Monday, 10 October 2016

Costa, Nolito watupia Hispania ikiibuka na ushindi dhidi ya Albania katika mbio za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018




Timu ya taifa ya Iceland, ikipunga kwa mashabiki baada ya mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Uturuki jana huko Reykjavik, Iceland. Iceland ilishinda mabao 2-0.

MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Diego Costa na Nolito wa Manchester City walizifumania nyavu wakati Hispania ikiifunga Albania na kuongoza katika Kundi G katika mechi za mbio za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 kwa Kanda ya Ulaya.

Wachezaji wa Ligi Kuu ya England David de Gea, Nacho Monreal na David Silva wote waliichezea Hispania katika mchezo huo walioibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika kundi hilo hilo, Italia ilihitaji takribani dakika 91 ili kupata bao la ushindi lililofungwa na Ciro Immobile na kutoka nyuma na kuichapa Macedonia.

Mshambuliaji wa Lazio Immobile alisawazisha mapema kwa Italia wakati ilipocheza na timu inayoshikilia nafasi ya 146 katika viwango vya ubora wa soka duniani.

Kwingineko katika Kundi G, Israel iliifunga Liechtenstein 2-1 kwa bao la mshambuliaji wa Brighton Tomer Hemed alipofunga mabao yote mawili kwa wenyeji.

Mshambuliaji wa Newcastle United Aleksandar Mitrovic alifunga mara mbili, kabla ya kiungo wa Southampton Dusan Tadic hajapachika bao la ushindi, wakati Serbia ikiichapa Austria kwa mabao 3-2.

Kwa matokeo hayo, Serbia inaoongoza Kundi D ikiwa juu ya Jamhuri ya Ireland na Wales.

Croatia inaoongoza katika Kundi I baada ya mshambuliaji wa Juventus Mario Mandzukic kuipatia timu hiyo ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Finland.

Iceland ni ya pili kufuatia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata dhidi ya Uturuki na katika kundi hilo hilo, Ukraine iliichapa Kosovo 3-0.

Sunday, 9 October 2016

Nigeria, Misri, Tunisia zaanza vizuri mbio za kusaka nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2018



Mchezaji wa Zambia, Rainford Kalaba (kulia) akitafuta njia kumpita mchezaji wa Nigeria, Ogeny Onazi wakati wa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia Kanda ya Afrika uliofanyika Levy Mwanawasa jijini Ndola, Zambia jana. Nigeria ilishinda 2-1. Picha na Mtandao).

NDOLA, Zambia
NIGERIA imeanza kwa ushindi kampenzi zake za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 Kanda ya Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Zambia katika mchezo wa Kundi B uliofanyika hapa.
 
Kwa ushindi huo, Nigeria wanaoongoza katika kundi lao, baada ya vigogo wengine wa Afrika Algeria kubanwa na kulazimishwa sare na Cameroonin na kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Kwingine, Misri iliifunga Congo 2-1 katika mchezo wa Kundi E uliofanyika Brazzaville huku katika Kundi A, Tunisia ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Guinea.

Katika mchezo wa Nigeria, mabao yao yalipatikana katika kipindi cha kwanza yaliyofungwa na nyota wanaongara katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.

Mshmabuliaji wa Arsenal Alex Iwobi ndiye aliyeiweka mbele Super Eagles baada ya kufunga bao katika dakika ya 32.

Mshambuliaji wa Manchester City Kelechi Iheanacho aliongeza uongozi huo wa City dakika 10 baadae na kukiweka kikosi cha kocha Gernot Rohr kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Nigeria nusura ipate bao la tatu na ingeweza kuwa mbele kwa mabao 3-0 katika mchezo huo uliofanyika Ndola kama sio nahodha wake John Mikel Obi kukosa bao katika kipindi cha pili, baada ya kupiga shuti la mbali lililookolewa kifundi na kipa wa Zambia Kennedy Mweene.

Zambia ilipambana kiume na juhusi zake zilileta mafanikio pale ilipopata bao la kufutia machozi katika dakika ya 71 kupitia kwa Collins Mbesuma.

