Friday, 3 November 2017
Naibu Waziri aridhishwa na maendeleo ya ujenzi TB III
SERIKALI imesema
ukusanyaji wa mapato unaofanywa kwa sasa ni muhimu kwani unaweza kuifanikisha
Tanzania kuwa na uwezo wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.
Kauli hiyo
imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi),
Elias Kwandikwa wakati alipotembea leo mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria au Terminal III la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Alisema serikali
inajenga awamu ya pili ya mradi huo kwa kutumia fedha za ndani, ishara ambayo
ni nzuri, kwani inaonesha kuwa katika siku za mbele serikali itakuwa na uwezo wa
kujenga miradi kwa kutumia fedha zake.
“Tunajenga mradi
huu kwa fedha zetu za ndani, lakini pia kwa kushirikiana na wdau wengine, hii ni
ishara nzuri kwamba sasa tunakokwenda tunao uwezo katika siku za usoni kuwa na
miradi kama hii kwa fedha zetu,” alisema Kwandikwa.
Alisema kwa sasa
hatua ya ujenzi wa mradi huo imefikia asilimia 66 na kwamba utakamilika
Septemba mwakani na kwamba baada ya ujenzi huo kukamilika itakuwa ni picha ya
kuelekea kwenye Tanzania mpya.
Kwandikwa alisema
mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Bam International imelipwa fedha zake na
kwamba wizara inahakikisha mkandarasi huyo anapata haki yake kwa wakati.
“Nilitembelea kule
KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), nikaona maendeleo ya ujenzi
kule na nikaridhishwa, nikatamani nije hapa, lakini nimefika hapa pia
nimeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea,” alisema.
Kwa upande wake,
Msimamizi wa Mradi huo, Barton Komba alisema, mkandarasi wa ujenzi huo
ameshalipwa fedha zake zote, hivyo kwa sasa hadai serikali na anafanya kazi
yake vizuri.
“Mpaka mwezi wa
tisa mwakani utakuwa umekamilika, lakini pia uwanja huu umezingatia watu wote
hata ndugu zetu wenye mahitaji maalumu, n uwanja uliozingatia viwango vya
kimataifa,” alisema Komba.
Tuesday, 31 October 2017
Tottenham, Real Madrid kuwania kutinga mchujo
LONDON, England
TOTTENHAM na Real
Madrid zinakutana kesho katika moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, huku kila
moja ikiwa na nafasi ya kufuzu kucheza kwa hatua ya 16 bora kutoka katika Kundi
H.
Timu yoyote itakayoshinda kesho inaweza kufuzu kucheza hatua hiyo, ambayo inajulikana kama raundi ya mwanzo
ya mtoano.
Tottenham Hotspur
FC na mabingwa watetezi Real Madrid zinakutana kwenye Uwanja wa Wembley, kila
moja ikijua umuhimu wa mchezo huo katika kusonga mbele katika mashindano hayo.
Baada ya timu hizo
kutoka sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika kwenye
Uwanja wa Santiago Bernabéu Hispania katika raudi ya tatu, timu hizo
zinalingana kwa pointi kileleni mwa msimamo wa kundi lao.
Timu hizo
zinalingana kila kitu katika msimamo wa kundi hilo, ambapo kila moja ina pointi
saba, huku Tottenham ikiongoza na kufuatiwa na Real.
Timu zinazofuata
katika msimamo wa kundi hilo, Borussia Dortmund na APOEL FC kila moja ina
pointi moja.
Tottenham
haijawahi kuifunga Madrid, ambapo imepoteza mechi tatu kati ya tano
walizokutana huko nyuma, huku wakitoka sare mara mbili.
Bao la kujifunga
la Raphaël Varane katika mchezo wao watatu ndio pekee, ambao Tottenham imewahi
kufunga ilipocheza dhidi ya Real Madrid katika dakika 450 walizocheza.
