Wednesday, 11 January 2017

Waziri Nape ampongeza Diamond Platnumz kupata nafasi ya kutumbuiza ufunguzi wa Afcon Gabon na ameishukuru Multchoice kutoa tiketi




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kushoto) akimkabidhi bendera ya taifa Diamond Platnumz wakati wa hafla ya kuaga iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice- Tanzania, Salum Salum (kulia) na Msanii Joti.

 Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amempongeza mwanamuziki wa Tanzania Nassib Abdul au Diamond Platnumz kwa kupata nafasi ya kutumbuiza katika ufunguzi wa fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon.
Nape pia ameipongeza Multchoice-Tanzania kwa kutoa tiketi sita kumuwezesha Diamond na wasanii wake kwenda Gabon kutumbuiza katika ufunguzi wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchi humu kuanzia Jumamosi Januari 14 hadi Februari 15, ambapo timu kutoka Mataifa 16 zitatifuana katika patashika hiyo.
 
Nape akizungumza katika hafla ya kumkabidhi bendera ya taifa Diamond jijini Dar es Salaam jana katika hoteli ya Serena alisema kuwa, kitendo cha msanii huyo kwenda kutumbuiza katika ufunguzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania.

Alimtaka Diamond kuliwakilisha vizuri  taifa licha ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kutopata nafasi ya kushiriki fainali hizo.
 
Nape pia aliishukuru Multchoice-Tanzania kwa kukubali kuwapatia tiketi sita wasanii wa Diamond ili kwenda kunogesha shoo hiyo ya mwanamuziki huyo mwenye mafanikio makubwa nchini.

Alisema nafasi ya Diamond angeweza kupewa msanii mwingine yoyote nyota kutoka katika nchi zinazojiita mahiri katika tasnia hiyo, na badala yake alipewa Mtanzania huyo.

Alisema hiyo ni fursa kubwa kwa Diamond kuitangaza Tanzania kimataifa katika muziki.

Naye Diamond alimshukuru Nape kwa kupiga hodi Multchoice na kuwaombea tiketi wasanii wake.

Kaimu Mkurugenmzi Mtendaji wa Multchoice- Tanzania, Salum Salum alisema Afcon ni uhondo mwingine kwa Watanzania kwani DStv ndio chaneli pekee itakayoonesha fainali hizo.

Alisema Diamond ataendelea kupata nafasi za kutumbuiza katika hafla mbalimbali za michezo na alimtakia heri ili siku moja aje kutumbuiza katika fainali za Kombe la Dunia.
Kaimu Mkurugenzi wa Multchoice-Tanzania, Salum Salum.
 “DStv ndio itakuwa chaneli pekee yenye ruksa ya kuonesha fainali hizo za Afco Tanzania na TV nyingine yeyote ikionesha hapa nchini itakuwa inaiba matangazo, “alisema Salum.
Wiki iliyopita Diamond alipata fursa ya kutumbuiza wakati wa utoaji wa tuzo za wachezaji bora wa mwaka wa Afrika zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) zilizofanyika Abuja, Nigeria.

Katika uzinduzi huo, Diamond ataimba kibao maalum pamoja na wasanii Mohombi na Franco, kiba ambacho pia kitakuwa wimbi wa mashindano hayo.

 

 

 

Tuesday, 10 January 2017

Simba yaifungisha virago Yanga Kombe la Mpinduzi, sasa kucheza na Azam FC Ijumaa



Na Mwandishi Wetu
SIMBA imefanikiwa kuifunga Yanga kwa penalti 4-2 katika mchezo wa Kombe la Kombela Mpinduzi na sasa itakwaana na Azam FC katika fainali itakayofanyika Ijumaa kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.


Azam ilitinga mapema fainali baada ya kuifunga Taifa Jang'ombe kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo katika majira ya saa 10 jioni.
 
Domayo alifunga bao hilo dakika ya 33 kwa shuti la umbali wa kama mita 19, baada ya kuwazidi mbinu viungo wa Taifa Jang’ombe, ambapo sasa watacheza na Simba katika mchezo utakaofanyika Ijumaa.

Hatua hiyo ya penalti ilifikiwa baada ya Simba na Yanga kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida katika mchezo huo wa nusu fainali uliohudhuriwa na umati wa watazamaji.


Penalti za Simba zilifungwa na Nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Muzamiru Yassin na beki Mkongo Janvier Besala Bokungu, wakati kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alikosa penalti yake huku akifanikiwa kuokoa shuti la Mzimbabwe Method Mwanjali.

Waliofunga penalti kwa upande wa Yanga ni pamoja na Simon Msuva na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko wakati kipa Mghana wa Simba, Daniel Agyei aliokoa penalti za Dida na Mwinyi Hajji Mngwali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi wa Zanzibar, Mfaume Ali Nassor, aliyesaidiwa na washika vibendera Mgaza Ally na Mbaraka Haule, Waziri Sheha mezani chini ya usimamizi  wa Ramadhan Nassor, ambapo timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Pamoja na kuonekana kuingia uwanjani, kinyonge baada ya kufungwa 4-0 na Azam FC Jumamosi katika mchezo wa mwisho wa kundi A,  Yanga ilifanikiwa kuwazidi Simba katika dakika 45 za mwanzo.

Yanga tena wakalijaribu lango la Simba dakika ya 15, baada ya winga Simon Msuva kupiga mpira uliorudi kufuatia pigo la mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kuokolewa, lakini kipa Agyei akaokoa tena akishirikiana na beki Method Mwanjali.

