Thursday, 22 December 2016

ukungu wavuruga safari za ndege kwa wanaotaka kwenda kula Krismas sehemu tofauti Uingereza



LONDON, England

UKUNGU katika maeneo yote ya kusini mashariki yamevuruga ratiba za ndege kwenye viwanja vya Heathrow, Gatwick na City, imesema Shirika la Ndege la Uingereza la British Airways.

Sintofahamu hiyo jijini hapa iliibuka wakati watu wakisafiri kwa ajili ya kwenda kusheherekea Siku Kuu ya Krismas, ambako walionywa kutarajia mvurugano kuzunguka Uingereza yote wakati kimbunga Barbara kikaribia kutokea.

Ofisa mmoja wa hali ya hewa alisema hali mbaya ya hali ya hewa inatarajiwa kesho Ijumaa na Jumamosi, huku ukungu ukitarajiwa kutokea zaidi katika sehemu za Scotland.

Kumetolewa tahadhari kibao sehemu kubwa ya kaskazini ya Scotland “kujiandaa” kuhusu hali hiyo mbaya ya hali ya hewa.

Multichoice-Tanzania yatoa msaada msimu wa Krismasi kwenye Kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madima Tandale




Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice-Tanzania, Maharage Chande akizungumza kabla ya kukabidhi msaada kwa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Al-Madina. Kushoto ni Mlezi wa kituo hicho, Kuruthum Yussuf leo.

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Multchoice-Tanzania mapema leo imekabidhi msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. Milioni 5 kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Msaada huo uliohusisha sare za shule, unga wa ngano, unga wa mahindi, biskuti, juice za aina mbalimbali, soda, mafuta ya kupikia, mchele na nguo zingine ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Maharage Chande kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, ambao baadhi yao aliambatana nao hadi Uswazi.

Vingine walivyokabidhi leo ni pamoja na vyombo vipya kabisa vya kulia chakula, fedha taslimu za kusaidia kulipia gharama zao za pango wanapoishi watoto hao na vitu vingine.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi msaada huo, Chande alisema kuwa kampuni yao kwa miaka mingi imekuwa na mahusiano mazuri na kituo hicho cha Watoto Yatima cha Al-Madina, ambapo wamekuwa wakisaidia mara kwa mara.
Mbali na msaada huo wa vyakula, vinywaji na sare za shule na nguo, Multchoice-Tanzania pia imelipa pango la miezi sita la Kituo hicho, ikiwa ni moja ya changamoto inayokisumbua sana kituo hicho chenye watoto 60.

Chande alisema kuwa wataendelea kukisaidia kituo hicho pamoja na vingine ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii kupitia fedha wanazopata kwa kuuza ving’amuzi bora kabisa vya DStv, ambavyo vimekuwa vikinunuliwa kwa wingi.

Alisisitiza kuwa Multchoice-Tanzania itaendelea kushirikiana na kituo hicho ili kuhakikisha watoto wanasonga mbele kwani ndio taifa la kesho, ambapo kila mmoja wetu ana wajibu wa kujitolea kwa namna moja au nyingine.

Hii sio mara ya kwanza kwa Multchoice-Tanzania kukisaidia kituo hicho,  kwani miezi kadhaa iliyopita wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani walikabidhi cherehanui kadhaa, ambazo zinatumiwa kuendeleza kipato chao kwa kushona nguo na kuziuza.

Akitoa shukrani Mkuu wa Kituo hicho, Bi. Kuruthum Yussuf alimshukuru Chande na Multchoice-Tanzania kwa ujumla kwa misaada wanaokipatia kituo hicho kwa miaka mingi sasa.

Hatahivyo, Bi. Kuruthum alisema kituo chao kinakabiliana na baadhi ya changamoto kama ukosefu wa eneo kwani kituo kipo katika eneo dogo lililobanwa sana, ambalo linawafanya watoto washindwe kucheza na kufanya shughuli zingine.
Aliwataka watu na taasisi mbalimbali kujitokeza kusaidia kama wanavyofanya Multchoice, ambao wamekuwa wamkikisaidia kituo hicho bila ya kuchoka.
 
Baada ya kumalizika kwa hafla ya kukabidhi msaada huo, Chande alitembezwa katika kituo cha ushonaji, ambacho kiko meta chache kutoka kilipo kituo hicho cha watoto yatima.




 
 


 


Wednesday, 21 December 2016

Ukata waifanya Temeke kuutema ubingwa taifa Cup bila kuingia dimbani, wamkumbuka Mbunge wao wazamani Mtevu


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI mashindano ya taifa ya netiboli yanatazamiwa kuanza Desemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, mabingwa watetezi Temeke wameutema ubingwa huo hata kabla ya kuingia dimbani kwa sababu ya ukata.

