Friday, 13 January 2017

Mrisho Ngasa aipa somo timu yake yazamani Yanga kama inataka kufanya vizuri



Na Mwandishi Wetu
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayechezea Mbeya City, Mrisho Ngasa amesema Yanga inahitaji wachezaji wawili wa kuchezesha timu ili kuwa na uwiano mzuri.

Akizungumza na gazeti hili, Ngasa alisema Yanga inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho.

“Ukiangalia Yanga wanavyocheza kwa sasa, unaona kabisa inakosa watu wa kuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho kama alivyo  Haruna Niyonzima ili wawe na uwiano mzuri katika timu, lazima wawapate hao watu,”alisema Ngasa.

Pia Ngasa alisema sababu hiyo ndio chanzo cha Yanga kufanya vibaya katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba.

“Mechi ilikuwa nzuri, Simba waliwazidi Yanga katikati kwani walikuwa wanacheza mipira mirefu kumtumia Msuva peke yake, hivyo Simba wakagundua njia hiyo, baada ya kusogea pembeni wakaua mipango ya Yanga," alisema Ngasa.

Ngasa alisema wachezaji wengi wa Yanga kwa sasa wamechoka baada ya kucheza michezo mingi ya kimashindano, hivyo miili yao inahitaji kupumzika.

Taifa Stars yapangwa kundi jepesi kinyang'anyiro cha kufuzu Mataifa ya Afrika Cameroon 2017


Na Mwandishi Wetu
 ALIYEKUWA Kocha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Charles Mkwasa amesema kilio chake kimesikika na hatimaye Tanzania imepangwa kwenye kundi rahisi kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2019.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa ambaye ameifundisha Taifa Stars akirithi mikoba ya kocha Mdenmark Mart Nooij amesema timu ambazo zipo kundi moja na Tanzania ni rahisi ukilinganisha na kundi la msimu uliopita ambapo ilipanga na Nigeria na Misri.

“Timu zilizopangwa kundi moja na Tanzania ni timu za kawaida ukilinganisha na Misri au Nigeria lakini maandalizi ya mapema ni muhimu ili kufanya vizuri,” alisema Mkwasa.

Pia Mkwasa alisema pamoja na kuonekana kuwa rahisi lakini kitendo cha nchi hizi kuwa na viwango vinavyokaribiana kinaweza kufanya iwe ngumu zaidi kwa maana ya kukamiana.

“jukumu linabaki kwa shirikisho la Soka (TFF), wachezaji pamoja na benchi la kiufundi kujiandaa kwani nilisema hadharani tumekuwa tukipangwa kwenye kundi la kifo ila droo ya sasa CAF walisikia kilio changu na inawezekana iwapo tutaamua,” alisema Mkwasa.

Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na vinara wa soka ukanda wa Afrika Mashariki Uganda, Lesotho na Cape Verde, ambapo wengi wanasema ni jepesi ukilinganisha na huko nyuma ilibyokuwa ikipangwa Stars.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars' ambayo ipo ukanda huu wa Afrika Mashariki imepangwa kundi F sambamba na Ghana, Ethiopia na Sierra Leone.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema ratiba hiyo ni faraja kubwa kwa Tanzani kwani wadau wa soka wakiungana na TFF, “hakuna shaka tunaweza kufuzu kwa fainali hizo za 2019.”

Hatahivyo,Lucas alisema pamoja na kuwepo katika kundi linaloonekana jepesi, lakini bado maandalizi ya Stars yanatakiwa kuwa makubwa kwani Uganda na Cape Verd bado ni timu nzuri.

Alisema kuwa Uganda Cranes ni timu nzuri na itakuwa na hamu kubwa ya kucheza tena fainali hizo za mwaka 2019 baada ya kushiriki zile za mwaka huu nchini Gabon, ambazo zinaanza leo.

Wenyeji wa michuano hiyo Cameroon ambayo imefuzu moja kwa moja imepangwa kundi B pamoja na Morocco, Malawi na mshindi kati ya Comoro na Mauritius.

Wakati huo huo;  timu za Sao Tomé, Madagascar, Comoro, Mauritius, Djibouti na Sudan Kusini wataanzia kwenye mechi za mtoano Machi na mataifa matatu yataingia kwenye hatua za makundi.

Jinsi makundi yalivyopangwa:

Kundi A: Senegal, Equatorial Guinea, Sudan, Sao Tome/Madagascar

Kundi B:  Cameroon, Morocco, Malawi, Comoro/Mauritius

Kundi C: Mali, Gabon, Burundi, Djibouti/Sudan Kusini.

Kundi D: Algeria, Togo, Benin Gambia.

Kundi E: Nigeria, Afrika Kusini, Libya, Shelisheli.

Kundi F: Ghana, Ethiopia, Sierra Leone, Kenya.

Kundi G: DR Congo, Congo Brazzaville, Zimbabwe, Liberia.

Kundi H: Ivory Coast, Guinea, Jamhuri ya Afrika ya kati, Rwanda

Kundi L: Burkina Faso, Angola, Botswana, Mauritania.

Thursday, 12 January 2017

DStv KUONESHA FAINALI ZA AFCON GABON 2017 KWA BEI MCHEKEA!



