo uliofanyika jijini Cairo, Misri.

Katika kikosi hicho, Jol amewaacha beki Mohamed Naguib, kiungo Saleh Gomaa na Ahmed Hamdy, ambacho kimetua leo tayari kwa mchezo huo.

Mchezaji aliyepona hivi karibuni misuli, Sherif Ekramy ameitwa baada ya kuwa nje ya uwanja tangu Februari,pamoja na kipa wa akiba Ahmed Adel akichukua nafasi katika mechi zilizopita.

Al Ahly imetinga hatua ya 16 bora baada ya kuifungisha virago Recreativo ya Angola kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-0, wakati Yanga walipinya baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

Yanga walishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Amavubi jijini Kigali, Rwanda kabla ya kutoka sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Ahly:

Makipa: Sherif Ekramy, Ahmed Adel na Mosad Awad.

Mabeki: Ahmed Fathi, Bassem Ali, Mohamed Hani, Saad Samir, Rami Rabia, Ahmed Hagazy na Sabri Rahil.

Viungo: Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Amr El-Sulaya, Ahmed El-Sheikh, Walid Soliman, Moemen Zakareya, Ramadan Sobhi na Abdalla El-Said.

Washambuliaji: Malick Evouna, Amr Gamal na Emad Meteb.
Yanga wenyewe wako Chake Chake Pemba wakijifua kwa ajili ya pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na la kuvutia huku Al Ahly wakitaka kuendeleza makali yao na Yanga kulipa kisasi cha kutolewa mwaka 2014.