Pamoja na presha kutoka kwa timu mwenyeji, Nigeria iligangamala na kuendeleza rekodi ya ushindi ugenini na kuongoza katika Kundi B, likiwa ni moja ya makundi magumu katika mechi hizo za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Timu nyingine mbili katika Kundi B, Algeria, ilimchezesha mchezaji wake anayekipiga Leicester City, Riyad Mahrez na Islam Slimani, wakati ikicheza na Cameroon na kutoka sare ya bao 1-1.

Muargeria El Arabi Soudani aliiweka mbele timu yake katika mchezo uliofanyika Blida, lakini yule wa Cameroon, Benjamin Moukandjo ilisawazishwa kabla ya mapumziko.

Pia katika mchezo mwingine uliofanyika Jumapili, Misri ilikwenda kileleni katika Kundi E kwa ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Congo Brazzaville, wakifuatiwa na suluhu ya Ghana nyumbani dhidiya Uganda katika mchezo uliofanyika Ijumaa.

Wenyeji waliuanza mchezo huo kwa nguvu wakati mchezaji wake anayecheza soka la kulipwa Ufaransa Ferebory Dore alipofunga bao la kuongoza kwa Congo Brazzaville katika dakika ya 24.

Hatahivyo, kikosi kabambe cha Misri kilijibu mapigo kwa mshambuliaji wake anayecheza soka la kulipwa Roma Mohamed Salah kusawazisha dakika nne kabla ya mapumziko na matokeo kuwa 1-1.

Katika dakika ya 58, Salah alibadili matokeo wakati alipomtengenezea mcherzaji wa Al Ahly, Abdallah El-Said aliyefunga na kufanya matokeo kuwa 2-1 kwa Misri.

Tunisia iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Guinea katika mchezo wa Kundi A huko Monastir uliofanyika baadae Jumapili.

Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Aymen Abdennour na Ahmed Akaichi yaliipatia timu hiyo ya Afrika Kaskazini ushindi ulioiweka katika nafasi ya pili katika Kundi A, nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliyoifunga Libya 4-0 Jumamosi.

Washindi watano wa makundi ndio watakaofuzu kwa ajili ya kuliwakilisha bara la Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Urusi mwaka 2018.

Timu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) yapania kufanya makubwa katika mashindano ya Shimiwi Dodoma 2016




Timu ya Wavuta Kamba wa TAA wakijifua katika mazoezi jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaendelea na mazoezi makali kujifua kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) yatakayofanyika Dodoma baadae mwezi huu.

TAA kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa katika mazoezi makali kujiandaa na mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika Dodoma kuanzia Oktoba 17 hadi 27 mwaka huu.
Timu ya Netiboli  ya  TAA ikifanya mazoezi kwenye uwanja wao jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA).
Timu hiyo inayotarajia kushiriki katika michezo ya netiboli, kuvuta kamba, soka, karata, bao, baiskeli na mingine, inajifua kwenye uwanja wao uliopo jirani kabisa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Timu ya netiboli inanolewa na mchezaji wazamani wa timu ya bandari na taifa, Taifa Queens, Judith Ilunda huku soka na kuvuta kamba nazo zikinolewa na makocha wenye uwezo mkubwa.

Kocha wa timu ya kamba ni Abunu wakati yule wa soka ni Kingley.
Timu ya  Soka ikifanya vitu vyake katika mazoezi yao kujiandaa na Shimiwi.
Bonanza la Uzinduzi wa Mashindano ya Shimiwi lilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi) Septemba 10 na kuhudhuriwa na wizara na taasisi mbalimbali za Serikali hapa nchini.
Mchezaji wazamani wa timu ya Bandari na timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, Judith Ilunda (mwenye fulana nyekundu) akiongoza mazoezi ya timu ya TAA wakijiandaa kwa ajili ya Shimiwi.
Mashindano ya Shimiwi yanafanyika mkoani Dodoma ili kuunga mkono agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la Serikali kuhamia katika makao makuu ya nchi.

Kingine ni kuwapa nafasi watumishi wa umma ambao hawajawahi kufika Dodoma kufahamu mazingira pia kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya kuhamia.