Sunday 30 October 2016

TP mazembe yakaribia taji la Shirikisho la Afrika baada ya kuilazimisha sare Mo Bejaia


Mchezaji wa Bejaia, Issama Mpeko (kushoto) akigombea mpira na mchezaji wa TP Mazembe, Mohamed Yacine Atmani wakati wa mchezo wa kwanza wa fainali wa mashindano ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Stade Mustapfa Tchacher, Blida, Algeria. Timu hizo zilifungana 1-1.

ALGIERS, Algeria
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la Shirikisho la Afrika baada ya kutoka sare dhidi ya Mouloundia Olympique de Bejaia katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika mjini hapa.

Mabingwa hao wazamani wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo wa Shirikisho kufuatia sare hiyo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Mustapha Tchaker El Bouleïda mjini Blida juzi usiku.

Mabao hayo yalifungwa katika kila kipindi kupitia kwa Jonathan Bolingi na Faouzi Yaya yaliviwezesha vigogo hivyo kila mmoja kuondoka na pointi moja.

Kwa sare hiyo, TP Mazembe inahitaji suluhu au ushindi wa aina yoyote ili kutangaza ubingwa wa mashindano hayo ya Afrika.

Yacine Athmani nusura afunge bao mwanzoni mwa mchezo huo baada ya kupiga shuti la mbali, lakini lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Sylvain Gbohouo katika dakika tatu tangu kuanza kwa mchezo huo.

Ingawa timu zote zilijaribu kuzifumania nyavu ndani ya dakika 30, lakini walikuwa wageni Mazembe ndio waliweka presha kwa wenyeji wao Mo Bejaia.

Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya mchezo kuwa mapumziko, wageni walifanikiwa kufunga bao lao la kwanza kupitia kwa Bolingi kwa penalti. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizka, ubao ulionesha 1-0 kikosi cha Hubert Velud kikiongoza.

Hatahivyo, baada ya kurejea uwanjani, nahodha wa Bejaia, Yaya aliwafungia bao wenyeji la kusawazisha katika dakika ya 66.

Mchezo wa Marudiano umepangwa kupigwa Jumapili Novemba 6 kwenye Uwanja wa Stade du TP Mazembe jijini Lubumbashi ili kumpata bingwa.

Mazembe iliwahi kuifunga Bejaia mara moja nyumbani mwaka huu, 1-0 katika hatua ya makundi, huku mchezo uliopita uliofanyika Algeria ulimalika kwa suluhu.

Mazembe imeshinda mara tisa taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika lakini haijawahi kushinda taji la Shirikisho, ambapo mshindi ataondokana kitita cha dola za Marekani 660,000 (sawa na sh bil 1.4) huku mshindi wa pili ataondoka na dola 462,000 (sh bil 1).

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika wenyewe mbali na fedha taslimu pia watawakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia.

Kidosho wa Kinondoni awa Miss Tanzania 2016 aondoka na gari na fedha taslimu


Miss Tanzania 2016 Diana Edward akipunga mkono akiwa pamoja na washindi wa pili na tatu, Grace Malikita (kushoto) na Mary Peter mara baada ya shindano hilo lililofanyika Rock City Mall  jijini Mwanza juzi. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Miss Kinondoni Dayana Edward ndiye mlimbwende wa Tanzania 2016 baada ya kuwashinda wenzake 29 katika viwanja vya Rock City Mall juzi usiku mkoani hapa. 

Mashindano hayo makubwa kabisa hapa nchini yaliamuliwa na majaji ambao ni Rita Mbelo,Catherine Kibaso,Sophia Masei,Raphael Siantini,Joe Makanyaga,Eliza Kilili,Juma Sultan,Prashant Patel na Ramesh Shah.

Mashindano hayo yalianza kwa warembo kucheza nyimbo mbali mbali kabla ya kutinga na mavazi ya ubunifu,ufukweni na vazi la jioni.

Jaji Shah aliweza kuwataja warembo walioingia 15 bora ambao ni Anna Nitwa,Sia Pius,Lisa Ndolo,Grace Malikita,Eunice Robert,Regina Ndimbo,Iluminata Dominic,Sporah Lulende na Maria Peter. 

Wengine ni Maureen Ayoub,Queen Nazir,Julietha Kabete,Maureen Kamanya na Abel John. 

Patel aliwataja warembo walioingia 5 bora ambao ni Grace Malikita,Anna Nitwa,Maria Peter,Julietha Kabete na Dayana Edward. 

Jaji Prashant Patel aliweza kutangaza warembo walioingia tatu bora, ambao ni Dayana Edward aliyeibuka mshidi, huku nafasi ya pili ikachukuliwa na Grace Malikita wakati Maria Peter alimaliza watatu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Annastazia Wambura aliomba mshindi wa shindano hilo ajitahidi kuzingatia nidhamu na uzalendo haswa pale atakapo wakilisha nchini katika mashindano ya mrembo wa dunia. 

Wambura alisistiza waandaji wa mashindano hayo waendelee kufuata taratibu za mashindano na kuhakikisha wanatekeleza mikataba waliosaini na warembo hao. 

Wambura ameomba mashindano hayo yafanyike katika mikoa mengine pia tofauti na hapa.

Dayana alikabidhiwa gari aina ya Toyota IST yenye thamani ya sh milioni 14.

Wednesday 26 October 2016

Mwenyekiti Riadha Zanzibar ajitosa kuwania ujumbe Kamati Olimpiki Tanzania (TOC)



Na Mwandishi Wetu
WAKATI wadau wa michezo Tanzania Bara wanasita kujitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Zanzibar kumekucha baada ya kiongozi mmoja wa michezo kukata utepe kwa kuchukua fomu.

Kiongozi huyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAA), Abdulhakim Cosmas kuchukua fomu leo akitaka ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC.

Rais wa TOC, Gulam Rashid amesema leo kuwa, Cosmas anawania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC.

Akizungumzia mchakato mzima wa kuchukua fomu ulioanza jana Jumanne, Rashid alisema kuwa unaendelea taratibu na wadau wengi wa michezo wanafika katika ofisi ndogo za TOC Zanzibar na kuchungulia na kuondoka.

Watu bado wanasuasua kwani baadhi yao wanakuja na kuondoka, alisema Gulam katika mahojiano maalum leo Jumatano.

Kwa upande wa Tanzania Bara, hadi leo jioni saa 10:00 wakati ofisi za TOC zilizoko Mwanyamala jengo la Biashara Complex zikifungwa hakuna mdau yeyote wa michezo aliyejitokeza kuchukua fomu yeyote.

Nafasi zinazowaniwa ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi, Mhazini Mkuu, Mhazini Msaidizi na wajumbe 10 wa Kamati ya Utendaji.