Tuesday, 31 July 2018

Waziri Kamwelwe akagua ujenzi Terminal 3 JNIA na kumtaka Mkandarasi Kiwanja cha Msarato kuwasilisha nyaraka Tanroads

Sehemu ya Jengo jipya la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 linavyoonekana kwa mbele.

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI  wa Ujenzi, chukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ametoa siku saba kwa Mhandisi mshauri katika ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Msalato Jijini Dodoma, kuwasilisha kwa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) nyaraka zote zinazohusu mradi huo kabla ya kuianza kazi aliyopewa.

Kamwelwe aliyasema hayo wakati alipotembelea alipotembelea ujenzi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya mafunzo tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli siku 11 zilizopita.
WAZIRI  wa Ujenzi, chukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe (kushoto) akisalimiana na Mhandisi Simba Bogohe wakati alipofanya ziara katika Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Juliue Nyerere. Kulia ni kaimu mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha.

Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais aliyetaka Tanroads kupewa usimamizi katika majukumu yote yanayohusu ujenzi.

Alisema hatua hiyo pia imelenga kwenda haraka na agizo jingine la juzi kutaka ujenzi wa kiwanja hicho kuanza mara moja, ili kuharakisha maendeleo ya Jiji hilo la Makao Makuu ya nchi, linaloanza kukua kwa kasi baada ya Serikali kuhamia huko rasmi hivi karibuni.

“Nina taarifa kuwa tayari TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania) mmeingia mkataba na mhandisi mshauri wa ujenzi wa kiwanja cha Msalato, hivyo natoa siku saba nyaraka zinazohusu ziwe zimepelekwa Tanroads kama mtu mwenye dhamana katika ujenzi wa uwanja huo,” alisema.
WAZIRI  wa Ujenzi, chukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere, Paul Rwegasha.

Pia aliipongeza Tanroads kwa kusimamia vizuri ujenzi wa jengo hilo la abiria la Terminal 3, hatua aliyoitaja kuwa ni moja ya mipango ya Serikali kuona taasisi zake zinasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili kuendana na kasi ya maendeleo kuelekea nchi ya uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Aidha, Waziri Kamwelwe alisema Serikali imeridhishwa na ujenzi wa uwanja huo ambao ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Mei mwakani na kutoa fursa ya utatuzi wa changamoto ya muda mrefu la ufinyu na uhaba wa sehemu ya kiwanja cha ndege cha JNIA.
WAZIRI  wa Ujenzi, chukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe akitaniana na Meneja Mradi wa ujenzi wa jengo hilo la Terminal 3, Wolfgan Marschick.

“Tunampongeza mkandarasi anayejenga mradi huu, anafanya kazi nzuri nasi kama Serikali tumekuwa macho kufuatilia usiku na mchana bila hata ya kuchoka ili tuweze kufikia malengo, aliongeza.
Meneja wa Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama akimuonesha mchoro wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere Waziri Kamwelwe.

Alisema ujenzi wa uwanja huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria zaidi ya 2800 kwa saa na Milioni 6 kwa mwaka na hivyo kutatua changamoto iliyokuwepo kwa kiasi kikubwa.
WAZIRI  wa Ujenzi, chukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe (katikati mstari wa mbele) baada ya kumaliza ziara ya kutembelea Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere.
 Awali, Mkurugenzi wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo, Wolfgang Marschick  mbali na mambo mengine  alimueleza Waziri kuwa moja ya changamoto anayokabiliana nao katika kutekeleza majukumu yake kuwa ni  kukwama kwa baadhi ya vifaa vya ujenzi katika Bandari ya Dar es Salaam,

Waziri alianza kulishughulikia suala hilo pale pale, ambapo alipiga simu kwa wahusika ili kuhakikisha vifaa hivyo, ambavyo alisema ni vidogo dogo lakini muhimu katika kukamilisha ujenzi huo vinatoka haraka ili kazi imalizike kwa wakati.
 

No comments:

Post a Comment