Friday, 6 January 2017

Mahrez wa Leicester City ndiye mchezaji bora wa Afrika wa mwaka wa Caf


Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Algeria na Leicester Riyad Mahrez akipozi kwa picha baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika katika hafla iliyofanyika jana usiku jijini Abuja, Nigeria.

ABUJA, Nigeria
MSHAMBULIAJI wa Leicester Riyad Mahrez ndiye mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka 2016, Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) limetangaza.

Mchezaji huyo wa Algeria mwenye umri wa miaka,25, aliyeisaidia Leicester kutwaa taji la Ligi Kuu ya England, tayari ndiye mchezaji bora wa PFA wa mwaka na yule wa BBC.

Mshambuliaji wa Gabon anayeichezea klabu ya Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang alikuwa wa pili na Msenegal wa Liverpool Sadio Mane alimaliza watatu katika mbio hizo za kuwania uchezaji bora.

Mshambuliaji wa Arsenal na Nigeria Alex Iwobi alishinda tuzo ya mchezaji chipukizi wa mwaka.

Mchezaji mwingine wa Nigeria anayekipiga katika klabu ya Manchester City, Kelechi Iheanacho alikuwemo katika orodha ya wachezaji waliokuwa wakiwania heshima hiyo.

Mahrez, 25, alimshinda nahodha wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye alipata heshima hizo mwaka jana, lakini juzi aliishia katika nafasi ya pili.

Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Ufaransa alisema kuwa ni heshima kubwa sana kwake kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka uliomalizika.

"Ni heshima kuubwa, nina furaha na ninashukuru. Nawashukuru wachezaji wenzangu wote Leicester na Algeria," alisema Mahrez wakati akipokea tuzo hiyo.

"Natoa tuzo hii kwa familia yangu na wote wanaoniunga mkono kila siku.”

Leicester ilishangaza pale ilipotwaa ubingwa wa England wakati ilikuwa haipewi nafasi yoyote hata ya kubaki katika ligi hiyo msimu uliopita.

Mahrez alifanya kazi kubwa katika klabu yake baada ya kufunga mabao 17 na ksaidia kupatikana kwa 10 katika mechi 37 alizoichezea timu hiyo.

Alikuwa mchezaji wa kwanza wa Algeria kushinda taji la Ligi Kuu na kupata mapokezi makubwa aliporejea nyumbani Algeria, ambako kwa mara ya kwanza alifikiriwa kuwa ni mchezaji wa rugby alipotakiwa kujiungta na timu hiyo miaka minne iliyopita.

Wachezaji wote watatu waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika pia walichaguliwa katika kikosdi cha CAF cha wachezaji 11, ambacho pia kinaundwa na beki wa Ivory Coast Eric Bailly wa Manchester United.

Kipa Denis Onyango alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani baada ya kumshinda mchezaji mwenzake wa Mamelodi Sundowns Khama Billiat na Mzambia Rainford Kalaba.

Onyango alifanya vizuri wakati klabu yake ya Mamelodi Sundowns ilipotwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika, na kuisaidia timu ya taifa ya Uganda `The Cranes’ kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu.

Mnigeria Asisat Oshoala alitwaa tuzo yake ya pili ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika kwa wanawake baada ya kuisaidia Nigeria kutetea taji la Afrika nchini Cameroon.

Nyota huyo wa timu ya wanawake ya Arsenal alishinda kwa mara ya kwanza tuzo hiyo wakati pia alipoweza kuisaidia Super Falcons kutwaa taji la Afrika mwaka 2014.

Wachezaji chipukizi wa Nigeria Kelechi Iheanacho na Alex Iwobi walitwaa tuzo ya wachezaji wanaochipukia vizuri na ile ya wachezaji chipukizi wa mwaka.

Mwamuzi wa Gambia Bakary Papa Gassama alishinda tuzo ya mwamuzi bora kwa mara ya tatu mfululizo.

WASHINDI WA TUZO

Mchezaji bora wa Afrika wa mwaka
Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)

Mchezaji bora wa mwaka anayecheza Afrika
Denis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mchezaji bora wakike wa mwaka
Asisat Oshoala (Nigeria & Arsenal)

Chipukizi mwenye kipaji cha aina yake
Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City)

Chipukizi bora wa mwaka
Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

Kocha bora wa mwaka
Pitso Mosimane (Mamelodi Sundowns)

Klabu bora ya mwaka
Mamelodi Sundowns

Timu bora ya taifa ya mwaka
Uganda

Timu bora ya taifa ya wanawake
Nigeria

Mwamuzi bora wa mwaka:
Bakary Papa Gassama

Kikosi cha CAF cha wachezaji 11 wa 2016

Kipa: Denis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mabeki: Serge Aurier (Cote d’Ivoire & PSG), Aymen Abdenour (Tunisia & Valencia), Eric Bailly (Ivory Coast & Manchester United) na Joyce Lomalisa (DRC &AS Vita).