MECHI WALIZOKUTANA
Mchezo wa kwanza
wa Tottenham kukutana na Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ulikuwa
katika msimu wa mwaka 2010/11, ambao ulimalizika kwa Real kushinda 4-0 nyumbani
katika mchezo wa kwanza wa robo fainali.
Mabao hayo
yalifungwa na Emmanuel Adebayor katika dakika ya nne na 57 na mengine yaliwekwa
kimiani na Ángel Di María (72) na Cristiano Ronaldo (87), huku Tottenham
ikicheza muda mwingi wakiwa 10 baada ya Peter Crouch kutolewa nje baada ya
kupewa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 15.
Ronaldo ndiye
aliyefunga bao pekee katika mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye Uwanja wa
White Hart Lane wakati Merengues wakikamilisha ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya
Tottenham, ambayo ilikuwa na akina Gareth Bale na Luka Modrić, ambao wote
kwa sasa wapo Real Madrid.
MAN CITY VS NAPOLI
Mchezo mwingine wa
leo utakaovuta hisia za wapenzi wengi wa soka ni ule utakaowakutanisha vinara
wa Ligi Kuu ya England, Manchester City dhidi ya Napoli.
Manchester City
haijafungwa hata mchezo mmoja na imejikusanyia pointi tisa baada ya kushuka
dimbani mara tatu, inacheza na Napoli iliyopo katika nafasi ya tatu ikiwa na
pointi tatu tu.
Man City inataka
kushinda mchezo huo wa leo ili kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu
kwa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kutoka katika Kundi F.
MECHI ZINGINE
Mechi zingine kesho zitakuwa kati ya Beşiktaş itakayocheza
dhidi ya Monaco wakati Sevilla itaikaribisha
Spartak Moskva huku Shakhtar Donetsk ikipepetana na Feyenoord.
Mechi nyingine ni
Liverpool itakuwa na kibaruia kizito kwenye uwanja wake wa Anfield wakati
itakapoikaribisha Maribor huku Porto itacheza dhidi ya RB Leipzig,na Borussia
Dortmund watacheza na APOEL.
Makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya
Kundi F
| Pos | Team | P | W | D | L | GF | GA | GD | Pts |
| 1 | Manchester City | 3 | 3 | 0 | 0 | 8 | 1 | 7 | 9 |
| 2 | Shakhtar Donetsk | 3 | 2 | 0 | 1 | 4 | 4 | 0 | 6 |
| 3 | Napoli | 3 | 1 | 0 | 2 | 5 | 5 | 0 | 3 |
| 4 | Feyenoord | 3 | 0 | 0 | 3 | 2 | 9 | -7 | 0 |
Kundi G
| Pos | Team | P | W | D | L | GF | GA | GD | Pts |
| 1 | Beşiktaş | 3 | 3 | 0 | 0 | 7 | 2 | 5 | 9 |
| 2 | RB Leipzig | 3 | 1 | 1 | 1 | 4 | 5 | -1 | 4 |
| 3 | Porto | 3 | 1 | 0 | 2 | 6 | 6 | 0 | 3 |
| 4 | Monaco | 3 | 0 | 1 | 2 | 2 | 6 | -4 | 1 |
Kundi H
| Pos | Team | P | W | D | L | GF | GA | GD | Pts |
| 1 | Tottenham Hotspur | 3 | 2 | 1 | 0 | 7 | 2 | 5 | 7 |
| 2 | Real Madrid | 3 | 2 | 1 | 0 | 7 | 2 | 5 | 7 |
| 3 | Borussia Dortmund | 3 | 0 | 1 | 2 | 3 | 7 | -4 | 1 |
| 4 | APOEL | 3 | 0 | 1 | 2 | 1 | 7 | -6 | 1 |
BMT yaendesha mafunzo kwa walimu wa michezo
![]() |
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja. |
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Michezo
la Taifa (BMT) linaendesha mafunzo kwa walimu wa shule za
msingi na sekondari ili kuendeleza michezo nchini.