Mashindano hayo yanashirikisha timu za mikoa, huku Halimashauri za Temeke, Ilala na Kindondo mkoani Dar es Salaam, kila moja ikipewa hadhi ya mkoa katika mashindano hayo yanayofanyika  kila mwaka.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania, Chaneta, Zainab Mbiro amesema leo kuwa mikoa ya Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Manyara, Arusha, Mara, Morogoro, Simiyu na Singida imethibitisha kushiriki  katika mashindano hayo.

Mbiro ambaye ni Mkuu wa Wilaya mstaafu alisema kuwa,  Dar es Salaam akiwa na maana Halimashauri zake zote tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni, hakuna iliyothibitisha kushishiriki katika mashindano hayo.

Katibu Mkuu wa timu ya Temeke, ambayo ndio bingwa mtetezi, Amina Mussa amethibitisha leo kuwa, ukata umewafanya washindwe kuthibitisha kushiriki mashindano hayo,  licha yao kuwa mabingwa watetezi.

Temeke imelitwaa taji hilo kwa mara tatu mfululizo na kama ingeshiriki mwaka huu na kulibeba, ingekuwa imelitwaa kwa mara ya nne mfululizo.

Amina alisema kuwa pamoja na jitihada zao kupeleka barua kwa mbunge wa Temeke, Meya na naibu Meya, lakini hadi sasa barua zao hazijajibiwa lolote na wamepoteza matumaini ya kusaidiwa na watu hao.

Alisema kuwa Mbunge aliyepita wa Temeke, Zuberi Mtemvu ndiye alikuwa mlezi wa timu hiyo na aliisaidia sana katika maandalizi yake na kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.

Alisema kuwa timu yao tangu Mtemvu ashindwe Ubunge imekuwa ikitapatapa, ambapo ilishindwa kushiriki hata mashindani ya Ligi Daraja la Kwanza yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro na hawajui hatma yao kama watashushwa daraja kwani walishindwa hata kulipia ada.

“Viongozi hao tuliwaandikia barua ya kuwajulisha kuhusu mashindano hayo ya Morogor, lakini hadii hii leo tunaongea na wewe hakuna majibu na hatujui hatma yetu kama tutashushwa daraja au kufungiwa, “alisema Amina na kungeza:

“Tangu Mtemvu atoke madarakani Temeke tumekuwa watu wa kusuasua katika michezo,  kwani viongozi wetu wa sasa wako kimya kabisa hawajasema lolote.”

Amina aliwaomba wafadhili mbalimbali kujitokeza ili kuisaidia timu hiyo ambayo bado inaendelea na mazoezi kila siku na wako tayari kwa mashindano mbalimbali yatakayojitokeza.

Tuesday, 20 December 2016

MATIP WA LIVEROOL NAYE AUNGANA NA WENZAKE SITA KUGOMA KUICHEZEA CAMEROON AFCON 2017 GABON



LONDON, England
JOEL Matip wa Liverpool ni miongoni mwa wachezaji saba wa Cameroon, ambao wamesema kuwa hawana mpango wa kuichezea timu ya taifa lao katika mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon), inayotazamiwa kuanza Januari 14 mwakani.

Beki huyo alikuwa na “maelewano mabovu” na benchi la ufundi huko nyuma, kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot).

Beki wa West Brom, Allan Nyom naye pia ni miongoni mwa wachezaji saba waliogoma kuichezea timu hiyo ya taifa katika Afcon.

Fecafoot italiomba Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) mchezaji huyo afungiwe kucheza katika klabu hake kwa wiki tatu za mashindano hayo ya Afrika.

Kocha wa timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos alisema: "Wachezaji hawa wameweka mbele maslahi yao badala ya yale ya taifa na shirikisho la soka lina haki ya kuchukua hatua dhidi yao kwa mujibu wa kanuni za Fifa.

Beki wa kati-Matip, 25, alijiunga na Liverpool kwa uhamisho huru katika kipindi cha majira ya joto kutoka klabu ya Bundesliga ya Schalke, ambapo ameichezea Liverpool mechi 14 msimu huu.

Nyom, aliyemwambia kocha Broos kuwa anataka kubaki West Brom ili kutetea namba yake katika timu hiyo, alijiunga na Baggies akitokea Watford katika kipindi cha dirisha la mwisho la usajili. 

 Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 naye ia ameichezea klabu yake mechi 14 hadi sasa.

Wachezaji wengine watano wa Cameroon, abao wamegoma kucheza Afcon ni pamoja na  Andre Onana (Ajax Amsterdam), Guy N'dy Assembe (Nancy), Maxime Poundje (Girondins Bordeaux), Andre-Frank Zambo Anguissa (Olympique Marseille) na Ibrahim Amadou (Lille).

Wachezaji wote hao saba maema mwezi huu walitajwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 35 kwa ajili ya mashindano hayo, ambao kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wwa timu hiyo kinatarajiwa kutangazwa wiki ijayo.

Cameroon katika mashindano hayo imepangwa pamoja na wenyeji Gabon, Burikina Faso na Guinea, ambao watacheza katika Kundi A.