Viungo: Khama Billiat (Zimbabwe & Mamelodi Sundowns), Rainford Kalaba (Zambia & TP Mazembe), Keegan Dolly (Afrika Kusini & Mamelodi Sundowns).

Washambuliaji: Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Borussia Dortmund), Sadio Mane (Senegal & Liverpool), Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City).

Wachezaji wa akiba: Aymen Mathlouthi (Tunisia & Etoile du Sahel), Kalidou Koulibaly (Senegal & Napoli), Salif Coulibaly (Mali & TP Mazembe), Islam Slimani (Algeria & Leicester City), Mohamed Salah (Misri & Roma), Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City) na Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

Sunday, 1 January 2017

Mourinho amtaka Martial kumsikiliza yeye na sio wakala wa mchezaji huyo ili aendelee kuichezea Manchester United



MANCHESTER, England
MSHAMBULIAJI wa Manchester United Anthony Martial anatakiwa "kunisikiliza mimi na sio wakala wake ", anasema kocha wa timu hiyo Jose Mourinho.

Wakala huyo Mfaransa aliripotiwa hivi karibuni akisema kuwa “anaangalia” uwezekano wa mteja wake kuhamia katika klabu ya Sevilla ya Hispania.

Martial,mwenye umri wa miaka 21, alikuwa mfungaji bora wa Man United msimu uliopita baada ya kufunga mabao 17, lakini bao lake la kusawazisha alilofunga jana Jumamosi wakati Manchester United ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Middlesbrough lilikuwa ni bao lake la tano kufunga msimu huu.

"Ni mchezaji wa ajabu na wa aina yake alikuwa mfungaji bora msimu uliopita, “alisema Mourinho.
"Martial alicheza, alitengeneza, pia alifunga. Alipambana, ni mchezaji mzuri. Najua ana kipaji cha hali ya juu sana.”

Martial, aliyejiunga na Man United akitokea Monaco kwa ada ya pauni mioni 36 mwaka 2015, alifanya kazi nzuri wakati timu yake ikitoka nyuma Jumamosi na kuibuka na ushindi huo dhidi ya Boro.

Alisawazisha kwa bao la dakika 85 kabla ya Paul Pogba hajafunga lile la ushindi dakika moja baadae.

Baadae, Mourinho alishauri kuwa Martial anatakiwa kufuata mfano wa mchezaji mwenzake wa timu hiyo Henrikh Mkhitaryan, aliyetakiwa na kocha wake kufanya zaidi, ambapo alijibu kwa kufunga mabao matatu katika mechi nne zilizopita.

Kocha huyo wazamani wa Chelsea aliongeza kusema: "Nilijua Mkhitaryan ni kipaji cha hali ya juu lakini nilikuwa simchezeshi. Kwa kipindi hiki hucheza hata beki ya kushoto wakati timu ikishinda na tunahitaji kulinda ushindi wetu na kuhitaji balansi zaidi.

"Martial anatakiwa kunisikiliza mimi na sio wakala wake. Anatakiwa anisikilize mimi katika mazoezi kila siku na katika kila mrejesho ninaompa kujaribu kumuimarisha na kumboresha zaidi.

"Huku Martial kika kukiha nasoma magazeti,  'Anthony Martial anakwenda Sevilla, Anthony Martial anakwenda kucheza kwa mkopo, Anthony Martial hana furaha'. Anthony Martial anachotakiwa ni kunisikiliza mimi na sio mtu mwingine yeyote.”

Beki wazamani wa United Phil Neville: "Nafikiri ni kitu rahisi. Klabu imewekeza kwa mchezaji huyo kiasi cha pauni milioni 56. Sasa ni jukumu lake kumuuliza wakala wake kwa nini anamuhusisha na kuhamia Sevilla na aseme kwa sasa niko katika moja ya klabu kubwa kabisa duniani. Nataka kuendelea kubaki Man United.”
Nahodha wazamani wa timu ya taifa ya England Alan Shearer: "Martial alikuwa mchezaji bora katika mchezo ule na aliweza kuirejesha Man United mchezoni. Na alicheza vizuri tangu mwanzo wa mchezo.”

WATU 39 WAUAWA KATIKA SHAMBULIZI LA KIGAIDI KATIKA KLABU YA USIKU JIJINI ISTAMBULI MKESHA WA MWAKA MPYA 2017





ISTAMBULI, Uturuki
KWA uchache watu 39, wakiwemo wageni 16, wamekufa katika shambulizi lililofanyika katika klabu ya usiku jijini hapa. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki amesema.

Suleyman Soylu pia alibainisha kuwa,  Polisi bado wanawasaka “magaidi” hao waliofanya shambulizi hilo katika klabu hiyo ya usiku ya Reina kwa saa 7:30 usiku kwa saa za hapa.