Katibu Mkuu wa
BMT, Mohamed Kiganja alisema jana kwa njia ya simu kuwa, kwa sasa mafunzo hayo
yako katika tarafa ya Ntebele wilani Kyela mkoani Mbeya.
Alisema kozi hiyo
inatarajia kumalizika Jumamosi, ambapo walimu 49 kutoka shule mbalimbali za
msingi na sekondari wanahudhuria mafunzo hayo.
Kiganja alisema
kuwa mafunzo yanayotolewa ni pamoja na yale ya ufundishaji soka, mpira wa wavu,
netiboli, riadha, mazoezi ya viungo na utawala katika michezo.
Alisema kuwa mbali
nay eye (Kiganja) wakufunzi wengine wa mafunzo hayo ya wiki mbili ni pamoja na
Danny Korosso, Richard Mganga na Damian Chonya, ambaye anafundisha netiboli.
Alisema baada ya
hapo mafunzo hayo yataendelea ama Songwe, Rukwa au Mtwara kutegemea na utayari
wa mahali husika kwa ajili ya mafunzo hayo.
Juganja alisema
kuwa wameamua kutoa mafunzo tarafani ili kuwapunguzia washiriki gharama za
nauli na malazi.
“Tumeamua
kuwafuata na kuendesha ya mafunzo ya michezo huko huko ili kuwapunguzia gharama
ya nauli na malazi, “alisema Kiganja.
Alisema tayari
mafunzo hayo yalishafanyika jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya walimu 80
walihitimu katika mafunzo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Monday, 30 October 2017
Kivumbi mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kesho
![]() |
Baadhi ya
wachezaji wa Basel ya Uswisi wakifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya
mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi kesho Jumanne.
|
ZURICH, Uswisi
RAUNDI ya nne ya
Ligi ya Mabigwa wa Ulaya hatua ya makundi inaendelea tena kesho, huku Bayern
Munich, Chelsea, Manchester United, Barcelona na Atletico Madrid ni miongoni
mwa timu zitakazoshuka dimbani.
Tayari kila timu
imeshacheza mechi tatu na leo na kesho zinakamiisha mechi nne kila moja na
kubakisha mbili ili kukamilisha hatua ya makundi kabla ya kufuzu kwa 16 bora au
hatua ya kwanza ya mtoano.
Timu mbili za
kwanza kutoka katika kila kundi zitakuwa zimefuzu kucheza hatua hiyo ya timu 16
bora.
BAYERN MUNICH
Bayern Munich
wanatarajia kukabiliana na Celtic iliyo tofauti kabisa katika mchezo wa Kundi B
utakaofanyika leo jijini Glasgow tofauti na kikosi walichocheza nacho awali,
ambacho walikifunga mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza Ujerumani.
Mshambuliaji Leigh
Griffiths anasema kuwa Celtic kwa sasa wako vizuri zaidi na mabingwa hao wa
Ujerumani wasitarajie kupata mteremko.
Kimsimamo, Celtic
wako katika nafasi ya tatu katika Kundi B, lakini sasa imefikia rekodi yao
waliyoiweka miaka 100 iliyopita ya kucheza mechi 62 za nyumbani bila kufungwa.
Timu hiyo inajua
kuwa itakuwa nje ya mashindano hayo endapo itapoteza mchezo huo na Paris
St-Germain (PSG) itakwepa kipigo cha nyumbani kutoka kwa Anderlecht.
"Mchezo utakuwa
tofauti kabisa hapa, hasa kutokana na mashabiki kuwa nyuma yetu, “ alisema
Griffiths.
"Katika
kipindi cha pili [mchezo wa ugenini] tulicheza vizuri zaidi. Tulitengeneza
nafasi kibao za kufunga mabao.
Endapo kikosi cha
kocha Brendan Rodgers kitatolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa leo,
watabaki kusaka nafasi ya tatu ili kufuzu kucheza Ligi ya Ulaya katika mechi
mbili za mwisho hatua ya makundi.
