Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kabla ya kuanza kwa mbio za kilometa 10 za mashindano ya wazi ya taifa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha leo. |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MASHINDANO ya wazi ya taifa ya riadha ya Ngorongoro ‘Ngorongoro National Open Athletics Championships’ yamefanyika
leo jijini Arusha na kushuhudiwa na watazamaji kibao waliofika kwenye Uwanja
wa Sheikh Amri Abeid huku wanariadha wa Arusha wakitamba.
Tofauti na mashindano hayo yanapofanyikia jijini Dar
es Salaam, leo uwanja huo ulikuwa na watazamaji kibao walioshuhudia wanariadha wao, wengi wakitokea Arusha wakitamba katika mbio na michezo mbalimbali.
Mashindano hayo yalidhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa mara ya kwanza katika mashindano ya taifa yalishirikisha mbio za barabarani za kilometa 10 badala ya zile za uwanjani za meta 10,000, ambazo jana hazikuwepo.
Katika mbio za kilometa 10, Jackson Mwakombe alimaliza
wa kwanza kwa kutumia dakika 32:00.22, baada ya kuongoza kwa muda mrefu mbio
hizo akiwaacha wenzake mbali.
Wanariadha wakichuana katika mbio za meta 5,000 za mashindano ya wazi ya taifa jijini Arusha leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. |
Arusha pia ilitwaa medali ya dhahabu katika kilometa
10 kwa wanawake wakati Neema Kisuda alipomaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 40:01.04
akifuatiwa na wanariadha wengine wa Arusha, ambao ni Gloria Makula na Sarah
Hiti waliomaliza katika nafasi ya pili na tatu kwa dakika 40:27.98 na 41:26.91.
Benjamin Michael alimaliza wa kwanza kwa kutumia
sekunde 10:99, huku Laurent Masatu na Bakari Barnabasi wote wa Arusha
wakimaliza katika nafsi ya pili na tatu kwa kutumia sekunde 11:10 na 11:18.
Mwanariadha kipita mbele ya bango la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambao ni wadhamini wa mbio za wazi za taifa zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. |
Katika mbio za meta 800, Mariam Salim, Grace Jackson
na Shamin Ramadhani wote wa Arusha walimaliza kwa dakika 2:18.09, 2:20.72 na
2:21.87 na kushika nafasi ya kwanza, ya pili na tatu kwenye Uwanja wa Sheikh
Amri Abeid.
Kwa upande wa meta 5,000 wanawake, Arusha ilishika
nafasi mbili za kwanza pale, Natalia Elisante na Angelina Daniel walimaliza wa
kwanza kwa kutumia dakika 16:54.52 na 17:18.80 huku Angelina John wa Singida
akimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 18:10.68.
Katika mbio za meta 800 kwa wanaume, mwanariadha wa
Manyara Gabriel Geay alitamba baada ya kumaliza wa kwanza kwa kutumia dakika
1:50.75 huku akifuatiwa na Faraja Damas na Simon Francis wote wa Arusha
waliotumia muda wa dakika 1:52.28 na 1:52.68.
Washindi wa kwanza katika kila mchezo wa mashindano
hayo yaliyodhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, waliondoka na Sh
150,000 kila mmoja wakati wale walioshika nafasi za pili kila mmoja alipata
100,000 na watatu Sh 50,000.
Watoto nao walichuana katika mbio za meta 100 wakati wa mashindano hayo ya wazi ya taifa leo Sheikh Amri Abeid. |
Washindi wa kwanza wa michezo yote kuanzia ile ya kilometa 10, meta 5,000, meta 100, meta 800, kuruka chini, meta 400, meta 1500, meta 200 na wale wa kupokezana vijiti, wote kesho watatembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, ikiwa ni ofa kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo.
Wanariadha wakike wakichuana katika mbio za meta 5,000. |
No comments:
Post a Comment