Hatahivyo, kwa saa kadhaa baada ya shambulio hilo, mamlaka za taifa zilikuwa kimya kuhusu suala hilo.

Watu wengine 69 walipatiwa matibabu hospitalini, alisema waziri huyo.

"Usakaji wa magaidi hao bado unaendelea…Natarajia (washambuliaji) watakamatwa haraka kwa mapenzi ya Mungu, “ alisema Soylu.

Mamlaka ya Uturuki imevizuia vyombo vya habari kuripoti shambulio hilo, lakini alizuii taarifa za viongozi.

Gavana wa Jiji la Istanbul, Vasip Sahin awali alibainisha kuwa ofisa wa polisi alikufa katika shambulio hilo.
Pia mshambuliaji mmoja alihusi, alisema gavana huyo, wakati Kituo cha Televisheni cha CNN cha Uturuki kiliripoti kuwa, mshambuliaji huyo alivalia vazi la Father Krismas .

"Magaigi wakiwa na silaha…walifanya vitendo vya kikatili ikiwemo kuwafyatulia risasi raia wema na watu wengine waliokuwa wakisheherekea  Mwaka Mpya na kucheza, “alisema Sahin alipozungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio katika eneo la Ortakoy.

Klabu hiyo sio maarufu tu kwa Waturuki, bali pia hata kwa wageni kutoka nje ya nchi, ambao walipenda kwenda kula bata, kwa mujibu wa Mtangazaji wa Shirika la Utangazji la Uingereza la BBC, Selin Girit jijini Istanbul.

Aliongeza kuwa watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa washambuliaji walikuwa wawili.
Iliripotiwa kuwa ndani ya klabu hiyo ya usiku kulikuwa na watu zaidi ya 700 wakati shambulio hilo likitokea, ambapo baadhi yao walirukia katika maji ili kujiokoa.

Shirika la Habari la Dogan liliriopit kuwa baadhi ya mashuhuda walidai kuwa baadhi ya washambuliaji hao walikuwa “wakizungumza Kiarabu” wakati channeli ya Televisheni ya Uturuki ya NTV ilisema polisi maalum walikuwa wakipekuwa klabu hiyo ya usiku.

Rais wa Marekani Barack Obama, ambaye yuko katika mapumziko huko Hawaii, ni miongoni mwa viongozi wa kwanza wa kimataifa kutoa taarifa baada ya kutaarifiwa na timu yake.

"Rais ametuma salamu za rambirambi kwa kupotea kwa maisha ya watu wasio na hatia…”ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Obama iliyotolewa na msemaji wa Ikulu ya Marekani Eric Schultz.

Serikali ya Uturiki imetoa amri ya kuzuia kwa muda vyombo vya habari vya hapa kuripoti taarifa hizo, kutokana na suala la kiusalama.

Hii sio mara ya kwanza kwa amri kama hiyo kutolewa.

Istanbul ilikuwa katika hali ya taadhari huku kukiwa na askari polisi zaidi ya 17,000 wakiwa kazini jijini hapa, kufuatia kuwepo na matukio kadhaa ya kivamizi katika miezi ya hivi karibuni.

Vitendo vingi vya kigaidi vimekuwa vikifanywa na Dola ya Kiislamu (IS) na wale wanaofahamika kama askari wa Kikurdi.

Chini ya wiki mbili, Balozi wa Urusi nchini hapa,  Andrei Karlov, aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Uturuki ambaye hakuwa kazini Mevlut Mert Altintas wakati akihutubia katika jiji la Ankara mwezi uliopita.

Baada ya mauaji hayo muuaji alikuwa akipiga kelele kuwa kitendo hicho ni kulipa kisasi kwa Urusi kujiingiza katika mgogoro katika jiji la Syria la Aleppo.

Mashambulizi makubwa Uturuki kwa mwaka 2016

Desemba 10: Mashambulizi mawili ya mabomu yalifanyika nje ya uwanja wa soka jijini Istanbul na kuua watu 44, kundi la askari wa Kikurdi walidai kuhusika ba tukio hilo.

Agosti 20: Shambulizi la bomu katika sherehe ya harusi huko Gaziantep liliua watu 30, huku kundi la IS likihisiwa kuhusika.

Julai 30: Wapiganaji 35 wa Kikurdi walijaribu kuvamia ngome ya kijeshi na kujikuta wakiuawa na Jeshi la Uturuki.

Juni 28: Shambulio la risasi na bomu katika uwanja wa ndege wa Ataturk jijini Istanbul viliua watu 41, katika shambulio lililodaiwa kufanywa na askari wa IS.

Machi 13: Watu 37 waliuawa na askari wa Kikurdi katika bomu kurushwa katika gari jijini Ankara.
Februari 17: Watu 28 walikufan katika shambulio jijini Ankara.