Rodgers alikuwa
kocha wa Liverpool F.C. kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 kabla ya kutua Celtic,
hivyo leo atakuwa akipambana na timu yake yazamani.
Nyumbani, Celtic
inaoongoza katika Ligi Kuu ya Scotland, lakini Griffiths anasema kuwa
walikatishwa tamaa kupoteza pointi mbili Jumamosi baada ya kulazimishwa sare ya
1-1 dhidi ya Kilmarnock.
Wakati winga
Patrick Roberts ataukosa mchezo huo dhidi ya mabingwa hao wa Ujerumani kutokana
na maumivu, kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes ana uhakika Robert Lewandowski
atakuwa fiti kwa mchezo huo.
Wakati huohuo,
beki wa kulia wa Ujerumani Joshua Kimmich anategemea timu yao itafuzu kwa hatua
ya 16 bora huku ikiwa imebakisha mechi mbili kabla ya kukamilisha hatua ya
makundi wakati watakaposafiri kwenda Glasgow.
CHELSEA DIMBANI
Kocha wa Chelsea,
Antonio Conte anasema kuwa anatumaini ataweza kumchagua kiungo N'Golo Kante kwa
ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Roma utakaofanyika
leo.
Kante aliumia
nyama za paja wakati akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa mapema mwezi huu na
alikosa mechi tano za awali za Chelsea, ikiwemo ile waliotoka sare ya 3-3
nyumbani dhidi ya Roma siku 11 zilizopita.
Kimsimamo Chelsea
inaongoza katika Kundi C ikiwa na pointi saba na inaweza kujihakikishia nafasi
ya kucheza hatua ya 16 bora endapo itapata ushindi katika mchezo wake huo wa
Italia leo.
Kocha Conte
anasema kuwa hawezi kuthubutu kumchezesha Kante endapo mchezaji huyo Mfaransa
hatakuwa fiti vya kutosha.
"Yeye (Kante)
anaweza kuwa tayari," alisema kocha huyo Muitalia wakati alipozungumza na
waandishi wa habari. Najua sana umuhimu wa mchezaji huyu. Nataka kuhakikisha
kuwa yuko tayari….”
Sare na Roma
katika Uwanja wa Stamford Bridge ilikuja baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu
kufungwa mfululizo na kuwaacha wakiwa pointi tisa tofauti na vinara Manchester
City.
Hatahivyo, ushindi
wa timu hiyo katika ligi dhidi ya Watford na ule wa Bournemouth na kuifunga
Everton katika Kombe la Ligi, kumeiongezea nguvu timu hiyo.
"Ulikuwa
ushindi mzuri (1-0 dhidi ya Bournemouth Jumamosi) kwa kujijengea kujiamini,
ushindi mzuri kabla ya mchezo mwingine mgumu dhidi ya Roma katika Ligi ya
Mabingwa wa Ulaya, “alisema.
"Ushindi
ulikuwa muhimu kutupa mwendelezo kushinda dhidi ya Watford, na Everton katika
(Kombe la Ligi), na sasa tunajiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Roma.”
Alvaro Morata
anatarajia kuanza katika mchezo huo wa leo, licha ya kutofunga katika mechi nne
tangu aliporejea kutoka katika maumivu ya nyama za paja aliyoyapata walipocheza
na kufungwa na Manchester City mwezi uliopita.
VINARA BARCELONA
Barcelona wenyewe
leo watakuwa dimbani kupepetana na Olympiakos Piraeus katika mchezo wa Ligi ya
Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi.
Barcelona ambao
wanashuka uwanjani leo huku wakiwa wanaoongoza katika kundi lao kwa kuwa na
pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu hadi sasa.
Mbali na kufanya
vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Barcelona pia inaongoza katika Ligi
Kuu ya Hispania ya La Liga ikiwa pointi nne dhidi ya Valencia iliyopo katika
nafasi ya pili.