Simba wakajibu dakika ya 16 baada ya kiungo Mohammed Ibrahim kupiga shuti kali lililodakwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Msuva tena akakaribia kufunga dakika ya 36 baada ya kumtoka kwa chenga nzuri beki wa kulia wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kumlamba chenga ya mpira wa kichwa kipa Agyei, lakini alipobinuka ‘kibaiskeli’ kwa pigo dhaifu lililokuwa linaelekea nyavuni, beki Janvier Besala  Bokungu akatokea na kuokoa.

 Vikosi vilivyoanza:


Yanga; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Saidi Juma ‘Makapu’, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke.
Simba: Daniel  Agyei, Janvier Bokungu, MOhammed Hussein 'Tshabalala', Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei, Juma Luizio, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim.

Friday, 6 January 2017

Azam FC ikizubaa tu kwa Yanga imekula kwao njia nyeupe kupanda boti kurudi Chamazi kujiandaa na Ligi Kuu Bara



Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki Azam FC ya Tanzania Bara italazimika kuifunga Yanga ili kutinga nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kutoka suluhu na Jamhuri juzi.

Azam FC ilijikuta ikiambulia pointi moja baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Jamhuri ya Pemba katika moja ya mechi za mashindano hayo kwenye Uwanja wa Amaan hapa.

Wakati Azam wakisubiri `huruma’ ya Yanga, mabingwa hao wa Tanzania Bara (Yanga), wenyewe tayari wameshakata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya juzi kuifunga Zima Moto kwa mabao 2-0.

Kimsimamo, Yanga wana pointi sita baada ya kushinda mechi mbili wakati Azam wenyewe mkononi wanashikilia jumla ya pointi mbili tu.

Nahodha wa Azam FC, John Bocco alisema baada ya mchezo huo dhidi ya Jamhuri kuwa, Yanga ni timu kubwa na wana kazi ngumu watakapokutana nao kesho kwenye Uwanja wa Amaan.

Endapo Azam FC itashindwa kuifunga Yanga itakuwa katika hali tete ya kucheza nusu fainali ya mashindano hayo na huenda ikapanda boti na kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda kupisha mashindano hayo.

“Tunawaheshimu Yanga kwa kuwa ni timu kubwa. Tunajua nasi ni timu kubwa na bora, itakuwa mechi ngumu sana.

“Lakini tunaiweka kando mechi ya leo na tunaanza maandalizi kwa ajili ya mechi ijayo kujiandaa dhidi ya Yanga,” alisema.

Jamhuri ilichapwa mabao 6-0 na Yanga, hivyo kuondoka na pointi moja mbele ya Azam hakuna shaka kuwa matokeo hayo yatakuwa ni faraja kubwa sana kwao.

Pambano hilo la Yanga na Azam FC litafanyika kwenye Uwanja wa Amaan kuanzia 2:30 usiku.

Timu ya Afcon ya Zimbabwe yabebwa na wachezaji wanaocheza soka nchini Afrika Kusini



HARARE, Zimbabwe
NYOTA Khama Billiat na kiungo mwenzake na nahodha Willard Katsande ni miongoni mwa wachezaji nane wanaocheza soka Afrika Kusini ambao wameitwa katika kikosi cha Zimbabwe kitakachoshiriki Afcon 2017 Gabon.

Zimbabwe katika mashindano ya mwaka huu imepangwa katika Kundi B, ambapo watacheza na mabingwa wazamani Algeria na Tunisia, na Senegal, wakati timu mbili za juu zitatinga robo fainali.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Zimbabwe kushiriki fainali hizo, ambazo walitolewa katika raundi ya kwanza nchini Tunisia mwaka 2004 na kupata pigo kama hilo nchini Misri miaka miwili baadae.

Mshambuliaji wa pembeni Billiat alikuwa mchezaji muhimu aliyeisaidia timu ya Afrika Kusini ya Mamelodi Sundowns wakati iliposhina taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa mara ya kwanza mwaka jana.

Pia mchezaji huyo alikuwa mmoja kati ya wachezaji watatu waliofikia hatua ya mwisho ya kumsaka mchezaji bora wa Afrika wa mwaka, ambapo Mualgeria  Riyad Mahrez ndiye aliyeshinda mjini Abuja juzi.

Katsande kutoka klabu maarufu Soweto ya Kaizer Chiefs naye alifanya kazi kubwa, baada ya kujipanga mbele ya mabeki wakati katika ushambuliaji.

Kikosi Kamili cha Zimbabwe
Makipa: Donovan Bernard (How Mine), Takabva Mawaya (ZPC Kariba) na Tatenda Mkuruva (Dynamos).
Mabeki: Teenage Hadebe, Lawrence Mhlanga (wote kutoka Chicken Inn), Onismor Bhasera (SuperSport Utd/Afrika Kusini), Bruce Kangwa (Azam/Tanzania), Oscar Machapa (V Club/Ivory Coast), Elisha Muroiwa (Dynamos), Costa Nhamoinesu (Sparta Prague/CZE), Hardlife Zvirekwi (CAPS Utd).

Viungo: Kudakwashe Mahachi, Danny Phiri (wote wa Golden Arrows/Afrika Kusini), Khama Billiat (Mamelodi Sundowns/Afrika Kusini), Willard Katsande (Kaizer Chiefs/Afrika Kusini,nahodha), Marvelous Nakamba (Vitesse Arnhem/Uholanzi),

Washambuliaji: Tinotenda Kadewere (Djurgardens/Sweden), Cuthbert Malajila (Wits/Afrika Kusini), Nyasha Mushekwi (Dalian Yifang/China), Knowledge Musona (Ostend/Ubelgiji), Tendai Ndoro (Orlando Pirates/Afrika Kusini), Evans Rusike (Maritzburg/Afrika Kusini), Mathew Rusike (CS Sfaxien/Tunisia)
Kocha wa kikosi hicho ni Kallisto Pasuwa.