Multchoice-Tanzania Wahakikisha shoo ya Diamond inafunika
 
Jumatano January 11, 2017

ILI kuwapa watanzania wengi uhakika wa kushuhudia michuano ya kombe Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017, 

Kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia king’amuzi chake maarufu cha DStv, itaonyesha michuano hiyo katika kifurushi chake cha bei ya chini kabisa maarufu kama DStv Bomba. Kifurushi hicho kinachopatikana kwa bei ya sh 19,975 tu, ni miongoni mwa vifurushi vya bei nafuu katika huduma ya ving’amuzi hapa nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandisha wa habari leo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Multichoice Tanzania Salum Salum, ametanabahisha kuwa kwakuwa DStv ndicho king’amuzi pekee kitakachoonyesha michuno hiyo mubashara kupitia chaneli yake ya michezo ya SuperSport4 (DStv 204), wameamua kuiweka michuano hiyo kwenye kifurushi cha bei nafuu kabisa cha Bomba, ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kuiona michuano hiyo moja kwa moja.

“Tunajivuna kuwa na sisi Tanzania tumepiga hatua kubwa sana na sasa hatuna sababu yoyote ya kuona michezo iliyerekodiwa, bali na sisi tunaitazama mubashara kupitia king’amuzi chetu bora cha DStv, tena kwenye kifurushi nafuu cha Bomba” alisema Salum na kuongeza kuwa kwa kuwa hii itawapa nafasi watanzania wengi kufurahia michuano hiyo kila mahali ikiwemo kwenye kumbi za burudani na hata majumbani.

Wakati huohuo, DStv na Wizara ya Habari Utamaduni Michezo na Sanaa, imefanikisha safari ya Mwanamuziki wa kizazi kipya hapa nchini Nasibu Abdul (Diamond) katika kufanikisha onyesho lake katika ufunguzi wa mashindano ya AFCON nchini Gabon.

Diamond ni miongoni mwa wasanii teule watakaotumbuiza katika hafla hiyo kitendo ambacho kimechukuliwa na watanzania wengi kuwa ni fursa ya Tanzania kusikika katika mashindano hayo japokuwa timu yetu haikuweza kufuzu kushiriki.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, utamaduni, michezo na sanaa Nape Nnauye alisema kuwa kuwepo kwa Diamond kwenye uzinduzi wa michuano hiyo ni kitendo cha kujivunia na kwamba serikali ikishirikiana na DStv imefanya jitihada kubwa kufanikisha safari ya WCB kuelekea Gabon.  

Kwa upande wake Diamond aliishukuru Serikali na DStv kwa ushirikiano wao hususan kufanikisha safari yao ya kuelekea Gabon. Aliongeza kuwa jitihada binafsi za Waziri wa Habari ziliwezesha zoezi hilo kufanikiwa na kwamba wanaahidi kuwa hawaendi kama WCB, bali kama watanzania na watahakikisha kuwa wanaipeperusha vema bendera ya Tanzania katika onyesho hilo.

Michuano ya AFCON ya mwaka huu inanogeshwa zaidi na uwepo wa wachezaji nguli ulimwenguni hususan wale wanaochezea vilabu vikubwa kama Manchester United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid na vilabu vingine vikubwa duniani. Wababe wa kabumbu kama Mohamed Elneny, Eric Bailly, John Obi Mikel, Pierre Aubemayang, Riyad Mahrez, Sadio Mane na Victor Moses ni miongoni mwa vigogo watakaoonyesha umahiri wao katika michuano hiyo.

Mtifuano huo wa AFCON mwaka huu unafanyika katika nchi ndogo ya Gabon, huku jumla ya timu 16 zikishiriki ikiwemo Uganda ambayo ndiyo timu pekee iliyofuzu kutoka Afrika Mashariki.

Tayari vuguvugu la michuani hiyo limeshaanza kushika kasi mitaani ambambo mashabiki wa timu mbalimbali wamekuwa wakitambiana kila mmoja akidai timu yake itanyakua ubingwa mwaka huu. 

Michuona ya AFCON 2017 inadhaminiwa na kampuni ya Total, na itaanza tarehe 14 January na fainali itakuwa tarehe 05 Februari. Tayari ratiba kamili ya michuano hiyo imeshatolewa na inapatikana katika tovuti ya www.dstv.com.

Wednesday, 11 January 2017

Mourinho akerwa na wachezaji wake kushangiliaji bao la Mata



LONDON, England
JOSE Mourinho amewakosoa wachezaji wake kwa kushangilia kupita kiasi bao la kwanza la Juan Mata wakati Manchester United ikiibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Hull City.

Manchester United waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali ya mashindano hayo.

Iliwachukua Man United dakika 56 kuvunja ngome ya Hull City na kufunga bao katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Mata alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira wa kichwa uliopigwana Henrikh Mkhitaryan.
Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Man United kushangilia kwa muda mrefu, kitendo ambacho kilimkera Mourinho ambaye alibainisha hilo baada ya mchezo huo.

"Tulitakiwa kucheza badala ya kutumia muda mrefu kushangilia bao, “alisema kocha hiyo alipozungumza na Sky Sports. "Katika kila mchezo wa kombe kila bao ni muhimu hivyo kwanini mnashangilia wakati mna nusu saa ya kucheza?

"Sifiki kama tulitakiwa kufanya vile, hakuna sabbau ya kushagilia bao la kwanza namna ile.”

Maelezo hayo yalikuja wakati Mourinho akiwataka wachezaji na mashabiki wa timu yake kuelekeza nguvu zao katika mchezo ujao dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa  Old Trafford utakaofanyika Jumapili.

Alipoulizwa kama alikatishwa tama na kiwango cha timu yake katika kipindi cha kwanza, kocha huyo wa United aliongeza: "Ndio kidogo. Kwa kweli hatukuwa katika kiwango chetu kipindi cha kwanza.

"Ndio, Hull walijipanga vizuri kama nilivyotarajia na haikuwa rahisi kwetu….”