Bondia Michael Yombayomba wakati wa uhai wake. |
BONDIA wazamani wa ndondi wa ridhaa nchini, Michael Yombayomba amefariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani baada ya kuugua tumbo, imeelezwa.
Baba Mdogo wa bondia huyo, David Yombayomba alisema leo kuwa mtoto wao huyo alilazwa Tumbi kutokana na tatizo ya tumbo kujaa gesi na kutapika kila anapokula chakula kabla kifo hakijamtuka.
Alisema kuwa mazishi ya bondia huyo wazamani ambaye ni bingwa wa Jumuiya ya Madola wa uzito wa bantam, yatafanyika kesho Jumanne Kibaha mkoani Pwani.
Yombayomba ni bondia pekee wa Tanzania hadi sasa
aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka
1998, alifariki juzi katika hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani,
baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.
Kwa miaka mingi, Tanzania ilikuwa ikirejea na medali
kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, lakini ikiwa ni katika mchezo wa
riadha huku ndondi na michezo mingine wakirejea mikono mitupu hadi pale Yombayomba
alivyofanya kweli.
Yombayomba alitwaa medali hiyo akiwa chini ya kocha
mkongwe na wa muda mrefu wa ndondi hapa nchini Locken Swai ndiye alikuwa kocha
wake bondia huyo alipokuwa akitwaa medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola
Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998.
Faida ya
Medali:
Yombayomba alitwaa ubingwa huo wa bantam na mara
aliporejea nchini aliyekuwa Mkuu wa Polisi (IGP), Omary Mahita alimpandisha cheo kutoka
askari polisi wa kawaida hadi kuwa na sajini (V3).
Yombayomba baada ya kuwa sajeni wa jeshi hilo,
alibadilika na mara kwa mara akiwa katika sare za kazi alikuwa akishika kifimbo
mkononi.
Baada ya muda alihamishwa kutoka katika Jeshi la
Polisi na kupelekwa katika kikosi cha Kuzuia Ghasia Ukonga, ambako hakudumu
sana kabla ya kufukuzwa kazi.
Michael Yombayomba (kushoto) akivishwa glovu na kocha Timothy Kingu kabla ya bondia huyo hajaanza mazoezi katika ukumbi wa Mlimani Park jirani na Mlimani city miaka kadhaa iliyopita. |
Hakufaidi
Usajini
Yombayomba alidumu na cheo hicho kwa miaka mitatu tu
kabla hajafukuzwa kazi.
Hatahivyo, baada ya kufukuzwa kazi kwa bondia huyo
kulikuwa na maneno mengi huku baadhi wakidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada
ya kuwa mlevi wa kupindukia na wengine wakidai ni utoro katika kambi ya taifa
kwa ajili ya maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika London
2002.
Yombayomba alikuwa hafichi unapozungumza naye kwani
alikuwa akitupa lawama kwa kocha wake wakati huo (jina tunalihifadhi), kuwa
alishindwa kumtetea wakati yeye ndiye aliyempa ruhusa ya kwenda kuaga familia
yake kabla ya kwenda London.
David Yombayomba; Baba Mdogo wa Michael. |
Inaelezwa kuwa wakati wa kambi hiyo ya Jumuiya ya
Madola, viongozi wa Kamati ya Olimpiki (TOC) wakati huo walitembelea kambi na
hawakumkuta Yombayomba, na walipouliza kocha akasema hayupo na wala hajui
aliko.
Baada ya kutimuliwa ndipo mabosi wake nao wakajuu
wakimtaka bondia huyo kueleza sababu za kutoroka kambini.
“Baada ya vyombo
vya habari kuandika habari hizo za utoro, bosi wangu aliamuru nifunguliwe
mashtaka na baadae nikatimuliwa kazi, lakini kwa chuki za kocha huyo ambaye
hakupenda mimi niwepo katika timu hiyo, ambayo nilitarajia kwenda kutetea
ubingwa wangu wa Jumuiya ya Madola, “alisema na kuongeza:
“Huyo kocha alikuwa na chuki zake binafsi
kwani alijua nikiendelea kuwepo katika kambi hiyo atashindwa kufanya maovu yake
akaamua kunizushia uongo ili niondolewe katika timu na bahati mbaya nikafukuzwa
na kazi, “anasema Yomba Yomba.
Medali ya
Dhahabu:
Katika hostori ya ndondi za ridhaa Tanzania hakuna
bondia yeyote aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya
Madola, isipokuwa Yombayomba peke yake.
Katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 50 ya Uhuru wa
Tanzania Bara, katika ndondi za ridhaa hakuna bondia kama huyo aliyewahi kutwaa
medali ya dhahabu katika michezo mikubwa kama hiyo ya Jumuiya ya Madola.
Mabondia wengine wa Tanzania tangu ilipokuwa
Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar kama akina Rashind Matumla, Haji
Matumla, Makoye Isangura, Titus Simba (marehemu), na wengineo, waliwahi
kutamba katika michezo kama ile ya Mataifa ya Afrika, Afrika na Afrika
Mashariki, lakini sio ile ya Jumuiya ya Madola.
Kiujumla, Yombayomba ni bondia aliyepata mafanikio
zaidi kwa kipindi chote miongoni mwa mabondia wa Tanzania kutokana na kufikia
hatua hiyo.
Sasa ni miaka 17 tangu alipotwaa medali hiyo nchini
Malaysia.
Wanavyomzungumzia:
Kocha Swai anasema kuwa Yombayomba alikuwa bondia
mwenye kipaji cha hali ya juu na alitumia vizuri mkono wake wa kushoto
(northpole) kuwachakaza wapinzani wake.
Kocha huyo anasema kuwa mara nyingi mabondia
wanaotumia mkono wa kushoto wako wachache na huchezaji wao ni tofauti kabisa na
wale wanaotumia mkono wa kulia.
Anasema kuwa, bondia huyo alikuwa mjanja na aliweza
kuwasambaratisha wapinzani wake.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT),
Makore Mashaga anasema wamempoteza shujaa wa ndondi ambaye bado mabondia
chipukizi walikuwa wakihitaji mawazo na ushauri wake katika kupiga hatua katika
mchezo huo.
Anasema BFT wako pamoja na familia ya Yombayomba
katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
Kocha wa timu ya taifa, Jonas Mwakipesile alisema kuwa
Yombayomba alikuwa bondia mzuri wakati akicheza na rekodi yake itakumbukwa
daima.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya BFT, ambaye ni
bondia wazamani Anthony Mwang’onda alisema itachukua muda mrefu kwa mabondia
wasasa kufikia rekodi ya Yombayomba.
Yombayomba mbali ana kupata cheo hicho, hata kazi ya
upolisi aliipata baada ya kutwaa ubingwa wa taifa katika mashindano ya taifa
yaliyofanyika Arusha mwaka 2002.
Bondia huyo alitwaa medali ya dhahabu ya uzito wa
bantam baada ya kumchapa Mcameroon, Herman Ngoudjo kwa jumla ya pointi 19-13 na
kuitoa Tanzania kimasomaso.
Yombayomba ameacha mke na watoto wawili, Scola na
Zacharia.
Mungu ailaze roho ya marehemu Michael Yombayomba
mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment