Na
Mwandishi Wetu
MAMLAKA
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeungana na Mbunge wa Viti Maalum na
Wakazi wa Mkoa wa Tabora kusaidia jitihada zao za kutokomeza mimba za utotoni
kwa kutoa msaada wa tani 12.5 za saruji kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya
wanafunzi wa kike wa shule za sekondari.
Akikabidhi
saruji hiyo hivi karibuni katika Kata ya Itonjanda, Manispaa ya Tabora, kwa
niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi
Julius Ndyamukama, ambayo ni sawa na mifuko 250 ya saruji, Kaimu Meneja
wa Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Rose
Comino, amesema TAA, ipo bega
kwa bega katika suala zima la kusaidia jamii katika masuala mbalimbali likiwemo
la Elimu, ambapo watoto wote ni sawa na wanastahili kupata elimu na sio
kukatizwa masomo kutokana na vikwazo mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni.
Rose amesema Wananchi wa Tabora waungane kwa pamoja
kuunga mkono jitihada za Mbunge wa Viti Maalum Munde Tambwe la ujenzi wa mabweni
kwa ajili ya watoto wa kike wa shule za sekondari, ambao wanatembea umbali
mrefu kwenda shule, ambapo sasa wanatokomeza mimba za utotoni na kushirikiana
kuwabaini wale wote wenye kutenda matendo hayo maovu.
“Kwa pamoja tuoneshe jitihada za dhati kwa
kuhakikisha watoto wetu wanakuwa sehemu salama mabwenini, nina uhakika wa
asilimia 100 kwa 100 tutapata watoto wengi wa kike watakaomaliza shule na
kufanya vizuri katika masomo yao,” amesema Rose.
Amesema TAA ni miongoni mwa taasisi ya serikali
iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na.30
ya mwaka 1997 na kupewa dhamana na
Serikali ya kuvisimamia na kuviendesha jumla ya viwanja 58, imekuwa ikitekeleza sera yake ya kurudisha
kwa Jamii katika masuala mbalimbali yakiwemo ya elimu.
Rose amesema viwanja vya ndege vinatoa fursa
mbalimbali za kibiashara zikiwemo za kuendesha migahawa, hoteli, maduka ya
bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa mizigo ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi.
Pia viwanja vya ndege vimekuwa miongoni mwa eneo
linalozalisha ajira rasmi na zisizo rasmi, ambazo zinahusisha mashirika
mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yenye kutoa huduma katika maeneo ya viwanja
vya ndege.
Naye Tambwe ameushukuru uongozi mzima wa TAA kwa kusaidia jitihada hizo, ambazo
anauhakika kwa lengo alilojiwekea ataweza kusaidia ujenzi wa mabweni mengi katika
kila kata ya Mkoa wa Tabora.
“Naomba
ndugu zangu tuunge mkono jitihada hizi nilizoanzisha, na pia kuungana na Rais John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure, mimi nimezaliwa hapa Tabora na
nimeona jinsi gani mabinti zetu wanavyotembea umbali mrefu kwenda na kurudi
shule jambo ambalo linachangia kupata vishawishi njiani na kujikuta wanapata
mimba za utotoni.” Amesema Tambwe.
Hatahivyo,
amesema mifuko 100 kati ya hiyo 250 itapelekwa kwenye Kata ya Itonjanda, ili
ujenzi uanze mara moja, na 150 iliyosalia itapelekwa kwenye shule nyingine.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itonjanda ameshukuru msaada huu
uliotolewa na TAA kwani watoto wamekuwa wakitembea umbali wa Kilometa 10 kwenda
shule, na wamekuwa wakiathirika kutokana na kupata mimba.
“Tumuunge
mkono Rais wetu kwani Tanzania bila elimu haitaenda tuunge jitihada hizi kwani
watoto wanakuwa wananawiri sana wanapoingia shule za sekondari, kwani wamekuwa
wakipewa fedha ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikiwaponza na kujikuta wanapata
ujauzito, ” amesema.
No comments:
Post a Comment