MANCHESTER UNITED
Manchester United
leo wanashuka dimbani kucheza dhidi ya Benfica katika mchezo itakaofanyika
kwenye Uwanja wa Old Trafford ikiwa imeshinda mechi zake zote tatu na
kujikusanyia pointi tisa.
Katika ligi ya
nyumbani, Manchester United iko katika nafasi nzuri kwani iko nyuma ya vinara
wa Ligi Kuu ya England Man City.
MECHI ZINGINE LEO
Leo Oktoba 30
mechi zingine zitakazofanyika ni ile ya Atlético Madrid itakayokuwa mwenyeji wa
Qarabağ katika mchezo utakaofanyikia kwenye Uwanja
wa Wanda Metropolitano, Sporting CP itaikaribisha
Juventus katika mchezo
mwingine.
Nayo Basel
itakwaana na CSKA Moskva katika
mchezo mwingine wa mashindano hayo huku PSG watatoana jasho na Anderlecht
katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Parc des Princes.
Nyalandu atema ubunge na nyadhifa zote CCM
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Singida
Kaskazini, Lazaro Nyalandu (pichani), leo ametangaza rasmi kujiondoa katika Chama cha Mapinduzi
na kuomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo au Chadema.
Kauli hiyo ameitoa
leo, ambapo alisema anajivua nyadhifa zote alizonazo ndani ya Chama cha
Mapinduzi, ukiwemo Ubunge, mbao ameutumkia kwa zaidi ya vipndi vinne.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka Singida, chama hicho mkoa humo kimebainisha kufurahishwa na
hatua hiyo na kudai kuwa alikuwa mzigo jimboni kwake.
Nyalandu baada ya
kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge wa Singida Kaskazini na kuihama CCM,
alikiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumpokea.
Mwenyekiti wa CCM
mkoa wa Singida Martha Mlata, alisema pamoja na kwamba hajapata taarifa rasmi
za kujiuzulu ubunge na kuhama chama kwa Nyalandu, amefurahi kama itakuwa ni
kweli mbunge huyo ameachia nafasi ya ubunge.
“Mimi kama
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida nafurahi kama kweli ameondoka, kwa sababu kwa
kweli alikuwa ni mzigo ndani ya chama. Nimeteseka sana kuliweka jimbo lake
vizuri,” alisisitiza Mlata.
Alisema mbunge
huyo alikuwa hatimizi majukumu yake ya kibunge ndani ya jimbo lake, hafanyi
ziara zozote jimboni wala kuhudhuria vikao vya Bunge.
“Niseme ukweli
tumefurahi na nina uhakika hata vijana wetu kule jimboni kwake wamefurahi.
Afadhali maana ametusaidia kumpata mtu atakayelitendea haki jimbo lile,”
alisema.
Awali, wakati
akitangaza kuhama chama chake na kujiuzulu nafasi ya ubunge jijini Arusha leo,
Nyalandu alisema ameamu kujiuzulu nafasi
zake zote ndani ya chama hicho ikiwemo ujumbe wa Halmashauri Kuu pamoja na
nafasi zote za uongozi ndani ya Chama hicho.
Pia alisema tayari
amemwandikia Spika wa Bunge Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yake ya
ubunge aliyoitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu alipochaguliwa kwa mara
ya kwanza mwaka 2000 hadi sasa.
Alisema
amechukua uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa kwake na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa
ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu.
Aidha, alitaja sababu
nyingine kuwa ni ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya
watanzania wenzake na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola
(Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga
sheria na kuisimamia serikali kutokuwa uhuru.
“Najiuzulu nafasi zangu zote na naomba Chadema
wanipokee kwa mikono miwili na pia natoa fursa kwa wananchi wachague mtu
wanayemtaka mara uchaguzi
utakapotangazwa, lakini kwa sasa nakihama Chama cha Mapinduzi, “alisema.
Subscribe to:
Posts (Atom)










